Na
Mary Gwera, Mahakama
Jaji Kiongozi Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amewataka Mahakimu na
Watumishi wa Mahakama kwa ujumla kuendelea kuhudumia wananchi licha ya
changamoto ya janga la Ugonjwa wa ‘Corona’ unaoendelea kutikisa dunia kwa sasa.
Akizungumza kwa nyakati
tofauti alipotembelea Mahakama kadhaa jijini Dar es Salaam, Machi 31, 2020,
Mhe. Jaji Dkt. Feleshi alisema kuwa kila Hakimu ajikumbushe wajibu wake kwa
kusoma vifungu 107A na B vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
vilevile wakumbuke kusimamia viapo vyao.
“Kipindi kama hiki
hakisimamishi migogoro kutokea kwenye jamii, hivyo ni lazima kazi zifanyike, ni
kipindi ambacho kinatukumbusha ni namna gani bora zaidi ya kuboresha huduma ya
utoaji haki nchini,” alieleza Mhe. Jaji Kiongozi.
Mhe. Jaji Kiongozi
aliongeza kwa kuwataka Watumishi hao kuwa wabunifu katika maeneo yao ya kazi na
kutokubweteka kwa kusikiliza idadi chache ya mashauri kwa Mahakama ambazo zina
idadi chache ya mashauri na kuwataka Mahakimu kutosita kudai nyongeza ya idadi ya
mashauri ya kuyafanyia kazi endapo waliopangiwa na Wafawidhi wao ni machache.
Aidha; Mhe. Jaji Dkt.
Feleshi aliwataka Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya ya Kigamboni, Temeke
na Ilala kuendelea kuboresha ushirikiano na Wadau wa Mahakama katika suala zima
la kuhakikisha kuwa haki inatolewa kwa wakati.
Mhe. Jaji Kiongozi
amefanya ziara ya ukaguzi wa shughuli za Mahakama katika Mahakama za Wilaya za
Kigamboni, Temeke na Ilala, Mahakama za Mwanzo za Temeke, Mbagala, Ukonga,
Buguruni na Ilala na amefanya ukaguzi wa ujenzi wa Kituo Jumuishi cha utoaji
haki kinachojengwa Chang’ombe wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo; Mhe. Jaji
Kiongozi amewasifu Wafawidhi na Watumishi wote wa Mahakama alizotembelea kwa
kuunga mkono jitihada za Viongozi Wakuu wa Mahakama za kuhakikisha kuwa huduma ya haki nchini inatolewa kwa ubora kwa wananchi wote.
Mhe. Jaji Kiongozi
aliwataka baadhi ya Watendaji wa Mahakama alioambatana nao kushughulikia
changamoto zote zilizoibuliwa katika ziara yake ambazo ni pamoja na uhaba wa
watumishi kwa baadhi ya Mahakama hasa Kada za Wasaidizi wa Ofisi, Mlinzi na
Makarani, ufinyu wa bajeti na kadhalika.
Msimamizi huyo wa
Mahakama Kuu na Mahakama za chini 'surbodinate courts' anatarajia kuendelea na ziara yake ya Kanda
ya Dar es Salaam ambapo atatembelea pia Pwani na Morogoro lengo ni kuangalia
maendeleo ya utekelezaji wa huduma ya utoaji haki pamoja na kuangalia ni kwa
jinsi gani Kanda hii imechukua tahadhari za mapambano dhidi ya janga la ‘Corona’ katika kuhakikisha usalama wa Watumishi na wateja wa Mahakama.
Jaji Kiongozi Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (kulia) akizungumza na
Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Kigamboni alipotembelea Mahakama hiyo mapema Machi 31, 2020.
Hakimu Mkazi Mfawidhi,
Mahakama ya Wilaya Kigamboni, Mhe. Agnes Mchome (wa tatu kushoto) akifafanua
jambo kwa Mhe. Jaji Kiongozi pindi Mhe. Jaji Kiongozi alipotembelea Mahakama
hiyo mapema Machi 31, 2020. Kulia ni Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Dar
es Salaam, Mhe. Lameck Mlacha.
Tahadhari dhidi ya
Virusi vya ‘Covid-19’: Mhe. Jaji Kiongozi na Mhe. Jaji Mfawidhi wakinawa mikono
kabla ya kuendelea na shughuli ya ukaguzi katika Mahakama ya Wilaya ya
Kigamboni.
Mhe. Jaji Kiongozi
akiwasalimia Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke mara baada ya kuwasili
katika Mahakama hiyo.
Mhe. Jaji Kiongozi
(katikati) akiendelea na ukaguzi katika Mahakama ya Wilaya Temeke, kushoto ni
Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Lameck Mlacha na kulia
ni Naibu Msajili, Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Joseph Fovo.
Mhe. Jaji Kiongozi
akionyeshwa ramani ya jengo la Kituo Jumuishi cha utoaji haki kinachojengwa
Wilayani Temeke.
Mhe. Jaji Kiongozi na
baadhi ya Maafisa wa Mahakama alioambatana nao wakikagua ‘site’ ya ujenzi wa
Kituo Jumuishi cha Utoaji haki kinachojengwa Chang’ombe wilaya ya Temeke jijini
Dar es Salaam.
Mhe. Jaji Kiongozi
akiwasili Mahakama ya Mwanzo Mbagala kwa ukaguzi, katikati ni Hakimu Mkazi
Mfawidhi, Mahakama ya Wilaya Temeke, Mhe. Susan Kihawa na kulia ni Hakimu Mkazi
Mfawidhi, Mahakama ya Mwanzo Mbagala, Mhe. Florence Madelemo.
Ukaguzi Mahakama ya
Mwanzo Ukonga.
Ukaguzi Mahakama ya
Wilaya Ilala iliyopo Tabata Kinyerezi. Wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi
Mfawidhi, Mahakama Wilaya Ilala, Mhe. Martha Mpaze na baadhi ya Watendaji wa Mahakama
walioambatana na Mhe. Jaji Kiongozi.
Mhe. Jaji Dkt. Feleshi
akisalimiana na sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Buguruni.
Ukaguzi, Mahakama ya
Mwanzo Ilala.
(Picha na Mary Gwera,
Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni