Emmanuel Oguda-Mahakama, Shinyanga
Vikao vya Mahakama ya Rufani, kwa mara ya kwanza vimeanza kufanyika Shinyanga baada ya kufunguliwa rasmi kwa huduma hizo na Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma jana mjini Shinyanga.
Ufunguzi huo umefanyika kwenye
ofisi za Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga kupitia gwaride maalum
lililoandaliwa na Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga na kukaguliwa na Mhe. Jaji
Mkuu.
Kufuatia ufunguzi huo, wananchi
wa Mkoa wa Shinyanga sasa wataanza kupata huduma za Mahakama ya Rufani. Kupitia
Tangazo la Gazeti la Serikali No. 579 la tarehe 24/7/2020, jengo la Mahakama
Kuu Shinyanga, limetangazwa kuwa ni Masjala Ndogo ya Mahakama ya Rufani. Kila mwaka, Mahakama ya Rufani itakuwa na
vikao katika jengo la kanda ya Shinyanga.
Katika vikao hivyo Jumla
ya mashauri 29 yanatarajiwa kusikilizwa na Majaji wa Mahakama ya Rufani akiwemo
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe Prof. Ibrahim Hamis Juma pamoja na Majaji wengine ambao
ni Mhe. Jacobs Mwambegele, Mhe. Augustine Mwarija na Mhe. Rehema Kerefu.
Aidha, kikao hicho cha
kwanza cha Mahakama ya Rufani kitasikiliza mashauri ya aina mbalimbali yakiwemo;
Maombi ya Madai 5, Rufaa ya Madai moja, na Rufaa za Jinai 23.
Jengo la Mahakama kanda
ya Shinyanga lilizinduliwa rasmi Agosti 7 mwaka huu na Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma baada ya kukamilika kujengwa Mwaka 2015 kwa
gharama za shilingi bilioni 3.9 ambazo ni fedha za ndani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni