Alhamisi, 30 Julai 2020

ZINGATIENI VIAPO VYENU ILI KUTENDA HAKI WAKATI WOTE: MSAJILI MKUU.

Na Innocent Kansha - Mahakama

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma amewataka Mahakimu Wakazi wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama ya wilaya kutekeleza kazi ya kutoa haki kwa mujibu wa kiapo cha uhakimu kinachowataka kutenda haki bila huba, hofu, upendeleo wala chuki.

Msajili Mkuu aliyasema hayo mapema wiki hii alipokuwa akitoa neno la utangulizi wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Mahakimu Wakazi waliokuwa wasaidizi wa sheria wa Waheshimiwa Majaji kilichofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu Masjala Kuu Jijini Dar es salaam.

“Mpende kujenga mazoea ya kujisomea ili muweze kumudu majukumu yenu kwa ufanisi na kuepuka utegemezi, huwezi kuwa taswira ya Mahakama kama huwajibiki ipasavyo katika utendaji wako wa kazi”, alisema Mhe. Chuma.

Mhe. Chuma aliwakumbusha na kuwahimiza kuelewa na kutekeleza kwa vitendo maboresho yanayoendelea mahakamani kama matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ikiwa ni moja ya vipaumbele kwa sasa. Aliwataka Mahakimu hao kuhakikisha wanashiriki ipasavyo kuhuisha taarifa za mashauri kwenye mfumo wa kusajili mashauri (JSDS II) na kuweka maamuzi kwenye mfumo wa kutunza maamuzi (TANZLII). “Haya ni maeneo mtakayoendelea kufuatiliwa kwa karibu katika utekelezaji wake”, alisisitiza.

Msajili Mkuu aliwashauri kutumia muda mwingi kuonyesha umahiri katika kuwajibika kwa manufaa ya umma na jamii kwa ujumla kwa kuwa  kundi hilo linategemewa kufanya mageuzi na pengine kushika nyadhifa mbalimbali za kiuongozi katika muhimili huu.

“Ni wakati wenu kujipambanua mtakapokuwa vituoni kwenu kutoa maamuzi na kuandika hukumu zinazoeleweka kwani hukumu pekee ina uwezo wa kuzungumza”, alisema.

Msajili Mkuu aliwaasa kufanya kazi kwa kuzingatia viapo vyao, kujiepusha na rushwa na aina yoyote ya ukiukaji wa maadili kwani rushwa ni adui wa haki na imekemewa pia katika vitabu vitakatifu kama Biblia na Quran, “kazi ya uhakimu ina miiko yake na si kazi ambayo anaweza kufanya mtu yeyote”, alisisitiza.

Juni 2019, Wasaidizi wa Sheria 53 wa Waheshimiwa Majaji waliapishwa kuwa Mahakimu wakazi na kuwekwa kwenye programu maalumu ya mwaka moja ya kusikiliza mashauri katika Mahakama za Mwanzo, wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi na baadaye kupangiwa vituo vya kazi baada ya kumaliza program hiyo.

 Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Mahakimu wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za wilaya waliopangiwa vituo vya kazi hivi karibuni.  

 Baadhi ya Mahakimu wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za wilaya waliopangiwa vituo vya kazi hivi karibuni wakiwa kwenye kikao kazi chao. 
 Baadhi ya Mahakimu wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za wilaya waliopangiwa vituo vya kazi hivi karibuni wakiwa kwenye kikao kazi chao. 




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni