Alhamisi, 15 Oktoba 2020

WASAIDIZI WA SHERIA WA MAJAJI RUFANI WAFUNDWA MASHAURI YA UCHAGUZI

Na Mwandishi wetu, IJA-lushoto

Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman amewataka Wasaidizi wa Sheria wa Majaji kutumia taaluma yao na kuzingatia umahiri na weledi katika uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi sambamba na kujiepusha na ushabiki wa kisiasa.

Akifungua mafunzo ya Wasaidizi wa sheria 39 wa Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania juu ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi hivi karibuni yaliyofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mh. Chande aliwaomba washiriki hao kuzingatia na kufuatilia mafunzo hayo kikamilifu ili wakayatumie katika utekelezaji wa majukumu yao .

“Mkiwa kama wasaidizi wa Sheria wa Majaji ni vyema kutumia taaluma yenu vizuri na kuzingatia umahiri na weledi katika uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi na kujiepusha na ushabiki wa kisiasa,” alisisitiza Jaji Chande.

Aidha, Mhe. Chande aliwataka washiriki hao kufanya kazi kwa kuzingatia maadili, umakini na kujiamini katika uandishi wa hukumu hivyo wanalazimika kuendelea kujinoa ili kuendana na kasi ya mabadiliko na izingatwe kuwa wao ni msaada mkubwa kwa Wahe. Majaji katika utekelezaji wa majukumu ya utoaji wa haki. 

Kwa upande mwingine, Jaji Chande aliupongeza Uongozi wa Mahakama ya Tanzania na wa Chuo hicho kwa kuwa mstari mbele katika kufanikisha mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa mbalimbali wa Mahakama katika kushughulikia mashauri ya Uchaguzi.

Mpaka sasa Mahakama kwa kushirikiana na Chuo tayari imeshafanya mafunzo ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa Maafisa mbalimbali wa Mahakama ikiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Zanzibar, Naibu Wasajili, Mahakimu Wakazi Wafawidhi lengo likiwa ni kuwawezesha kuyashughulikia kwa ustadi zaidi na kwa wakati.

Jaji Mkuu (Mstaafu), Mhe. Mohamed Chande Othman akifungua rasmi Mafunzo kwa Wasaidizi wa sheria wa Majaji juu ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi yaliyofanyika katika Chuo cha uongozi wa Mahakama Lushoto.

 Mkuu wa Chuo Cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo  akiwakaribisha washiriki hao katika hayo.

Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu (Mstaafu) Mhe. Mohamed Chande Othman, Jaji wa Mahakama Kuu Mstaafu Mhe. Robert Makaramba (Kulia) na Jaji wa Mhakama Kuu na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo (kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu - Mahakama ya Tanzania Bw Edward J. Nkembo (kulia), Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Bw. Joseph Mwaiswelo (katikati) na Hakimu Mahakama ya Wilaya Lushoto Mhe.  Japhet Manyama (kushoto).

Mgeni rasmi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni