Na Innocent Kansha – Mahakama Dodoma.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dodoma Mhe. Mustapher Siyani amewataka
Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama ya Tanzania kusikiliza mashauri uchaguzi kwa
kuzingatia weledi na kutenda haki ili wasiathiri Imani ya wananchi kwa Mhimili
wa Mahakama.
Akifungua awamu ya tatu
ya mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa Mashauri ya uchanguzi kwa Waheshimiwa
Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi Tanzania, Jaji Siyani amewataka
Mahakimu hao wafawidhi kusimamia masjala
kwa karibu zaidi, ili mashauri yanayofunguliwa yaweze kushughulikiwa ndani ya
muda stahiki.
Jaji Mfawidhi
aliwakumbusha Mahakimu hao kutilia mkazo matumizi ya Teknologia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) ili mashauri yanayofunguliwa kwa njia ya mtandao (E-Filing)
yaweze kusikilizwa na kumalizika kwa wakati.
“Mafunzo haya ni muhimu
kwenu binafsi na Mahakama kama taasisi, umuhimu wake hauelezeki kwa maneno
mepesi, kwa wale ambao wamewahi kusikiliza mashauri ya uchaguzi wanaelewa nini
ninachozungumzia hapa”, alisistiza Jaji Siyani.
Alisema, katika
kuyashughulikia mashauri yatokanayo na uchaguzi, suala la muda ni jambo la
muhimu kwani viongozi wa ngazi za juu wa Mahakama pia wameelekeza mashauri hayo
kutodumu Mahakamani kwa zaidi ya miezi minne tu na si vinginevyo, hivyo
amewataka Mahakimu hao kujiandaa kutekeleza majukumu maelekezo hayo muhimu.
Jaji Mfawidhi alisema
Mahakama haiwezi kujitenga na mchakato wa kidemokrasia wa nchi yetu,hivyo ushiriki
wa muhimili uko katika hatua zote ikiwemo kabla ya kuanza kwa uchaguzi na hata
baada ya matokeo kutangazwa. Aliongeza kuwa Ibara ya 107 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania imetamka dhahiri kuwa Mahakama ndicho chombo chenye kauli ya mwisho
katika kutoa haki.
Alifafanua kuwa mara
baada ya uchaguzi Mkuu, Mahakama zimepewa mamlaka ya kushughulikia malalamiko
yatokanayo na uchaguzi huo, hivyo baada ya muda mfupi, mashauri hayo yataanza
kufunguliwa kwenye Mahakama mbalimbali nchini
Mahakama ya Tanzania
kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto inaendelea kutoa mafunzo
kwa watumishi mbalimbali ili kuwajengea uwezo waweze kutekeleza majukumu yao
hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu ujao wa mwaka huu.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma (katikati
mstari wa mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kufungua mafunzo ya
namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa Mahakimu Wakazi Wafawidhi
wa Mahakama za Hakimu Mkazi Tanzania, kushoto kwake ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi
wa Mahakama Lushoto ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt Paul
Kihwelo na kulia ni Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Robert Makaramba.
Baadhi
ya washiliki wa mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa
Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi Tanzania yanayoendelea huo wakifuatilia.
Jaji
mstaafu wa Mahakama kuu ya Tanzania Mhe. Robert Makaramba ambaye ni mkufunzi wa
mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa Mahakimu Wakazi
Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi Tanzania akitoa mada.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni