Na Magreth Kinabo na Tawani Salum- Mahakama
Jaji Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Meaza Mengistu amefurahishwa na utendaji kazi wa uwazi wa Mahakama ya Tanzania, ikiwemo huduma ya Mahakama inayotembea (Mobile Court) kwa kuwa hurahisisha hutoaji haki kwa wakati.
Mhe. Mengistu alitoa kauli hiyo leo wakati alipotembelea Mahakama inayotembea iliyokuwa ikitoa huduma kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, eneo Luguruni Mbezi na Mahakama ya Wilaya Kigamboni zilizopo jijini Dar es Salaam.
Jaji Mkuu wa Ethiopia alifurahishwa na Mahakama Inayotembea kwa jinsi inavyofanya kazi na kusema kuwa inasaidia kuondoa mlundikano wa mashauri, pia husaidia kutoa huduma za kimahakama sehemu ambazo hazina mahakama, ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya siku tatu.
‘‘Mahakama hii ni suluhisho tosha la umalizwaji wa mashauri ndani ya Mahakama’’ pia vifaa vilivyopo ndani kwa mfano kuwepo kifaa maalum cha kuwapandishia walemavu, Mahakama hii imezingatia wenzetu walemavu na kuwa ni ishara tosha kuwa sasa Mahakama imedhamiria kuwa karibu na wananchi,” alisema Jaji Mkuu huyo.
Aliongeza kuwa aliamua kufanya ziara hapa nchini Tanzania baada ya kuona kuwa Mahakama ya Tanzania ina maboresho makubwa hivyo basi hakuweza kujiuliza mara mbili kuja kutembelea Mahakama ya Tanzania hasa kutokana na kasi ya umalizwaji wa mashauri, ujengwaji wa mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo husaidia kumalizwaji wa mashauri kwa wakati.
“Nimefurahishwa na maboresho makubwa ya ujenzi wa mahakama kwa kutumia teknolojia ya moladi yenye gharama nafuu na uwepo wa mazingira rafiki, ukiwemo utendaji kazi wa uwazi’’ alisisitiza.
Naye Mhe. Moses Ndelwa ambaye ni Mratibu wa Mahakama Inayotembea, alisema Mahakama hiyo, imeendelea kusikiliza mashauri kwa ngazi ya Mahakama ya Mwanzo. Hivyo kwa upande wa jiji la Mwanza mashauri 57 yalifunguliwa na kutolewa uamuzi.
Aliongeza kwamba katika jiji la Dar es Salaam mashauri 92 yalifunguliwa na kusikilizwa. Pia mashauri yote yamesikilizwa na kutolewa uamuzi ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.
“Kwa mwananchi anayehitaji kufungua shauri la madai, anaweza kufungua katika Mahakama Inayotembea kama madai yake yanathamani isiyozidi shilingi milioni hamsini (Tzs. 50,000,000/=). Mashauri yanaweza kufunguliwa moja kwa moja katika gari la Mahakama Inayotembea au katika Mahakama ya Mwanzo inayopatikana karibu na kituo ambacho Mahakama Inayotembea inatoa huduma.
Ndelwa alifafanua kuwa imekuwa ikisikiliza mashauri ya jinai yanayotokana na operesheni maalumu, ambapo jumla ya watuhumiwa 184 walifikishwa katika Mahakama inayotembea, mashauri yalisikilizwa ndani ya siku moja na kutolewa uamuazi.
Alisema mbali na usikilizaji wa mashauri, Mahakama hiyo inatoa huduma nyingine kama vile kutoa fomu za kiapo, kuthibitisha nyaraka mbalimbali, kutoa fomu za kufungulia mashauri, kutoa nakala za hukumu, kupokea malalamiko na kutoa vipeperushi pamoja na taarifa mbalimbali zinazohusu Mahakama.
Mpaka sasa takribani wananchi 97 wamepata huduma mbalimbali za kimahakama kupitia Mahakama Inayotembea.
Kwa upande wa Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni, Mhe. Agnes Mchome alisema Mahakama hiyo katika kipindi cha mwaka 2019 mashauri yaliyofunguliwa ni 318, yaliyotolewa uamuzi 250 na yaliyobakia ni 186.
Wakati huohuo, Jaji Mkuu huyo alipata fursa ya kuzungumza na baadhi ya viongozi na wanachama wa Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA) ambacho pia kinachohusisha Mahakimu na kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi wao.
Jaji Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Meaza
Mengistu (mwenye kitenge) akitoka katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ubugo iliyoko Mbezi
Luguruni, jijini Dar es Salaam wengine ni baadhi ya watalaamu kutoka Benki ya Dunia
na Viongozi wa Mahakama ya Tanzania.
Jaji Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Meaza
Mengistu (kushoto) akipata maelezo leo
kuhusu gari maalum la Mahakama
Inayotembea linavyofanyakazi kutoka kwa na Kaimu Mkurugenzi wa Menejimenti ya Usimamizi
wa Mashauri wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Victoria Nongwa mara baada ya kuwasili katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo iliyoko Mbezi
Luguruni, jijini Dar es Salaam.
Jaji Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Meaza
Mengistu (kushoto) akiuliza jambo leo baada kujifunza kuhusu Mahakama
Inayotembea inavyofanya kazi na kuhifurahia huduma hiyo mara
baada ya kuwasili katika ofisi ya Mkuu
wa ya Ubungo iliyoko Mbezi Luguruni,
jijini Dar es Salaam.
Jaji Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Meaza
Mengistu (aliyevaa kitenge) akipokewa na
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi, Mhe. Agnes Mchome wa Mahakama ya Wilaya ya
Kigamboni, baada ya kuwasili leo katika Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni na
Mahakama ya Mwanzo Kigamboni iliyopo
jijini Dar es Salaam. (aliyevaa gauni jeusi) ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt. na mwenye tai nyekundu ni Mtaalamu kutoka Benki ya Dunia, Bw. Wleed Malik.
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi, Mhe. Agnes Mchome wa Mahakama
ya Wilaya ya Kigmboni, jijini Dar
es Salaam, akitoa taarifa ya kuhusu utendaji kazi wa mahakama hiyo, kwa Jaji Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Meaza Mengistu (ambaye hayupo pichani) .
Jaji Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Meaza
Mengistu (aliyevaa kitenge) akiwa katika picha ya pamoja) na baadhi ya Viongozi wa Mahakama
ya Tanzania wakati alipotembelea leo Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni iliyopo jijini Dar es Salaam, ambapo alijifunza kuhusu
ujenzi wa Mahakama hiyo kwa kutumia gharama nafuu na yenye mazingira rafiki. (Kulia wa kwanza) ni Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Maboresho ya Mahakama ya Tanzania,
Mhe. Zahra Maruma, wa pili kulia ni Mtaalamu kutoka Benki ya Dunia, Bw. Waleed Malik, wa tatu kulia ni Mtaalamu kutoka Benki ya Dunia, Bi Clara Maghani. (aliyevaa shati la bluuni) ni Makamu wa Rais wa Mahakama Kuu ya Ethiopia, ambaye aliambatana na mgeni huyo, Mhe. Tesfaye Niwai, (wa kwanza kushoto) ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi, Mhe. Agnes Mchome wa Mahakama
ya Wilaya ya Kigamboni, jijini Dar
es Salaam.
Jaji Mkuu
huyo(aliyevaa kitenge) akiwa katika picha ya pamoja baadhi ya viongozi na wanachama wa Chama cha
Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA) ambacho pia kinachohusisha Mahakimu wakati aalipowatembelea leo kwa ajili ya kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi wao kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania.
Jaji Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Meaza Mengistu (kushoto) akizungumza jambo na wanachama wa TAWJA na kulia ni Mwenyekiti wa TAWJA, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Joaquine De. Mello. |
(Picha na Magreth Kinabo- Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni