Na
Lydia Churi-Mahakama, Kilwa Masoko
Hakimu Mkazi wa Mahakama
ya wilaya ya Kilwa Mhe. Frank Michael Lukosi amesema kujengwa kwa jengo jipya
la Mahakama ya wilaya ya Kilwa kumerahisisha utendaji kazi wa Mahakama hiyo
ambapo hivi sasa mashauri yanamalizika kwa wakati.
Akizungumza na Maafisa
Habari wa Mahakama leo wilayani humo, Mhe. Lukosi amesema kuna mabadiliko
makubwa katika utoaji wa huduma za kimahakama baada ya kuanza kutumika kwa jengo
jipya la Mahakama ya wilaya ambapo awali Mahakama ilikuwa ikitumia jengo
lililoazimwa kwa ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya lililokuwa na nafasi
finyu kwa ajili ya kutolea huduma.
“Tulikuwa tukipeana zamu
kutoa huduma kutokana na kuwa na vyumba vichache, tulikuwa tukipata shida ya mtandao
(internet) na wakati huo huo mashauri yalikuwa yakichelewa kuanza na hivyo kuchelewa
kukamilizika”, alisema Hakimu huyo.
Alisema jengo jipya
linakidhi idadi ya vyumba vya Mahakimu, watumishi wengine pamoja na vyumba kwa
ajili ya Mawakili na waendesha mashtaka. Aliongeza kuwa kutokana na jengo hilo kuunganishwa
kwenye mkongo wa taifa wa Mawasiliano hivi sasa wanapata mtandao vizuri na kazi
ya kuingiza mashauri kwenye mfumo wa kusajili na kuratibu mashauri wa Mahakama
(JSDS 2) inafanyika kwa ufasaha.
Akizungumzia mashauri
yanayosajiliwa na Mahakama ya wilaya ya Kilwa, Mhe. Lukosi amesema mwaka jana
kulikuwa na mashauri mengi yaliyosajiliwa lakini mwaka huu mashauri ni machache
(52) kutokana na kutokea kwa tatizo la mafuriko pamoja na uwepo wa ugonjwa wa
Covid 19 nchini.
Kwa mujibu wa Hakimu
huyo, wilaya ya Kilwa inaongoza kwa kuwa na mashauri mengi ya jinai yanayohusiana
na ubakaji, mimba za utotoni na mashauri ya Ndoa.
Wakati huo huo, Katibu
Tawala (DAS) wa wilaya ya Kilwa Bw. Haji Mbaruku Balozi amesema anaishukuru Serikali
ya awamu ya tano kwa kujenga jengo la Mahakama linaloendana na hadhi ya Mhimili
wa Mahakama ambapo hivi sasa wananchi wanapata haki zao kwa wakati.
Alisema licha ya kujengwa
kwa jengo hilo wilayani humo, bado Mahakama inakabiliwa na changamoto ya
ukosefu wa baadhi ya majengo ya Mahakama za Mwanzo wilayani humo.
Bw. Balozi pia
aliishukuru Serikali kwa kuyaingiza mabaraza ya Ardhi ndani ya mfumo wa Mahakama ambapo alisema wananchi
waliokuwa wakikosa haki zao wakati mabaraza hayo yalipokuwa nje ya mfumo wa
Mahakama sasa watapata haki zao.
Jengo la Mahakama ya wilaya
ya Kilwa lilizinduliwa rasmi mwezi Januari mwaka huu na Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma. Mahakama ya Tanzania inaendelea na ujenzi wa
majengo ya Mahakama katika maeneo mbalimbali nchini.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya wilaya ya Kilwa Mhe.
Frank Michael Lukosi akizungumzia Maboresho yaliyofanywa na Mahakama ya Tanzania.
Katibu Tawala (DAS) wa wilaya
ya Kilwa Bw. Haji Mbaruku Balozi akizungumzia Maboresho yaliyofanywa na Mahakama ya Tanzania. Ameishukuru Serikali ya awamu ya tano
kwa kujenga jengo la Mahakama linaloendana na hadhi ya Mhimili wa Mahakama.
Jengo la Mahakama ya wilaya ya Kilwa. Pichani ni wananchi wakisubiri kupatiwa huduma.
Jengo la Mahakama ya wilaya ya Kilwa. Pichani ni wananchi wakisubiri kupatiwa huduma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni