Na Magreth Kinabo – Mahakama
Mwenyekiti wa Kamati ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na
Takwimu ya Jaji Mkuu, Mhe. Shaaban Lila amewataka wajumbe wa kamati hiyo kutoa uzoefu wao
kuhusu matumizi ya teknolojia na kuzitafutia
ufumbuzi changamoto mbalimbali
wanazokabiliana nazo katika eneo
hilo.
Akizungumza jana wakati akifungua kikao cha kamati hiyo cha siku mbili kilichofanyika kwenye ukumbi wa mkutano wa
Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi
uliopo Jijini Dar es Salaam, Jaji Lila, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, alisema
teknolojia hiyo imeanza kutumika mahakamani na wana majukumu tisa ya kuyafanyia kazi.
‘‘Tutumie kikao hiki kubadilishana uzoefu na kuzitafutia ufumbuzi
changamoto tunazokabiliana nazo katika matumizi ya TEHAMA ukitaka kutatua
tatizo ni lazima uliweke bayana na kulitafutia ufumbuzi, ’’ alisema Mwenyekiti
huyo.
Lila aliongeza kwamba kamati hiyo imepewa majukumu mbalimbali ya
kuyatekeleza ili kuhakikisha eneo la TEHAMA linatekelezwa ipasavyo,
hivyo aliwataka wajumbe hao kutoa ushauri wa kuendelea kuboresha eneo hilo.
Alifafanua kuwa mifumo ya TEHAMA
iendelee kuboreshwa iwe ya manufaa kwa wananchi na
Mahakama pia kuwataka wajumbe wa kikao hicho kuyataja maeneo
yanayotakiwa kuboreshwa.
Kwa upande wake Katibu wa kamati
hiyo, ambaye pia Mkurugenzi wa TEHAMA wa
Mahakama ya Tanzania, Bw. Enock Kalege akitoa taarifa ya maendeleo ya
teknolojia hiyo, alisema imeleta matokeo
chanya katika shughuli mbalimbali
za Mahakama licha ya kuwepo kwa baadhi ya changamoto kama
vile rasilimali fedha na watu kwa ajili
ya kuendelea kulitekeleza jukumu husika.
Kalege alisema kwamba teknolojia
hiyo pia inasaidia kuwa na takwimu sahihi kama vile vifaa vya TEHAMA ili kuweza kuboresha na kupanga
mipango ya sasa na baadae kwa
faida ya Mahakama.
‘‘Tumefanikiwa kukamilisha jukumu hili la TEHAMA kwa asilimia 71 kupitia miradi
ya uwekezaji kwenye eneo hili, na tunaendelea
kutekeleza asilimia 29 iliyobakia,’’ alisisitiza.
Akizungumzia kuhusu eneo hilo, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert
Chuma alisema kwa upande wa kufungua
mashauri kwa njia ya Mahakama Mtandao limeendelea kutekelezwa kama
ilivyoagizwa na Jaji Mkuu wa Tanzania.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru alisema
ili kuhakikisha teknolojia hiyo inaendelea
kurahisisha huduma ya utoaji haki na kupunguza gharama za uendeshaji wa shughuli tofauti za Mahakama ni vema watumishi wakaendelea kujengewa uwezo
na kubadili mitazamo yao.
Mwenyekiti wa Kamati ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na
Takwimu ya Jaji Mkuu, Mhe. Shaaban Lila
ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, (aliyenyoosha mkono) akizungumza jambo jana wakati akifungua kikao cha kamati hiyo cha siku mbili kwenye ukumbi wa mkutano wa Mahakama Kuu
ya Tanzania Divisheni ya Ardhi uliopo
Jijini Dar es Salaam.
|
|
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara, Mhe.
Patricia Fikirini( wa kwanza kushoto) akichangia jambo.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni