Jumatatu, 30 Machi 2020

JAJI KIONGOZI ATAKA KESI ZA JINAI KUSIKILIZWA MFULULIZO


Na Magreth Kinabo- Mahakama

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi, amewataka Mahakimu kusikiliza kwa mfululizo kesi za jinai ili kupunguza msongamano wa mahabusu, na kuepukana na maambukizi ya Virusi vya Corona.

Jaji Kiongozi alitoa agizo hilo leo alipoanza rasmi ziara ya siku tano ya ukaguzi maalum, Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dar es salaam.

“Anzeni kusikiliza kesi za jinai mfululizo, itasaidia tusiwe na msongamano wa mahabusu, na wale wanaostahili dhamana  wapewe,  hatua hii itatuwezesha kujikinga na maambukizi ya  virusi vya Corona", alisema Jaji Kiongozi.

Aidha Jaji Kiongozi amewataka  watumishi wa Mahakama kuendelea kuepukana na vitendo vya rushwa na kuzingatia maadili ya kazi zao.
Dkt. Feleshi  pia amezipongeza Mahakama za Mwanzo kwa kutokuwa na mlundikano wa mashauri.

Katika ziara hiyo Jaji Kiongozi alikagua ujenzi wa jengo la Mahakama ambalo pia litajulikana kama Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki  kilichopo Kinondoni. Jaji Kiongozi pia alikagua  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Mahakama ya  Wilaya Kinondoni na Mahakama za Mwanzo za Sinza, Kinondoni,Kawe. Kimara, Magomeni na Kariakoo.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi (katikati) akikagua  ujenzi wa  jengo  la Kituo  Jumuishi  cha  Utoaji Haki (IJC) kilichopo Kinondoni. Kituo hicho  kinajumuisha Mahakama Kuu,  Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Mwanzo pamoja na ofisi za wadau wa Mahakama.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi (kulia) na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam( kushoto) wakinawa mikono ikiwa ni hatua ya kupambana na maambukizi  ya virusi  vinavyosababisha ugonjwa wa Corona  mara baada ya kuwasili  katika eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni na Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni leo Jijini Dar es Salaam. Jaji Kiongozi yuko katika ziara maalum ya kikazi kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.


Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Kariakoo akitoa taarifa ya utendaji wa Mahakama hiyo kwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi (hayupo pichani).

Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Kawe, Mhe. Mary Kassanga (kulia) akitoa taarifa ya utendaji kazi wa Mahakama hiyo kwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi (hayupo pichani).



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni