Jumamosi, 5 Septemba 2020

WANANCHI WAELIMISHWE TARATIBU ZA MASHAURI YA UCHAGUZI

Na Lydia Churi-Mahakama, Morogoro

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo amefunga mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani na kuwataka Majaji hao kuamua mashauri ya uchaguzi kwa kutumia lugha rahisi na inayoeleweka vizuri kwa wananchi.

Jaji Mkuu pia ametoa wito kwa watumishi mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania wakiwemo Majaji na Mahakimu kuwaelimisha wananchi ili wafahamu taratibu zinazopaswa kufuatwa katika mashauri yanayohusu uchaguzi ili kurahisisha suala la upatikanaji wa haki kwa wakati.

“Kanuni za uchaguzi zielimishwe kwa wananchu kupitia vyombo vya habari na zielimishwe kwa lugha ya Kiswahili ili wananchi walio wengi waelewe na pia kuepuka upotoshaji”, alisisitiza.

Jaji Mkuu pia amewashauri waheshimiwa Majaji kuwa makini na afya zao kwa kuwa wanayo kazi kubwa katika jamii ambayo ni kutoa wa haki.”Angalieni afya zenu kwa uangalifu mkubwa kwani tunatoa huduma muhimu kwa jamii”, alisema.

Wakati huo huo, Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Omar Othman Makungu ameishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kumualika kuhudhuria mafunzo hayo kwa kuwa hatua hiyo ni kuimarisha Muungano na kuendeleza ushirikiano katika masuala ya utoaji haki.

Alisema amefaidika na mafunzo hayo kwa kuwa yamewaandaa na kuwaweka tayari kusikiliza mashauri yatakayotokana na uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu. Aliongeza kuwa Mahakama ya Zanzibar pia inaandaa mafunzo ya aina hii ambayo yanatarajiwa kufanyika mapema mwezi Oktoba.

Naye Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Bethuel Mmila akizungumza kwa niaba ya Majaji wa Mahakama hiyo, ameishauri Mahakama kuandaa mafunzo kama hayo kwa aina nyingine za mashauri ili kuendelea kuwajengea uwezo na uzoefu katika kutoa maamuzi yanayowakabili.

Mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika kwa nyakati tofauti na yanawahusisha Maafisa wa Mahakama wa ngazi mbalimbali wakiwemo Majaji, Wasajili, Mahakimu na Wasaidizi wa Sheria wa Majaji.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifunga mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani yaliyofanyika Mjini Morogoro.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitazama cheti alichokabidhiwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Bethuel Mmila baada ya kumaliza mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani yaliyofanyika Mjini Morogoro.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimkabidhi cheti Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Rehema Kerefu Sameji baada ya kumaliza mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani yaliyofanyika Mjini Morogoro.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimkabidhi cheti Jaji Mkuu wa Zanzibar baada ya kumaliza mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani yaliyofanyika Mjini Morogoro.



 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni