Jumamosi, 10 Oktoba 2020

MAHAKAMA YA MWANZO UYOLE YAZINDULIWA

Na Rajabu Singana, Mahakama Kuu Mbeya

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Dkt. John Utamwa ameushukuru uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kujenga jengo la kisasa la Mahakama ya Mwanzo Uyole ambalo amesema litawawezesha kufanya kazi kwa ufanisi na utulivu na litakuwa ni chanzo cha watu kupata haki zao kwa wakati.

Akizindua jengo hilo mjini Mbeya hivi karibuni, Jaji Dkt. Utamwa pia aliwakumbusha watumishi pamoja na wadau kwa ujumla kuwa ni jukumu la kila mmoja kulitunza na kulilinda jengo hilo kwa sababu kutokana na uwepo wa vitendo viovu vinavyoweza kupelekea uhujumu wa miundombinu ya taasisi za Umma.

“Waswahili hutumia msemo wa kitunze kikutunze wanaposisitiza kuwa, ukiwa na kitu chochote kizuri, ni vema kukitunza ili kiweze kukusaidia zaidi. Ninatoa msisitizo wa jambo hili kwa kuwa, historia ya Mahakama hii inatia mashaka hasa kwa kufahamu kuwa iliwahi kuungua moto”  

Taarifa ya uzinduzi wa jengo hilo iliyotolewa na Ofisi ya Mtendaji wa Mahakama Kuu kanda ya ilieleza kwamba mnamo tarehe 5/5/2018 watu waovu wasiojulikana walichoma moto jengo lililokuwepo na kusababisha kuungua vifaa vyote vilivyokuwemo ndani zikiwemo samani, majalada yaliyokwisha na yaliyokuwa yanaendelea pamoja na vielelezo vya mashauri.

Aidha, Kutokana na umuhimu wa Mahakama hiyo Uongozi wa Mahakama ya Tanzania ulichukua jitihada za haraka na kuanza ujenzi wa jengo jipya ili kuwaondolea wananchi usumbufu wa kufuata huduma za Mahakama kwa umbali mrefu.

Mahakama ya Mwanzo Uyole ni miongoni mwa Mahakama za Mwanzo nane (8) za Wilaya ya Mbeya zinazohudumia wananchi wa Jiji la Mbeya na Wilaya ya Mbeya Vijijini inayohudumia Kata zipatazo 14. Ujenzi wa Mahakama hii ulianza rasmi tarehe 22 Desemba, 2018 na Mkandarasi PIM Innovators CO. LTD akisimamiwa na Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA). 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mbeya Mhe. Dkt. John Utamwa akikata utepe kuzindua Jengo la Mahakama ya Mwanzo Uyole iliyoko Mbeya mjini. Kushoto ni Jaji wa Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Mbeya Mhe. Dkt. Adam Mambi na kulia ni Jaji wa Mahakama kuu kanda hiyo Mhe. Dunstan Ndunguru. 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mbeya Mhe. Dkt. John Utamwa akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mbeya Mhe. Dkt. John Utamwa akiwa katika picha ya pamoja na Waheshimiwa Majaji wa kanda ya Mbeya pamoja na watumishi wengine na Viongozi wa Dini wakati wa hafla ya uzinduzi.


 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni