Na Innocent Kansha – Mahakama
Kamati ya Taifa
ya Mahakama Kuu ya Tanzania ya kusukuma mashauri ya Jinai imefanya kikao
chake cha kupitia maendeleo ya kesi za jinai ambazo hazijakamilika kusikilizwa
ndani ya siku 60 na zaidi, ili kutambua sababu za ucheleweshwaji na kuchukua
hatua stahiki za kiutawala kuharakisha usikilizwaji wa mashauri hayo.
Akifungua rasmi
kikao hicho mapema Aprili 03, 2020 kilichofanyika katika Kituo cha Mafunzo na
Habari kilichopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Dkt. Benhajj Masoud aliwataka wadau wote wa Haki Jinai kutambua
mchango wao wa moja kwa moja kupunguza msongamano na kuweka mazingira wezeshi
ya utoaji haki.
Aidha; Mhe. Jaji
Dkt. Benhajj aliwataka pia Wadau wa kikao hicho kuendelea na wajibu wa utoaji
haki kwa wote na kwa wakati licha ya changamoto ya ugonjwa wa corona.
“Ugonjwa huu ni
changamoto ambayo hatuna budi kuikabili kwa kutumia njia mbadala za
usikilizwaji wa mashauri mahakamani ili kuondosha mlundikano wa mashauri na
msongamano usio wa lazima,” alisema Mhe. Jaji Benhajj.
Mhe. Jaji huyo
aliwataka Wajumbe wa kikao hicho kushughulikia changamoto zilizopo kwa ngazi ya
kitaifa na kuwataka wadau wa Haki Jinai kutoa ushirikiano wa dhati kufanikisha
azma ya kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani hasa kwa ngazi ya mikoa na
wilaya.
“Matumizi ya
tehama kwa Mahakama na wadau hayakwepeki hasa katika kipindi hiki cha mlipuko
wa virusi vya corona vinavyosambaa kwenye mazingira ya msongamano kuna haja ya
mahakama na wadau wake kuongeza jitihada ambazo zilishawekwa kupitia kanuni za
kusajili mashauri kwa njia ya mtandao ‘E – Filing System’ kupitia Gazeti la
Serikali toleo na 148 la mwaka 2018,” alieleza.
Aliongeza kuwa, Mahakama
haiwezi kutimiza jukumu lake peke yake bila kuwepo na ushirikiano wa wadau wa
haki jinai katika kutoa ushauri na mwelekeo wa maagizo mbalimbali ya ngazi za
juu, changamoto kwa mahakama na hususani kwa kamati hii ili kutafakari na
kushauri namna bora ya kusukuma mashauri na kupunguza mlundikano.
Nae, Msajili wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmilla Sarwatt alisema lengo la kikao kazi
cha kusukuma mashauri ni kujadili namna ya kuendesha na kupunguza mlundikano wa
mashauri mahakamani hasa katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa virusi
vya corona.
Mhe. Sarwatt
alizitaja mbinu za kupunguza mashauri Mahakamani ikiwa ni pamoja na kuendesha
mashauri ya jinai kwa njia ya mtandao, utaratibu wa kupanga muda wa kusikiliza
kesi ili kuondoa msongamano usio wa lazima mahakamani na pia kusajili kesi
mahakamani pindi upelelezi unapo kuwa umekamilika.”
Akizungumzia umuhimu
wa kikao hicho, Mkurugenzi Msaidizi Upelelezi Makosa ya Jinai nchini, Bw.
Charles Kenyela aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kushirikisha wadau wa haki
jinai ili kutatua changamoto na kutafuta namna bora ya uendeshaji wa mashauri
hasa katika kipindi hiki cha mlipuko wa virusi vya corona.
Kamati ya
kitaifa ya kusukuma kesi inaundwa na wadau mbalimbali wa haki jinai ikiongozwa
na Mahakama Kuu ya Tanzania, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mkurugenzi
wa Makosa ya Jinai, Takukuru, Magereza, Uhamiaji, Chama cha Mawakili
Tanganyika, Idara ya ustawi wa jamii na wengineo.
Jaji wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Benhajj Masoud (aliyesimama mbele) akitoa hotuba ya
ufunguzi wa kikao cha kamati ya Taifa ya kusukuma mashauri ya Jinai
kilichofanyika mapema Aprili 03,2020 katika kituo cha mafunzo na habari kilichopo Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam.
Msajili wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt (aliyesimama mbele) ambaye ni
Mwenyekiti wa kamati ya Taifa ya kusukuma mashauri ya Jinai akifafanua jambo
mbele ya wajumbe wa kamati hiyo wakati wa kikao hicho.
Mkurugenzi wa
Mashtaka nchini, Bw. Biswalo Mganga ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya haki
jinai akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari wakati wa kikao cha kamati
ya Taifa ya kusukuma mashauri ya Jinai kilichofanyika katika
kituo cha mafunzo na habari kilichopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam.
Mkurugenzi
Msaidizi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, Bw. Charles Kenyela ambaye ni
Mjumbe wa kamati ya Taifa ya kusukuma mashauri ya Jinai akifafanua jambo mbele
ya waandishi wa habari wakati wa kikao hicho.
(Picha na Innocent Kansha- Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni