Na Lydia Churi-Mahakama, Dodoma
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka
Majaji na Mahakimu watakaosikiliza mashauri yatakayotokana na uchaguzi Mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu kuandika hukumu hizo katika lugha
nyepesi, inayoeleweka na inayoelimisha wananchi.
Akifungua mafunzo ya namna bora ya
uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa Maafisa 282 wa Mahakama wakiwemo waheshimiwa Majaji leo jijini
Dodoma, Jaji Mkuu pia amewataka Wasajili kujitayarisha kutoa muhtasari wa hukumu
husika kwa lugha nyepesi kila hukumu inaposomwa baada ya shauri la uchaguzi
kukamilika ili wananchi waweze kujifunza.
“Katika mafunzo haya, kutakuwa na muwezeshaji atakayewaongoza
katika uandishi wa hukumu katika mashauri ya uchaguzi (Judgment Writing for
Election Petitions and Related Cases), hivyo tumieni wakati huu kujifunza
uandishi wa mihutasari yenye kubeba mafunzo kwa wananchi bila kutumia maneno ya
kisheria na kiufundi”, alisema.
Alisema Mahakama, inatakiwa kutenda haki, hivyo mafunzo hayo
ni sehemu ya matayarisho yatakayowezesha kutimiza wajibu huo wa kutoa haki
katika masuala ya Uchaguzi. Aliongeza kuwa Ibara ya 113 A ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, inawakumbusha Majaji, Mahakimu na Wasajili kutojiunga
na chama chochote cha siasa, isipokuwa wanayo haki ya kupiga kura iliyotajwa
katika ibara ya 5 ya Katiba.
“Katazo hili linatambua wajibu wetu Majaji, Wasajili na
Mahakimu ili Mahakama isionekane kupendelea au kukandamiza upande wowote
unaoshindana katika siasa na katika uchaguzi mkuu, lengo likiwa ni kuwatayarisha
Majaji na Mahakimu kusikiliza mashauri ya
uchaguzi kwa weledi, kwa wakati na kwa uwazi na haki”, alisema Jaji Mkuu.
Amewataka Majaji na Mahakimu kuamua mashauri ya uchaguzi kwa uwazi, utulivu, kujiamini na kuamini kile wanachokifanya
kwa mujibu wa sheria na utaratibu ili kuongeza imani ya wananchi kwa Jaji au
Hakimu husika na kwa Mahakama ya Tanzania kwa ujumla.
Alisema nafasi ya Mahakama katika kuisaidia Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwapa watanzania Uchaguzi huru na wa haki, usio na vitendo vya jinai ni kwa Mahakama kutimiza wajibu wake wa kupokea, kusikiliza na kutoa maamuzi katika mashauri ya jinai yatakayojitokeza katika hatua mbali mbali za uchaguzi kwa haraka.
Jaji Mkuu alisema kufunguliwa kwa mashauri ya kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani isichukuliwe kuwa ni kuonyesha udhaifu bali mashauri hayo yachukuliwe kuwa ni nafasi kwa wananchi kuhakikishiwa kuwa uchaguzi uliomalizika ulikuwa huru na wa haki kama Katiba ya Tanzania inavyotaka.
Alifafanua kuwa Katiba inampa Mwananchi haki ya kupiga kura, kugombea
nafasi ya uongozi na pia inampa haki ya kufungua shauri mahakamani. “Haki ya
kupiga kura na kupigiwa kura hazitakuwa maana endapo hazitaambatana na haki ya
kufungua shauri la uchaguzi pale mgombea anapoamini kuwa uchaguzi haukuwa huru
na wa haki’, alisema.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa
kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) yanalenga kuwajengea
uwezo maafisa wa Mahakama na kuwaandaa kutoa haki kwenye mashauri ya Uchaguzi
Mkuu ujao wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Awamu ya kwanza ya mafunzo yaliyoanza leo katika ukumbi wa
mikutano wa Takwimu-Dodoma yanawahusisha Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu,
Wasajili na Naibu Wasajili, na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu
Mkazi.
Aidha, awamu ya pili itawajumuisha waheshimiwa
Majaji wa Mahakama ya
Rufani na yatafanyika Septemba 2-4, 2020 mkoani Morogoro. Mahakimu Wakazi
Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya nao watapatiwa mafunzo hayo baadaye katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama
Lushoto-Tanga.
Wawezeshaji wa mafunzo hayo ni baadhi ya Majaji wa Mahakama
ya Rufani na Mahakama Kuu waliopo na wastaafu, Naibu wasajili, Mahakimu pamoja
na wawezeshaji kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Tume ya Kurekebisha Sheria
ambao ni wadau muhumu katika masuala ya Uchaguzi.
Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na baadhi ya viongozi wengine wa Mahakama ya Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma mara baada ya kufungua Mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa Maafisa wa Mahakama, leo jijini Dodoma. Waliokaa wa pili kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Arusha Mhe. Mohamed Gwae akichangia mada wakati wa mafunzo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dar es salaam Mhe. Lameck Mlacha akichangia mada wakati wa mafunzo.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifungua mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa Maafisa wa Mahakama 282, leo jijini Dodoma.
Baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa kwenye Mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa Maafisa wa Mahakama, leo jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni