Na Innocent Kansha – Mahakama
Mtendaji
Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru amewataka Maafisa Utumishi
na Utawala wa Mahakama kutumia vyema tovuti rasmi za kiserikali zenye miongozo
mbalimbali ya kiutendaji kazi itakazowawezesha kufanya kazi kwa ufanisi.
Akifungua
rasmi kikao kazi cha siku mbili cha Maafisa hao mapema Septemba 03
kinachofanyika katika Ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam, Bw. Kabunduguru
alisema kuwa maamuzi yoyote yanayofanywa na Kiongozi lazima yazingatie miongozo
ya kisheria na sababu za maamuzi hayo ni
lazima zifuate utaratibu stahiki.
“Nataka
muwe watawala wenye kufanya kazi zenu kwa umakini mkubwa kwa kuzingatia uweledi
wa taaluma zenu, acheni kutumia mitandao ya kijamii badala yake someni tovuti
rasmi za kiserikali kuna miongozo na mambo mengi mazuri ya kuwaongezea ujuzi wa
kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa”, alisisitiza Mtendaji Mkuu.
Aliwataka
pia kuhakikisha wanakuwa na nyaraka zote muhimu za sheria, kanuni na miongozo
mbalimbali ya kazi zenu itawasaidia kujua taratibu za majukumu yenu ya
kuwaongoza watumishi wenzenu na kuwaongezea uwezo wa kupata maarifa ya ziada,
alieleza Mtendaji Mkuu.
Aidha,
Bw. Kabundunguru aliongeza kuwa matarajio ya Mahakama baada ya kumalizika kwa
kikao kazi hicho ni kutumika kama suluhisho la kupanga mikakati ya namna bora
ya kusimamia na kuboresha baadhi ya mambo kama vile usimamizi wa rasilimali
watu ikihusisha mahudhulio, maadili na mahusiano kazini, miundo ya maendeleo ya
utumishi, upimaji wa utendaji kazi unaozingatia taratibu zilizowekwa.
Maeneo
mengine aliyoyasisitiza Mtendaji Mkuu ni uwasilishaji wa nyaraka kwa kuzingatia
maelekezo, kuwasilisha maombi ya watumishi baada ya kufanya upembuzi yakinifu,
usimamizi madhubuti wa kumbukumbu na nyaraka za kitaasisi na usimamizi
madhubuti wa miundombinu, vyombo vya usafiri na mali nyingine za Umma.
Kwa
upande mwingine, Mtendaji Mkuu huyo aliwasisitiza Maafisa hao kuzingatia na
kuendeleza ushirikiano na Mihimili mingine ya Serikali katika kutimiza majukumu
yao.
“Tafuteni
namna bora ya kufanya kazi na kupunguza malalamiko, Mahakama kama muhimili upo
huru na unajitegemea katika kutimiza majukumu yake ya kikatiba, ila hauwezi
kufanya kazi peke yake bila ushirikiano na taasisi zingine, tambueni kuwa Wakuu
wa Wilaya na Mikoa ni wenyeviti katika kamati za maadili ya watumishi wa Mahakama
kwa kupitia Sheria na. 4 ya mwaka 2011 ya uendeshaji wa Mahakama,” alisisitiza.
Hata
hivyo, Bw. Kabundunguru alieleza kuwa anatambua changamoto mbalimbali zinazoikabili
Mahakama ikiwa ni pamoja na uhaba wa miundombinu hasa ya majengo kwa baadhi ya
maeneo ya kazi ila aliwahakikishia kuwa Mahakama itaendelea kuboresha
miundombinu ya majengo kwa kukarabati na kujenga majengo mapya kwa awamu na
hatimae kumaliza changamoto hiyo.
Kwa
upande mwingine, Bw. Kabunduguru alisema kazi kubwa imefanyika kwenye usanifu,
ujenzi pamoja na usimikaji na usimamizi wa mifumo ya mbalimbali ikiwemo mfumo
wa kuratibu na kusimamia uendeshaji wa mashauri (JSDS II), ambao umerahisisha
upatikanaji wa Takwimu na kuongeza uwajibikaji na uwazi kwenye mwenendo wa
mashauri na pia kuongeza imani ya wadau na umma kwa Mahakama.
Mtendaji
Mkuu alizungumzia juu ya Mpango Mkakati mpya wa Mahakama ya Tanzania utakaoanza
mwaka 2020/2021 hadi 2024/2025 ambao utaendeleza mikakati ya kuboresha
miundombinu na kuongeza matumizi ya TEHAMA kuboresha zaidi shughuli za kimahakama.
Baadhi
ya Maafisa Utumishi na Tawala wa Mahakama ya Tanzania wakimsikiliza Mgeni rasmi
alipokuwa akifungua kikao kazi kinachofanyika katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es
Salaam.
Mtendaji
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha akisisitiza jambo mbele ya
washiriki wa kikao kazi.
Baadhi
ya Maafisa Utumishi na Tawala wa Mahakama ya Tanzania wakifuatilia kikao hicho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni