Na Innocent Kansha – Mahakama Dodoma.
Msajili wa Mahakama Kuu
ya Tanzania Mhe. Sharmillah Sarwatt amewakumbusha Naibu Wasajili wa Mahakama
Kuu ya Tanzania kutumia mamlaka waliyopewa kurejesha taswira chanya na imani ya
wananchi na wadau kwa Mahakama hasa katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa
kufanyika Oktoba mwaka huu.
Akitoa kuhusu Uongozi
kwenye mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi Jijini Dodoma
kwa baadhi ya Wasajili na Naibu Wasajili wa Mahakama, Msajili wa Mahakama Kuu amesema
kiongozi aliyeaminiwa siku zote ni lazima atumie busara katika kutekeleza
majukumu yake na hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi kwa kuonyesha umahiri
katika kuitumikia nafasi ya kiutawala.
“Tuchunge kauli zetu
zisije kukinzana na viapo vyetu vya utumishi kwenye suala zima la utawala wa
sheria, tumeaniniwa katika nafasi hizi za uongozi wasajili ndiyo injini ya
Mahakama katika suala zima la kuratibu shughuli zote za mashauri”, alisisitiza
Mhe. Sarwatt.
Alisema wasajili wanapaswa
kutekeleza majukumu yao katika kiwango cha hali ya juu na kwa weledi uliotukuka
kwa maslahi mapana ya Taifa kwani uchaguzi siyo jambo dogo, linagusa ustawi wa
Taifa na maisha ya wananchi wote.
Aliongeza kuwa hatima ya
Mahakama ipo mikononi mwa watumishi hao katika kusimamaia chombo hiki muhimu cha utoaji haki,
kwa kipindi hiki cha uchaguzi ni muhimu kufanya kazi bila woga, ujasiri na
kuisaidia Mahakama kufikia lengo.
“Kama viongozi mnapaswa kuzingatia
maadili ya kazi katika maeneo mnayoyaongoza ni jambo la msingi hasa katika
kipindi hiki cha uchaguzi yapaswa kuonyesha mfano kwa watumishi wengine,
alisisitiza.
Kwa ujibu wa Mhe. Sarwatt,
majukumu ya Msajili kwa kuzingatia na kufuata kanuni za uchaguzi, kanuni ya 9(1)
zimetoa mamlaka ya kukutaka baada ya kupokea nyaraka za shauri la uchaguzi
kabla ya yote kufanya mambo makuu matatu ambayo ni kupokea na kusajili shauri
endapo tu limekidhi vigezo vya kisheria kwa taratibu za kikanuni, kurudisha kwa
maana ya kuwasiliana na mleta nyaraka hizo mahakamani kwa nia ya kushauriana
namna bora ya kuwasilisha nyaraka husika na mwisho ni kutopokea na kusajili
hati hizo za shauri kwa kutoa sababu zenye mashiko ya kisheria au kwa
kuzingatia kanuni ya kutozipokea na kuzisajili kama shauri Mahakamani.
“Tunatakiwa kuwa bora
kuliko jana kwa kuongeza bidii katika majukumu yetu na kutambua maeneo ambayo
hatupo vizuri ili kuongeza juhudi lengo ikiwa ni kupata matokeo chanya ya
utekelezaji wa jukumu la kikatiba kwa Mahakama”, alisema Msajili huyo.
Mgeni rasmi kwenye
mafunzo ya Namna bora ya uendeshaji wa Mashauri ya Uchaguzi, Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dodoma Mhe. Mustapher Siyani akiwa kwenye
picha ya pamoja na Wasajili na Naibu Wasajili. Wa kwanza kulia ni Jaji
mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Robert Makaramba na wa kwanza kushoto ni Mkuu
wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Jaji Mhe. Dkt. Paul kihwelo na wa pili kutoka kushoto ni
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Sharmillah Sarwatt.
Mkuu wa chuo cha Uongozi
wa Mahakama Lushoto (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (mwenye tai nyekundu) akitoa ufafanuzi wa jambo wakati mafunzo
hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni