Na Lydia Churi-Mahakama, Shinyanga
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka watumishi wa Mahakama kubadili tabia na
mitazamo ili iendane na ubora wa majengo mapya na yenye vifaa vya kisasa yanayojengwa
na Mahakama ya Tanzania katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizindua jengo la
Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga leo, Jaji Mkuu amesema Mahakama
haitokani na majengo mazuri peke yake, bali huduma bora kwa wananchi ambapo pia
amewataka watumishi wa Mahakama kuacha tabia zisizoendana na maadili mema wanapotekeleza
wajibu wao..
“Maboresho makubwa
tuliyofanya kupitia Mpango Mkakati, Programu ya Maboresho na uwekezaji mkubwa
katika TEHAMA hayataboresha huduma za utoaji haki kama watumishi na viongozi
katika ngazi zote za Mahakama hawatakuwa na mitazamo chanya ya kuwaheshimu na
kuwathamini wanaofika mahakamani kutafuta haki” alisema Jaji Mkuu.
Alisema, nguvu na uwezo
wa Mahakama kwa kiasi kikubwa unategemea imani ya wananchi kwa Mhimili huo na
kuwa dhana ya sasa inayoongoza ujenzi wa majengo ya Mahakama ni kujenga majengo
yanayotoa huduma jumuishi (Integrated Justice Centres), yaani kutoa huduma za
zaidi ya ngazi moja ya Mahakama na pia wadau wanaotoa huduma mbali mbali kuwa
katika jengo moja.
Jaji Mkuu alisema maboresho
yatakuwa endelevu endapo watumishi wote watayaelewa na kutambua Mahakama inaelekea
wapi. “Nawaomba watumishi wa Mahakama tutekeleze dhana ya kumiliki maboresho na
tutafanikiwa endapo kila mtumishi atafuatilia utekelezaji wake na kuyaelewa na
kuwa tayari kuyafafanua kwa wananchi, wadau na hata kwa Mihimili ya Serikali na
Bunge” alisisitiza.
Alisema maboresho ya miundombinu
ya majengo ya Mahakama yanalenga mambo makuu mawili ambayo ni kuhakikisha wananchi
wanapata huduma za utoaji haki katika majengo bora yakiwa na vitendea kazi vya
kutosha na kuwapunguzia wananchi umbali mrefu wanapotafuta huduma za Mahakama.
Jaji Mkuu aliwapongeza wananchi
wa Mkoa wa Shinyanga kwa kupewa kipaumbele katika kupatiwa huduma za Mahakama
Kuu kwani mikoa ya Morogoro, Pwani, Singida, Manyara, Njombe, Geita, Katavi,
Lindi, Simiyu na Songwe bado inasubiri kwa hamu kuwa na majengo yao ya kutoa
huduma katika ngazi ya Mahakama Kuu.
Pamoja na kusogezewa
huduma katika ngazi ya Mahakama Kuu; wananchi wa Mkoa wa Shinyanga, kupitia
jengo lililozinduliwa wamesogezewa pia huduma za Mahakama ya Rufani. Kupitia
Tangazo la Gazeti la Serikali No. 579 la tarehe 24/7/2020, jengo la Mahakama
Kuu Shinyanga, limetangazwa kuwa ni Masjala Ndogo ya Mahakama ya Rufani.
Alifafanua kuwa tangazo
hilo lina maana kuwa, Mahakama ya Rufani itafanya kikao chake cha kwanza Shinyanga
kuanzia tarehe Agosti 10 hadi 28, 2020 ili kusikiliza jumla ya mashauri 29. Kila
mwaka, Mahakama ya Rufani itakuwa na vikao katika jengo kanda ya Shinyanga.
Wakati
huo huo, Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande
Othman ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kubuni na kuendeleza mkakati wa
ujenzi wa majengo ya Mahakama yenye ubora zaidi.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack aliipongeza
Mahakama ya Tanzania kwa kusogeza karibu na wananchi. Alisema kazi ya Mhimili
wa Mahakama pamoja na Serikali ni kutoa huduma bora kwa wananchi ili wawe na
furaha na amani.
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi
amesema Mahakama ya Tanzania imejipanga kama mihimili mingine ilivyojipanga
katika suala la uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba mwaka huu. “Mahakama
itasimama kwenye nafasi yake katika uchaguzi Mkuu”alisisitiza Jaji Kiongozi.
Msajili
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma amewataka
watumishi wa Mahakama pamoja na wadau kuyalinda, kuyaenzi na kuyaishi maboresho
ya Mahakama ikiwemo majengo pamoja na matumizi ya Tehama. Aliwataka watumishi
kutenda haki na kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu na uadilifu.
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru
alipongeza watangulizi wake Mahakama kwa ubunifu na usimamizi mzuri wa miradi
ya ujenzi wa majengo ya Mahakama likiwemo jengo la kanda ya Shinyanga
lililozinduliwa.
Akizungumzia gharama za
ujenzi wa jengo hilo, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Bw. Leonard Magacha
amesema kuwa ujenzi wa jengo hilo umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 3.9
ambazo ni fedha za ndani.
Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Mohamed Chande Othman akiwa ameongozana na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi wakiwasili kwenye viwanja vya Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Shinyanga.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Mohamed Chande Othman na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack wakifungua pazia kuashiria kuzindua jengo la Mahakama Kuu kanda ya Shinyanga.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na viongozi wengine wakipatiwa maelezo ya jengo lililozinduliwa na Naibu Msajili wa kanda ya Shinyanga Mhe. Romuli Mbuya.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na viongozi wenzake wakipatiwa maelezo ya jengo lililozinduliwa na Naibu Msajili wa kanda ya Shinyanga Mhe. Romuli Mbuya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni