Ijumaa, 14 Agosti 2020

MAHAKAMA MANYARA YAMALIZA MASHAURI 283 NDANI YA MIEZI SITA

 Na Innocent Kansha – Mahakama Babati.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara imefanikiwa kusikiliza na kumaliza jumla ya mashauri 283 kati ya mashauri 343 yaliyosajiliwa katika kipindi cha Januari hadi Julai 31 mwaka huu.

Akizungumza na Maafisa Habari wa Mahakama ya Tanzania, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara Mhe. Simon Kobero alisema mashauri hayo yamesikilizwa na kumalizika kati ya mwezi Januari na Julai, mwaka huu.

“Mashauri yaliyobaki mwezi Desemba 2019 yalikuwa ni 309, yaliyosajiliwa kati ya Januari na Julai mwaka huu ni mashauri 343, tumesikiliza na kumaliza jumla ya mashauri 283 na kubakiwa na mashauri 345”, alifafanua Mhe. Kobero.

Kwa mujibu wa Hakimu Mfawidhi huyo, asilimia kubwa ya mashauri yanayofunguliwa kwenye Mahakama hiyo ni ya kukutwa na nyara za serikali, Dawa za kulevya hasa bangi na mirungi, Mauaji na mashauri mengine ya kawaida.

Alisema mashauri yanayohusu kukutwa na nyara za serikali hasa wanyama pori yanatokana na uwepo wa Hifadhi za Taifa katika mkoa huo ikiwa ni pamoja na mbuga za wanyama za Manyara, na Tarangire na mapori mengine ya akiba.

“Shughuli za kiuchumi, uboreshaji wa miundombinu na kuongezeka kwa watu kumechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa vitendo vya ujangili kwenye hifadhi za Taifa zinazotuzunguka hasa vitendo vya kuwinda wanyama pori bila vibali vinavyotolewa na mamlaka husika”, alifafanua Mhe. Kobero.

Kuhusu Maboresho ya miundombinu ya Mahakama, Hakimu Mkazi huyo alisema yamesaidia kuleta uwazi na uhuru zaidi, kuongeza ari ya utendaji kazi kwa ufanisi na kwa kiwango cha juu katika suala zima la utoaji haki kwa haraka na wakati.

Akizungumzia matumizi ya Tehama, Mhe. Kobero alisema yamechagizwa na ufungwaji wa mkongo wa Taifa wa mawasiliano ambao umerahisisha shughuli za utoaji haki huku akitolea mfano wa mfumo wa uhuishaji mashauri (JSDS II) ambao unafanya kazi vizuri na kurahisisha upatikanaji wa taarifa za kumbukumbu za mashauri.

Naye Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara Bw. Jacob Swalle alisema morali ya watumishi katika utendaji kazi imeongezeka, aliongeza kuwa hivi sasa kila mtumishi ana chumba chake na pia jengo hilo linatumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Babati kuendesha shughuli za utoaji haki.

“Tunafarijika kuona mazingira yaliyo bora ya kuwahudumia wateja wetu wametengewa eneo bora la kusubiria wakati wa kupewa huduma za kimahakama kwani sasa tunaona haki ikitendeka kwa haraka na uhakika zaidi”, aliongeza Bw. Swalle.

Wakili wa Serikali Mwandamizi na Mkuu wa Mashitaka Mkoa wa Manyara Bw. Mutalemwa Kishenyi alisema uboreshaji miundombinu na usogezaji huduma karibu na wananchi kunaiwezesha Mahakama kuwa huru katika utoaji haki, kuondoa ucheleweshaji wa kutoa haki, kurejesha imani kwa wadau wake, huduma kufikika kwa urahisi zaidi na hivyo kuokoa muda na kumwezesha mwananchi kushiriki katika shughuli za kiuchumi.

Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Babati Bw. Halfan Ahmed Matipula alisema kama serikali wanafarijika kutokana na kusogezwa kwa huduma za kimahakama karibu zaidi na wananchi na changamoto nyingi za wadau sasa zitataliwa kwa haraka zaidi.

“Ofisi imekuwa ikipokea migogoro ya wananchi ambayo mingi inatokana na uelewa mdogo wa masuala ya kisheria tunashauri na kuwaelekeza sehemu sahihi ya kupeleka migogoro hiyo ili kila mtu apate haki yake kwa wakati na kwa uboreshaji huu basi wananchi watapata nafuu kubwa”. Alisema Katibu Tawala.  

 

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara Mhe. Simon Kobero 
Jengo la Mahakama Hakimu Mkazi Manyara 
Wakili wa Serikali Mwandamizi na Mkuu wa Mashitaka Mkoa wa Manyara Bw. Mutalemwa Kishenyi 
Jengo la Mahakama Hakimu Mkazi Manyara 

Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara Bw. Jacob Swalle

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni