Na Innocent Kansha – Mahakama Kondoa
Mahakama ya wilaya ya
Kondoa imesikiliza na kumaliza mashauri ya jinai na madai 184 kati ya mashauri
262 yaliyokuwepo katika Mahakama za wilaya za Kondoa na Chemba.
Akizungumza na Maafisa
Habari wa Mahakama ya Tanzania, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya
Wilaya ya Kondoa Mhe. Francis Robert Mhina alisema mashauri hayo yamesikilizwa
na kumalizika kati ya mwezi Januari na Julai, mwaka huu.
“Mashauri yaliyobaki
mwezi Desemba 2019 yalikuwa ni 152, yaliyosajiliwa kati ya Januari na Julai
mwaka huu ni mashauri 110, tumesikiliza na kumaliza jumla ya mashauri 184 na
kubakiwa na mashauri 78”, alifafanua Mhe. Mhina.
Kwa mujibu wa Hakimu
Mfawidhi huyo, asilimia kubwa ya mashauri yanayofunguliwa kwenye Mahakama hizo
ni yale yanayohusu ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji, pamoja na mauaji,
kujeruhi na mashauri ya kukutwa na nyara za wanyama pori.
Alisema mashauri yanayohusu
nyara za taifa hasa wanyama pori yanatokana na uwepo wa mapori tengefu ya
hifadhi za Swaga swaga na Mkungunero.
“Wananchi wengi
wanaoishi kando kando ya hifadhi hizi wamekuwa wakiendesha shughuli zao
mbalimbali za kiuchumi bila kuzingatia mipaka na kujikuta wanakinzana na sheria
za hifadhi kama kulima ndani ya hifadhi, kuvua samaki, kuchoma mkaa, kukutwa na
nyara za Taifa na kuwinda wanyama pasipo kuwa na vibali halali”, alisema Mhe.
Mhina.
Mhe. Mhina alisema asilimia
kubwa ya mashauri ya mauaji yanatokea Wilaya ya Chemba. Mahakama ya Wilaya ya Kondoa
pia inahudumia Wilaya Chemba kwa sasa.
Kuhusu matumizi ya
Tehama katika Mahakama ya wilaya ya Kondoa, Mhe. Mhina amesema yamesaidia kwa
kikubwa kurahisisha suala la upatikanaji wa haki kwa wakati. Aliongeza kuwa mfumo
wa kusajili mashauri (JSDS II) unatumiwa vizuri na watumishi katika kutunza
kumbukumbu za kila siku za mashauri baada ya kufungiwa mkongo wa Taifa wa
mawasiliano.
Naye Katibu Tawala wa
Wilaya ya Kondoa Bw. Andrea Ng’hwani alisema Serikali Wilayani humo imeyapokea
maboresho ya miundombinu ya Mahakama kwa furaha kwani yametatua changamoto na
kero za wananchi wa Kondoa kwa kiasi kikubwa.
“Nawakumbusha wananchi
kuwa nchi hii inaongozwa kwa misingi ya kisheria na hakuna mazingira yoyote
yanayoruhusu mtu kujichukulia sheria mikononi ndiyo maana kuna Jeshi la Polisi
na Mahakama ili kutatua kero zao” alisisitiza Katibu Tawala.
“Kero za wananchi
zimepungua sana na sasa hatupokei malalamiko yanayohusu Mahakama kiutendanji na
mambo mengine yanayohusu uelewa wa taratibu za kimahakama tumekuwa mstari wa
mbele kuyatolea ufafanuzi wa kuwaelekeza sehemu sahihi ya kutatua na kupata
ufafanuzi”, alisema Katibu Tawala.
Bw. Ng’hwani alisema
wananchi wanapaswa kupeleka migogoro yao mahakamani ili iweze kutatuliwa
kisheria na pale wanapoona hawajaridhika na maamuzi, wakate rufaa Mahakama ya juu zaidi kupata haki ili
Amani na utulivu vizidi kuimarika.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kondoa Bw. Andrea Ng’hwani akitoa rai kwa wananchi wa Kondoa kuitumia Mahakama ya wilaya ya Kondoa kutatua migogoro yao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni