Jumamosi, 4 Aprili 2020

WADAU WASHAURIWA KUSHIRIKIANA NA MAHAKAMA KUTOA HAKI KWA NJIA YA MTANDAO


Na Lydia Churi na Rashid Omar-Mahakama
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe Dkt. Eliezer Feleshi amewashauri wadau wa Mahakama wakiwemo jeshi la Polisi na Magereza kushirikiana na Mahakama katika kutoa haki kwa njia ya Mtandao hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inapambana na kuenea kwa virusi vya Corona.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kikazi katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji alipoenda kukagua shughuli za Mahakama, Jaji Kiongozi alisema Mahakama imeshaingia kwenye matumizi ya Tehama hivyo analishauri jeshi la Polisi na Magereza kujiandaa kufanya kazi kwa mtandao hasa katika kipindi hichi cha maambukizi ya virusi vya Corona.

“Mahakama ya Tanzania itahakikisha milango ya utoaji haki iko wazi ili wananchi wapate haki kwa wakati”, alisema Mhe. Jaji Feleshi.

Jaji Kiongozi alisema Mahakama ya Tanzania iko tayari kufika magerezani na kusikiliza mashauri endepo Jeshi la Magereza litakuwa tayari kushirikiana na Mahakama.” Badilisheni kumbi zenu tutakuja na kusikiliza mashauri huko, alisisitiza.

Akizungumza na watumisi wa Mahakama katika maeneo aliyopita, Jaji Kiongozi aliwataka watumishi hao kufanya kazi kwa uaminifu na kwa kuzingatia maadili ili kulinda heshima ya Mahakama ya Tanzania.

Akisoma taarifa ya Mahakama ya Wilaya ya Mkuranga, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mkuranga Mhe. Herrieth Mwailolo alisema kwa upande wa usikilizwaji wa mashauri, kati ya Januari na Machi, 2020, jumla ya mashauri 127 yaliamuliwa. Katika kipindi hicho, Mahakama hiyo ilisajili mashauri128 na mashauri yaliyobaki kipindi cha nyuma yalikuwa 196.

Kwa upande wa Mahakama za Mwanzo, Mhe. Mwailolo alisema jumla ya mashauri 133 yalisajiliwa kati ya Januari na Machi ambapo 110 yalisikilizwa na kumalizika wakati yaliyovuka mwaka 2019 yalikuwa ni 74. 

Jaji Kiongozi anaendelea na Ziara yake maalum ya kukagua shughuli za Mahakama katika mkoa wa Morogoro ambapo ataembelea Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Mahakama ya wilaya ya Mvomero, na Mahakama za Mwanzo za Morogoro, Mvomero, na Kingolwira.
 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe Dkt. Eliezer Feleshi akikagua kazi za Mahakama katika Mahakama ya Wilaya ya Mkuranga. Kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dar es salaam Mhe. Lameck Mlacha.

 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe Dkt. Eliezer Feleshi akisisitiza jambo wakati wa ukaguzi wa shughuli za Mahakama.
 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe Dkt. Eliezer Feleshi akisalimiana na Watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Kibiti mara baada ya kuwasili. Kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dar es salaam Mhe. Lameck Mlacha.
 Viongozi pamoja na Watumishi wa Mahakama wakimsikiliza Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe Dkt. Eliezer Feleshi.
 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe Dkt. Eliezer Feleshi akiwa na Viongozi wengine wa Mahakama ya Tanzania.






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni