Na
Lydia Churi-Mahakama, Kigoma
Mahakama Kuu ya Tanzania
Kanda ya Kigoma imefanikiwa kwa asilimia 100 kumaliza mashauri yote ya
mlundikano na kuvuka kiwango kilichowekwa na Mahakama ya Tanzania.
Mahakama ya Tanzania
ilijiwekea mkakati wa kumaliza mashauri ya mlundikano kwa kuweka muda wa shauri
kumalizika mahakamani ambapo kwenye Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu shauri
linatakiwa kumalizika katika kipindi cha miezi 24, Mahakama za Hakimu Mkazi na
Mahakama za wilaya miezi 12 na Mahakama za Mwanzo ni miezi sita.
Akizungumza na Maafisa
Habari wa Mahakama ya Tanzania, Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu ya Tanzania kanda
ya Kigoma Mhe. Ilvin Mugeta alisema kuanzishwa kwa Mahakama Kuu mkoani Kigoma
na kujengwa kwa jengo jipya la Mahakama hiyo kumerahisisha shughuli za utoaji
haki kwenye kanda hiyo ambapo hivi sasa hakuna mlundikano wa mashauri kwa
viwango vilivyowekwa na Mahakama ya Tanzania. Aliongeza kuwa kwa upande wa
Mahakama Kuu mashauri yalisikilizwa na kumalizika ndani ya miezi 24.
Jaji Mfawidhi huyo alisema
licha ya Mahakama kuweka kiwango cha kitaifa, Kanda ya Kigoma pia ilijiwekea
kiwango cha muda wa kumaliza mashauri ambapo kwa Mahakama Kuu ni miezi 6,
Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama za wilaya miezi minne wakati Mahakama za
Mwanzo ni miezi mitatu.
“Juni 30 mwaka huu tulifanya tathmini ya viwango
tulivyojiwekea na kugundua kuwa tumefanikiwa kwa asilimia 77 kwani kati ya mashauri
115 yaliyokuwepo Mahakama Kuu, ni mashauri 19 tu ndiyo yalivuka miezi 6 nayo
yalikuwa ni yale yaliyokatiwa rufaa na majalada yake yalikuwa yamecheleweshwa
kutoka Mahakama za chini”, alisema Jaji Mugeta.
Kwa upande wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi na Mahakama za wilaya, Jaji Mfawidhi alisema baada ya tathmini ya
Juni 30, hakukuwa na mashauri ya mlundikano kwa mashauri ambayo Mahakama hizo
zina mamlaka nayo. “Tumefanikiwa kwa asilimia 71 kufikia lengo la kikanda la
miezi 4 tulilojiwekea na lengo la kitaifa la miezi 12 pia tumefanikiwa kwa
asilimia 100”, alisema.
Kwa mujibu wa Jaji
Mugeta, Kanda ya Kigoma imefanikiwa kwa asilimia 100 kuvuka lengo la kitaifa la
kumaliza mashauri ndani ya miezi sita na lengo la Kanda la miezi mitatu
iliyojiwekea kwa Mahakama za Mwanzo kwa kuwa mashauri yote 240 yaliyokuwepo
kwenye Mahakama hizo yalisikilizwa na kumalizika katika kipindi cha miezi mitatu.
Kuhusu utoaji wa hukumu
ndani ya siku 90, kanda ya Kigoma imefanikiwa kwani mpaka Juni 30 hakukuwa na
shauri ambalo halikusomwa hukumu ndani ya siku 90 na pia kwa upande wa nakala
za hukumu kanda hiyo ilifanikiwa kutoa nakala hizo ndani ya siku 21.
Aidha, Jaji Mugeta
alisema kuhusu Mahabusu na Magereza, wamefanikiwa kusimamia mkakati wa taifa wa
kuondoa msongamano wa mahabusu na wafungwa magerezani kwa asilimia 100.
Tathmini iliyofanyika Juni 30 mwaka huu ilionesha kuwa hakukuwa na gereza lenye
msongamano mkoani humo, magereza yote yalikuwa na idadi ya wafungwa na mahabusu
kwa kadri ya uwezo wake.
Kuhusu matumizi ya Tehama
kwenye kanda hiyo, Jaji Mfawidhi alisema vifaa vya Tehama vimefungwa kwenye
Mahakama zote kuanzia Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama zote
za wilaya. Aliongeza kuwa Magereza ya Kasulu, Kibondo na Bangwe tayari
yamefungiwa vifaa hivyo isipokuwa magereza mawili ya Kwitanga na Ilagala ambayo
yatafungiwa ifikapo Septemba mwaka huu.
Alisema mashauri 20
yanayohusu mahabusu yameshasikilizwa kwa njia ya Mahakama mtandao (Video
conference) na mpango uliopo ni kuiwezesha ofisi ya Taifa ya Mashtaka kupata
vifaa vya Tehama ili kurahisisha utendaji wa kazi.
Alisema Kanda ya kigoma
inafanya vizuri kwenye matumizi ya mfumo wa kusajili mashauri kwa njia ya
mtandao (JSDS ll) na imefikia hatua ya kuwasajili Mawakili wa kujitegemea
kwenye mfumo huo kwa mujibu wa sheria ya kusajili mashauri kwa mtandao.
Mahakama ya Tanzania
inaendelea na Maboresho ya huduma zake kwa kusogeza huduma zake karibu zaidi na
wananchi kwa kujenga majengo mapya, kuboresha sheria na kanuni mbalimbali na
kutumia Tehama kurahisisha shughuli za utoaji haki nchini.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu ya Tanzania kanda
ya Kigoma Mhe. Ilvin Mugeta akizungumzia Mafanikio ya kanda hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni