Na Lydia Churi-Mahakama, Dodoma
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema
Mahakama kupitia Mpango Mkakati wake wa pili wa miaka mitano (2020-2025)
imewaahidi wananchi mambo matano ikiwemo maboresha ya miundombinu yake ili
kurahisisha upatikanaji wa haki.
Akifungua awamu ya pili
ya mafunzo ya namna bora ya uendeshaji
wa mashauri ya uchaguzi kwa Majaji wa Mahakama kuu leo jijini Dodoma, Jaji Mkuu
ameyataja mambo mengine kuwa ni kukamilisha usimamizi wa mashauri kwa
njia za Tehama, kuboresha uwezo wa watumishi kutimiza wajibu wao, kuimarisha
shughuli za ukaguzi, usimamizi na malalamiko na kuimarisha ushirikiano na
wadau.
“Tutatumia Mpango mkakati
wa miaka mitano wa Mahakama kama nyenzo ya kubainisha ahadi kwa maana ya
tutafanya nini kwa miaka mitano ijayo”, alisema Jaji Mkuu.
Alisema wakati wa
uchaguzi ni wakati wa kila mhimili wa dola kujitathmini na pia kuahidi itafanya
nini katika miaka mitano ijayo hivyo amewataka watumishi wa Mahakama kuusoma,
kuuelewa na kuutekeleza Mpango Mkakati wa pili ambao utawaongoza kuanzia mwaka
2020 hadi 2025.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, tathmini
ya Mpango Mkakati wa mwaka 2016-2021, iliyofanywa katika maeneo mbalimbali imeonesha
kupungua kwa mlundikano wa mashauri kutoka asilimia 12 mwaka 2015 hadi kufikia
asilimia tano mwaka 2019.
Alisema ufanisi pia ulipimwa
kupitia mafanikio katika kuongezeka kwa matumizi ya TEHAMA na matumizi ya
teknolojia katika uendeshaji wa mashauri na ufanisi katika watumishi wa ngazi
mbalimbali kupata mafunzo.
Jaji Mkuu ametoa wito kwa
Majaji na watumishi wote wa Mahakama kuhakikisha wanausoma mpango huo ili
wafahamu malengo na muelekeo wa mhimili kwa kuwa mafanikio ya mpango mkakati
yanategemea namna viongozi na watumishi wote wa Mahakama watakavyokubali kuumiliki
mpango huo.
Akizungumzia mashauri
yatakayotokana na uchaguzi mkuu ujao, Jaji Mkuu amewataka Majaji kutumia nafasi
muhimu ya kusikiliza mashauri hayo kuibua maeneo ya uchaguzi ambayo yanahitaji
maboresho.
Alisema Majaji ni viongozi, hivyo maamuzi yao hayana budi kushawishi kuboresha sheria au kubadilisha sera zinazohusu masuala ya sheria na haki.
Baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu wakiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati-waliokaa) mara baada ya kufungua mafunzo hayo.
Majaji wa Mahakama Kuu Zanzibar wakiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati-waliokaa) mara baada ya kufungua mafunzo hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni