Na Lydia Churi-Mahakama, Dodoma
Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amewataka Majaji wa Mahakama
Kuu kuwa tayari kusikiliza mashauri yatakayofunguliwa kutokana na uchaguzi Mkuu
unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Akifunga awamu ya kwanza
ya mafunzo ya namna bora ya uendeshaji
wa mashauri ya uchaguzi kwa baadhi ya waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Jaji Kiongozi amesema Mahakama itampangia Jaji yeyote kusikiliza
mashauri ya uchaguzi hivyo kila Jaji anapaswa kuwa na hali ya utayari na
kujiandaa kutekeleza wajibu huo muhimu.
“Mafunzo
mliyopata yana lengo la kuweka mazingira sahihi ili Jaji yeyote atakapopangiwa
kusikiliza mashauri yatokanayo na uchaguzi Mkuu awe tayari wakati wote”,
alisisitiza Jaji Kiongozi.
Alisema Mahakama imepanga kumaliza mashauri yatakayotokana na uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ndani ya miezi minne (4) kwa kuwa tayari imeshaonesha
mwelekeo wa kuyashughulikia. Aliongeza kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015
mashauri ya aiona hiyo yalisikilizwa na kumalizika ndani ya miezi sita (6)
tangu kufunguliwa kwake.
Jaji
Feleshi amewataka Majaji Wafawidhi kujiandaa na pia kuhakikisha wanawaandaa Naibu
Wasajili pamoja na Mahakimu ili wawe tayari kusikiliza mashauri hayo. Kiongozi
huyo pia ameagiza mashauri mengine yaliyopo na yanayoendelea kufunguliwa mahakamani
yaendelee kusikilizwa na kumalizika kwa wakati licha ya kuwepo kwa mashauri
yatakayotokana na uchaguzi Mkuu.
Aidha,
ametoa wito kwa Majaji wote kuendeleza ushirikiano uliopo baina yao, kujaliana
na kupendana wakati wote kwa kuwa mahakama ni familia.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Mahakama ya
Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) yamesaidia
kuwajengea uwezo Maafisa wa Mahakama na kuwaandaa kutoa haki kwenye mashauri ya
Uchaguzi Mkuu ujao wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Mafunzo yaliyomalizika leo yaliwahusisha baadhi
ya Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Awamu inayofuata pia
itawahusisha Majaji wengine wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Jumatatu Agosti 24
yataanza mafunzo hayo kwa Wasajili, Naibu Wasajili na Mahakimu
Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi.
Mafunzo haya pia
yatatolewa kwa waheshimiwa Majaji
wa Mahakama ya Rufani kuanzia Septemba 2-4, 2020 mkoani Morogoro. Mahakimu
Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya nao watapatiwa mafunzo hayo baadaye katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama
Lushoto-Tanga.
Wawezeshaji wa mafunzo hayo ni baadhi ya
Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu waliopo na wastaafu, Naibu
wasajili, Mahakimu pamoja na wawezeshaji kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi,
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa
na Tume ya Kurekebisha Sheria ambao ni wadau muhumu katika masuala ya Uchaguzi.
Baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakimsikiliza Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi (hayupo pichani) alipokuwa akifunga awamu ya kwanza ya mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi leo, jijini Dodoma.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tanga Mhe. Edson Mkasimongwa akipokea cheti baada ya kuhudhuria mafunzo yaliyomalizika leo kwa awamu ya kwanza.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma Mhe. Ilvin Mugeta akipokea cheti baada ya kuhudhuria mafunzo yaliyomalizika leo kwa awamu ya kwanza.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma Mhe. Mustapher Siyani akipokea cheti baada ya kuhudhuria mafunzo yaliyomalizika leo kwa awamu ya kwanza.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akipokea cheti kutoka kwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi Mhe. Imani Aboud mara baada ya kumalizika kwa mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi leo jijini Dodoma.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akionesha cheti alichopokea baada ya kuhudhuria mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi yaliyomalizika leo, jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni