Na Innocent Kansha – Mahakama Logindo.
Mahakama ya Wilaya ya
Longido imefanikiwa kusikiliza na kuyatolea uamuzi mashauri ya Jinai na Madai
72 kati ya mashauri 90 yaliyosajiliwa katika kipindi cha Januari hadi Julai 31
mwaka huu.
Akizungumza na Maafisa
Habari wa Mahakama ya Tanzania, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya
Longido Mhe. Aziza Emily Temu alisema mashauri hayo yamesikilizwa na kumalizika
kati ya mwezi Januari na Julai, mwaka huu.
“Mashauri yaliyobaki
mwezi Desemba 2019 yalikuwa ni 128 yaliyosajiliwa kati ya Januari na Julai
mwaka huu ni mashauri 90, tumesikiliza na kumaliza jumla ya mashauri 72 na
kubakiwa na mashauri 146”, alifafanua Mhe. Temu.
Kwa mujibu wa Hakimu Mfawidhi
huyo, asilimia kubwa ya mashauri yanayofunguliwa kwenye Mahakama hiyo ni ya
kukutwa na Dawa za kulevya hasa Bangi na Mirungi, Mauaji na mashauri ya madai
kwa uchache.
Alisema mashauri
yanayohusu kukutwa na dawa za kulevya mirungi na bangi, yanachangiwa na Wilaya
ya Longido kuwa mpakani mwa Tanzania na Kenya hivyo kutumika kama korido ya
kusafirisha mihadarati.
Kuhusu matumizi ya Tehama
yalivyochangia utoaji haki kwa wakati kwenye Mahakama hiyo, Mhe. Temu alisema
mashauri yote yaliyosajiliwa kuanzia mwaka 2012 yameingizwa na kuhuishwa kwenye
mfumo wa utunzaji kumbukumbu za kimahakama (JSDS II) ambapo kazi hii imechagiwa
na kufungiwa mkongo wa Taifa wa mawasiliano.
“Imepelekea urahisishaji
wa upatikanaji wa takwimu, kutunza taarifa za mashauri kwa haraka, kutuma
taarifa za ujumbe mfupi kwa wadaawa ili kuwafahamisha hatua mbalimbali za
mashauri yao na kuonyesha dhahiri shairi tuko katika Mahakama ya kimtandao
zaidi”, alisema Hakimu huyo.
“Mahali pazuri pa
kufanyia kazi panaleta ufanisi mzuri kiutendaji kwa maana ya utoaji haki kwa
wakati na kuonekana haki ikitendeka, nawasihi wadau wetu kurejesha imani kwa
Mahakama yao, tumejiwekea mipango madhubuti ya kuhakikisha tunawahudumia kwa
weledi kwa kufuata kanuni na misingi ya kisheria” alisisitiza Mhe. Temu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya
Longido mkoani Arusha Mh. Frank James Mwaisumbe alisema wananchi wana fursa ya
kuitumia Mahakama yao iliyosongezwa karibu na yenye hadhi, wafahamu kuwa ipo
kwa ajili yao ili kupata haki na si vinginevyo na hasa jinsia ya kike.
“Uwepo wa Mahakama hii ya
kisasa itakuwa suluhisho la utatuzi wa migogoro kwenye jamii hii ya kifugaji
hasa unyanyasaji wa kijinsia kwa akina mama wanaohesabika kama watoto kwenye
koo za Kimaasai, hivyo itasaidia kutatua matatizo yaliyokuwa yakiamriwa kijadi
na kuacha manung’uniko kwa ustawi wa jamii”, alisema Mkuu wa Wliaya.
Mh. Mwaisumbe alisema serikali
itaendelea kutoa elimu ikishirikiana na Mahakama ili wanajamii waelewe umuhimu
wa chombo hiki na jinsi kinavyotenda kazi zake, na sasa itakuwa jibu la mambo
yote yanayokwenda kinyume na taratibu za kisheria.
Jengo
la Kisasa la Mahakama ya Wilaya ya Longido linalotumika kutolea huduma za
utoaji haki kwa Wananchi.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama ya Wilaya ya Longido Mhe.Aziza Emily Temu akielezea jinsi maboresho ya
Miundombinu ya Mahakama yalivyochangia ufanisi kata utoaji wa haki kwa wakati
kwa wananchi wa Wilaya ya Longido.
Mkuu
wa Wilaya ya Longido mkoani Arusha Mhe. Frank James Mwaisumbe akielezea namana hatua
ya Mahakama ya kusongeza huduma za kimahakama karibu na wananchi itakavyokuwa
suluhisho kwa jamii.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni