Jumamosi, 10 Oktoba 2020

WATUMISHI WA MAHAKAMA KUU SONGEA WATEMBELEA HIFADHI YA TAIFA YA RUAHA

Na Brian Haule-Mahakama, Songea

Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa kanda hiyo Mhe. Sekela Cyril Moshi wametembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ili kujifunza uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yake kwa lengo la kuongeza ujuzi utakaosaidia katika kushughulikia mashauri yanayohusu ujangili wa wanyamapori.

Watumishi hao walipata wasaa huo wa kutembelea hifadhi ya Ruaha hivi karibuni ambapo pia walitumia muda huo kujadili changamoto mbalimbali zinazotokana na mashauri yanayohusu nyara za Serikali hususan ujangili wa wanyamapori.

Akielezea changamoto katika usikilizwaji wa mashauri yanayohusu ujangili wa wanyamapori, Jaji Mfawidhi wa kanda ya Songea alisema mashauri hayo huchelewa kumalizika mahakamani kutokana na upelelezi wake kuchukua muda mrefu.

Kuhusu dhamana alisema ni haki ya mshtakiwa hivyo aliwataka Mahakimu kutotoa masharti magumu ya dhamana ambayo yako nje ya sheria kwani kwa kufanya hivyo ni kumnyima mshtakiwa haki ya dhamana.

Kwa upande wake Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea Mhe. Isaya Arufani alisema Suala la dhamana lichukuliwe kama ni hatua ya kusubiri kesi kusikilizwa.

“Tunaweza tukampa mshtakiwa masharti magumu ya dhamana akakaa huko gerezani muda mrefu, tukajikuta hatufikiii lengo na lengo ni kufikia maamuzi ya mwisho”, alisisitiza Mhe. Arufani.

Naye Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Mbinga Mhe. Aziza Hassan Mbajo alisema katika usikilizaji wa mashauri ya ujangili kila anayehusika, yaani Mahakama ana wadau wake wanapaswa kutimiza wajibu kwa wakati.

Bwana Kolady Kayanda Msimamizi wa Mradi wa Faru kutoka Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF) ofisi ya Masasi, alisema Kesi zinazohusu nyara za serikali zinapokaa mahakamani kwa muda mrefu  huwafanya wao kushindwa kuendelea na hatua nyingine zaidi.

Meneja Mawasiliano wa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF) Bi Joan Itanisa alisema ziara ya Watumishi wa Mahakama itasaidia kuweka uelewa wa pamoja kati ya Mahakama na Taasisi hiyo ili wawe kitu kimoja katika kuhifadhi rasilimali za Taifa.

Ziara ya watumishi wa Mahakama kanda ya Songea ilidhaminiwa na Shirika la Kimataifa la Hifadhi ya Mazingira (WWF) na kuendeshwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Songea Mhe. Sekela Cyril Moshi (kushoto) na Jaji wa Kanda hiyo Mhe. Isaya Arufani wakifuatilia mazungumzo na watumishi pamoja na wenyeji wao wakati wa ziara ya Watumishi wa Mahakama Kuu kanda ya Songea katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha. 
Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Songea wakiwa kwenye mazungumzo wakati wa ziara yao katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha. 

Msimamizi wa Mradi wa Faru wa Shirika la kimataifa la hifadhi ya wanyamapori (WWF) Bw. Kolady Kayanda akielezea jambo kwa watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Songea walipotembelea hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni