Na
Lydia Churi-Mahakama Morogoro
Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amemaliza ziara yake ya siku
tano kwa Kanda ya Dar es salaam na kuwataka watumishi wa Mahakama kufanya kazi
kwa bidii, kuzingatia maadili na kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona.
Akizungumza na watumishi
wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro pamoja na Mahakama za wilaya za Morogoro
na Mvomero, Jaji Kiongozi amewakumbusha watumishi hao kutekeleza wajibu wao
huku wakichukua tahadhari kwa kufuata maelekezo yote yanayotolewa na wataalamu
wa afya katika kukabiliana na kuenea kwa maambukizi ya virusi vya Corona.
Alisema Mahakama
itaendelea na huduma zake za utoaji haki licha ya kuwepo kwa ugonjwa huo isipokuwa
imejipanga pia kutoa huduma hizo kwa njia ya Tehama. Aliongeza kuwa katika
kukabiliana na Corona, watumishi hawana budi kuzingatia maelekezo yanayotolewa
ikiwa ni pamoja na kunawa mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka mara kwa
mara.
Ziara ya Jaji Kiongozi
imethibitisha kutekelezwa kwa maelekezo ya wataalamu wa Afya ambapo hatua mbalimbali
zimechukuliwa katika kupambana na Corona ikiwa ni pamoja na kuwekwa kwa vifaa
vya usafi kama maji tiririka, sabuni tishu pamoja na vitakasa mikono katika
Mahakama zote.
Akizungumzia hatua
zilizochukuliwa, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro
Mhe. Abeesiza Kalegeya alisema hatua nyingine zilizochukuliwa ni kupunguzwa kwa
misongamano na mikusanyiko ya watu Mahakamani baada ya kuwekwa utaratibu wa kupunguza
idadi ya watu wanaoingia Mahakamani. Hivi sasa wanaoruhusiwa kuingia ni
wadaawa/washtakiwa wa kesi, mashahidi, Mawakili, Polisi pamoja na wadau wengine
wa Mahakama wanaohitaji huduma muhimu.
Kuhusu ufunguaji wa mashauri, Mhe. Kalegeya alisema mashauri
yanayofunguliwa ni yale ambayo upelelezi umekamilika. Kwa upande wa
usikilizwaji wa mashauri ambayo Mahakama ya Hakimu Mkazi na wilaya hazina
mamlaka nayo na upelelezi haujakamilika, yanaahirishwa kwa mwezi moja. Pia mahabusu
hawaletwi mahakamani isipokuwa wale ambao mashauri yao yapo hatua ya
usikilizwaji. Kwa mashauri ambayo washtakiwa wapo nje kwa dhamana, kipaumbele
kimewekwa kwa yale yaliyokaa mahakamani kwa muda wa zaidi ya miezi 12.
Kwa mujibu wa Hakimu Mkazi
Mfawidhi huyo, Mahakama hivi sasa zimeweka utaratibu wa kuweka masharti nafuu
ya dhamana kwa washtakiwa ili kuwezesha kupunguza msongamano wa mahabusu gerezani
ili kuzuia kuenea kwa virusi vya Corona.
Katika ziara yake, Jaji
Kiongozi pia alikagua miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama inayoendelea
katika kanda ya Dar es salaam. Miradi iliyokaguliwa ni pamoja na ujenzi wa Vituo
Jumuishi vya Utoaji Haki vinavyojengwa Kinondoni, Temeke, na Morogoro.
Mahakama ya Tanzania
imeanza ujenzi wa vituo Jumuishi vya Utoaji haki sita katika miji ya Arusha,
Mwanza, Dar es salaam, Dodoma na Morogoro. Vituo hivyo vinavyotarajiwa
kukamilika ndani ya miezi kumi vitajumuisha Mahakama Kuu, Mahakama za Hakimu
Mkazi, Mahakama za wilaya na Mahakama za Mwanzo na Ofisi za Wadau ndani ya
jengo moja. Lengo ni kurahisisha huduma za utoaji haki na kusogeza huduma za
Mahakama karibu zaidi na wananchi.
Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akisalimiana na watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro mara baada ya kuwasili kukagua shughuli za Mahakama. Kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo Mhe. Abeesiza Kalegeya.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akizungumza na watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Morogoro alipofika kukagua shughuli za Mahakama.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (wa tatu kushoto) akioneshwa ramani ya jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji haki linalojengwa mkoani Morogoro. Wa pili kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dar es salaam Mhe. Lameck Mlacha.
Jaji
Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akielezea jambo alipotembelea mradi wa ujenzi wa jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji haki
linalojengwa mkoani Morogoro. Anayefuatia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania kanda ya Dar es salaam Mhe. Lameck Mlacha.
Jaji
Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (wa nne kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama alipotembelea Mahakama ya wilaya ya Mvomero kukagua shughuli za Mahakama. Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama alipotembelea Mahakama ya Mwanzo Mvomero kukagua shughuli za Mahakama.
Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji haki lililoanza kujengwa mkoani Morogoro.
(Picha na Victor Kitauka- Mahakama, Morogoro
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni