Na Francisca Swai-Mahakama, Musoma.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Musoma Mhe. Ephery Sedekia Kisanya, amemtaka mkandarasi ( Moladi Tanzania Limited) anayeendelea na ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya Bunda kukamilisha ujenzi wa jengo hilo kwa wakati uliopangwa.
Akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Mahakama ya wilaya ya Bunda hivi karibuni, Jaji Kisanya amemtaka Mkandarasi huyo kuharakisha ujenzi ili kuboresha huduma za Mahakama katika wilaya hiyo kwani hivi sasa inatumia jengo la kupanga ambalo halina miundombinu ya kimahakama.
Kwa mujibu wa Jaji Kisanya, Mahakama ya wilaya ya Bunda hivi sasa inaendesha shughuli zake katika eneo finyu hivyo watumishi wanatoa huduma katika mazingira magumu pia kodi kubwa inalipwa ambayo ingeelekezwa kwenye shughuli nyingine za maendeleo.
Aidha, Mhe. Kisanya amempongeza Mtendaji wa Kata ya Mcharo iliyoko wilayani Bunda, Bw. Yelaniah Chacha Motte, kwa uvumilivu wao na kuazima chumba kimoja katika jengo lao la kata ambacho kinatumika kama Mahakama ya Mwanzo Mcharo kwani majengo ya Mahakama hiyo ni ya zamani sana na chakavu na kuwaasa watumishi wa Mahakama hiyo kuendeleza ushirikiano na wadau hao.
Mhe. Kisanya Kisanya pia alitembelea wilaya ya Serengeti ambapo Mtendaji wa Mahakama kuu kanda ya Musoma Bw. Festo Chonya, alimueleza Mhe Jaji kuwa, katika mwaka huu wa fedha wana mpango wa kuanza ujenzi mdogo wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Mugumu Mjini katika eneo lililopo la Mahakama ya Wilaya Serengeti kwa kutumia fedha za matumizi ya kawaida (OC).
Bw. Chonya alisema wameamua kufanya hivyo kutokana na Mahakama ya Mwanzo Mugumu mjini kutumia jengo la Halmashauri ambalo pia ni chakavu na finyu.
Wakati huo huo Jaji Kisanya aliwapongeza watumishi wa Mahakama kwa utendaji wao mzuri wa kazi na kuwaasa kuendelea kujituma na kufanya kazi kwa kuzingatia maadili, na pale wanapopata nafasi kujiendeleza ili kupata vigezo vitakavyowawezesha kupanda vyeo na kuboresha utendaji kazi zaidi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni