Na
Mary Gwera, Mahakama
Shirika
la Haki Miliki Duniani (WIPO), limeipongeza Mahakama ya Tanzania kwa mafanikio
katika utekelezaji wa Mradi wa Haki Miliki nchini.
Akizungumza
katika Mkutano wa Nchi Wanachama uliofanyika kwa njia ya video ‘video
conference’, mapema Septemba 01 mwaka huu, Afisa Programu kutoka Shirika hilo,
Bi. Alexandra Bhattacharya ameisifu Mahakama kwa utekelezaji mzuri wa Mradi huo
na kuahidi kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu zaidi.
“Napenda
kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa
kujitoa kwa dhati kupigania mradi huu kuwa ajenda ya Mahakama na ya kitaifa kwa
ujumla,” alisema Bi. Bhattacharya.
Katika
mkutano huo, Mahakama ya Tanzania imetoa uzoefu wake katika utekelezaji wa
Mradi wa Haki Miliki kwa nchi Wanachama wa Shirika hilo, ambapo Mhe. Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya
Mahakama walishuhudia wasilisho hilo.
Akiwasilisha
andiko lake katika Kikao cha WIPO kilichofanyika kwa njia ya video, Mratibu wa Mradi huo kutoka Mahakama ya Tanzania, Mhe. Upendo Ngitiri amewaeleza
Wajumbe wa mkutano huo kuwa Mahakama imefanikiwa katika utekelezaji wa Mradi
huo kutokana na uongozi madhubuti wa Mhe. Jaji Mkuu.
“Mahakama
ya Tanzania imefanikiwa katika utekelezaji wa mradi huu, ikiwa ni pamoja na
kutoa mafunzo ya haki miliki kwa Wahe. Majaji na Mahakimu, vilevile programu ya
Mafunzo ya Haki Miliki imefanikiwa kuingizwa katika Mpango Mkuu wa Mafunzo wa
Mahakama ya Tanzania,” alieleza Mhe. Ngitiri ambaye pia ni Hakimu Mkazi kutoka
Kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri-Mahakama.
Kwa
mujibu wa Mhe. Ngitiri, alisema Mahakama pia inaendelea na maandalizi ya
uandaaji wa majumuisho ya sheria na kesi zinazohusu hati miliki na kuongeza
kuwa Mhimili huo pia uko mbioni kusaini hati ya makubaliano (MoU) na WIPO lengo
likiwa ni kuimarisha mahusiano na ushirikiano zaidi.
Aidha,
Mhe. Ngitiri aliwapa uzoefu wajumbe wa kikao hicho na kuwaeleza kuwa ili kufanikisha uanzishwaji na
utekelezaji wa Miradi inayohusisha
taasisi za kimataifa ni muhimu kuzingatia
sera ya nchi na tasisi wanazotoka, kuzingatia mikataba na sera ya
kimataifa,kuangalia mahitaji ya nchi na kujitoa kwa ajili ya nchi yako.
Mahakama
ya Tanzania ilianza kutekeleza mradi wa WIPO mwaka 2018, faida za mradi huo ni
pamoja na kuwajengea Maafisa wa Mahakama uwezo wa kuamua vyema mashauri
yanayotokana na uvunjifu wa haki miliki ikiwemo migogoro inayotokana na wizi wa
alama za biashara.
Vilevile,
kuwajengea uwezo Maafisa wa Mahakama katika eneo la Usuluhishi (ADR) na kutoa
fursa kwa Majaji wa Tanzania kubadilishana uzoefu na Majaji wa nchi mbalimbali
katika eneo la utoaji haki kupitia Taasisi ya Uongozi wa Mahakama ya WIPO (WIPO
Judicial Institute).
Mkutano
huo wa WIPO uliofanyika kwa njia ya Video ulishikisha Viongozi Waandamizi
Serikali kutoka nchi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Switzerland, Sweden, Malawi,
Cambodia, Uganda, Rwanda, Nepal, Ethiopia, Zambia, Msumbiji na nyinginezo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni