Na Lydia Churi-Mahakama, Mwanza
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi ameiomba
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa-Takukuru kuwaelimisha wananchi na
kuyachunguza malalamiko ya rushwa dhidi ya Mahakama kwani mengine hutokana na
wananchi kutofahamu taratibu mbalimbali za Mahakama.
Akizungumza
na Mkuu wa wilaya ya Magu Mkoani Mwanza Pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi
na Usalama ya wilaya Magu, Jaji Kiongozi amesema tuhuma za rushwa dhidi ya
Mahakama zinaweza kusababishwa na wananchi kutofahamu taratibu za utendaji kazi
wa Mhimili huo ikiwemo jinsi ya upatikanaji wa nakala za hukumu, mwenendo wa
shauri na namna ya usikilizwaji wa mashauri katika ngazi mbalimbali za
Mahakama.
“Mahakama
haijishirikishi na vitendo vya rushwa wala haiwalindi wanaojihusisha na vitendo
hivyo”, alisema Jaji Kiongozi na kuongeza kuwa vitendo vya rushwa hufanywa na
mtumishi mwenyewe asiye na maadili.
Alisema
Mahakama haitasita kuwachukulia hatua kali za kinidhamu watumishi wake wanaojihusisha
na vitendo vya rushwa na imekuwa ikifanya hivyo wakati wote.
Kuhusu
upatikanaji wa nakala za hukumu, Jaji Kiongozi alisema Mahakama ilianzisha
huduma ya usambazaji wa nyaraka zake mbalimbali iitwayo Posta Mlangoni baada ya
kuingia mkataba na shirika la Posta Tanzania ambapo hivi sasa nakala za hukumu
Pamoja na nyaraka nyingine husambazwa na kufikishwa moja kwa moja kwa wananchi.
Alisema
licha ya kuwepo kwa huduma hiyo, bado kuna baadhi ya wananchi ambao hawajaikubali
huduma hiyo na kutaka kufika wenyewe mahakamani kuchukua nakala za hukumu hivyo
pamoja na Mahakama kuwaelimisha wananchi, ameiomba pia Takukuru kuwaelimisha
wananchi wanaopeleka malalamiko ya aina hiyo dhidi ya Mahakama.
Wakati huo huo, Mkuu wa wilaya ya Misungwi Bw.
Juma Samwel Sweda ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa maboresho ya huduma zake
ikiwemo kujenga na kukarabati majengo yake na kuongeza kasi katika usikilizaji
wa mashauri. “Hivi sasa majengo yanajengwa na mashauri yanapungua hususan
kwenye mahakama ya wilaya ya Misungwi”, alisisitiza.
Mkuu
huyo wa wilaya pia aliiomba Mahakama ya Tanzania kuangalia uwezekano wa kujenga
jengo la kisasa la Mahakama ya wilaya ya Misungwi kwa kuwa jengo lililopo hivi
sasa ni dogo ukilinganisha na mahitaji halisi.
Jaji Kiongozi anaendelea na ziara yake ya
kikazi kwenye Mkoa wa Geita ambao ni sehemu ya Mahakama Kuu kanda ya Mwanza.
Kiongozi huyo anatarajiwa kukagua shughuli za Mahakama katika wilaya za Chato na
Bukombe.
Watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Magu wakimsikilza Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi alipozungumza nao.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (wa nne kushoto), Mkuu wa wilaya ya Magu Bw. Salum Kali (wa nne kulia) na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Mwanza Mhe. Sam Rumanyika wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo na baadhi ya Viongozi wa Mahakama ya Tanzania wakati Jaji Kiongozi alipomtembelea Mkuu huyo wa wilaya ofisini kwake.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa wilaya ya Kwimba (wa pili kulia) pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya na Viongozi kutoka Mahakama ya Tanzania.Wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Mwanza Mhe. Sam Rumanyika.
Watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Kwimbawakimsikilza Jaji Kiongozi alipozungumza nao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni