Na Innocent kansha – Mahakama Muleba.
Msajili
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma amewataka Mahakimu kutumia vizuri
mamlaka ya kisheria waliyopewa ili kutatua tatizo la ucheleweshaji wa ufungaji wa
mashauri ya Mirathi mahakamani.
Akizungumza
kwa nyakati tofauti na Watumishi wa Mahakama za Wilaya za Biharamulo na Muleba
katika ziara yake inayoendelea kwenye Kanda ya Bukoba, Mhe. Chuma alisema
uzoefu unaonesha kuwa Mahakimu walio wengi wanapomaliza kusikiliza mashauri ya
aina hii kwa hatua ya kuteua wasimamizi wa mirathi hawaweki amri za kuwakumbusha
wadaawa kurudi mahakamani kufunga Mirathi yao.
“Someni
sheria hiyo vizuri ili muweze kuitumia kwa ukamilifu wake tuweze kupunguza
tatizo hili, kuna hadi adhabu zimewekwa kwenye sheria ya mirathi kama msimamizi
wa mirathi atashindwa kukamilisha zoezi hilo kwa njia rasmi zilizowekwa na
zinazokubalika”, alifafanua.
Mhe.
Chuma aliwataka Mahakimu kutumia muda uliobaki hadi kufikia mwisho wa mwezi Disemba
2020 kumaliza mashauri ya mlundikano katika Mahakama zao. Aliongeza kuwa endapo
kila Hakimu ataonesha bidii ya kazi na kasi ya usikilizaji wa mashauri yake,
hili linawezekana.
Aidha,
aliwataka watumishi wa Mahakama kutunza na kuzingatia maadili pindi
wanapotimiza majukumu yao na kulinda viapo vyao kama vinavyojieleza. Alisema mahakama
haitegemei kusikia mtumishi analalamikiwa kwa kushindwa kutunza maadili ya kazi
zake pale anapowajibika.
‘’Malalamiko
mahakamani yatamalizika endapo kila mtumishi atawajibika ipasavyo kwa nafasi
yake, kila mtumishi atambue kuwa ana nafasi kubwa ya kufanya mageuzi makubwa ya
kiutendaji na kuhakikisha Mahakama inakuwa kioo na mfano wa kuigwa kwa jamii
tunayoihudumia, alisema.
Alisema,
Mahakama inakemea kwa nguvu zote watumishi kujihusisha na vitendo vya rushwa
kwani vinapoteza imani na kuchafua taswira nzuri ya Taasisi kwa wananchi. “Yeyote
atakayebainika kujihusisha na vitendo
hivi hatutasita kumchulia hatua kali za
kinidhamu ikiwemo kumwondoa kazini.
Kwa
upande wa matumizi ya Tehama ndani ya Mahakama, Msajili Mkuu amewataka
watumishi kutenga muda wa kutembelea mara kwa mara mitandao ya kijamii ya
Mahakama ili waweze kupata habari na taarifa mbalimbali za shughuli zinazofanywa
na Mhimili huo ili waweze kujielimisha kwa mambo mbalimbali.
Katika
hatua nyingine, Msajili Mkuu ameahidi kushirikiana na Serikali katika kutatua
changamoto zitokanazo na mashauri ya jinai ikiwemo ucheleweshwaji wa upelelezi,
wananchi kuipa Mahakama ushirikiano katika utoaji wa ushahidi mahakamani ili
mashauri yaweze kukamilika ndani ya muda uliopangwa.
Akizungumza
na Mkuu wa wilaya ya Muleba Mhandisi Richard Henry Ruyango alipomtembelea
ofisini kwake, Msajili Mkuu alimuomba Mkuu wa wilaya kusaidia kuwaelimisha
wananchi ili kupunguza malalamiko yanayotoka na uelewa mdogo wa taratibu
mbalimbali za kimahakama.
Naye
Mkuu wa Wilaya hiyo ameihakikishia Mahakama ya Tanzania kuendelea kutoa
ushirikiano wa hali na mali kuhakikisha Mahakama inafikia malengo yake
iliyojipangia.
“Kupitia
Ofisi yangu nimefarijika kuona Mahakama imepiga hatua kubwa katika mambo mengi kama
kuimarisha huduma za utoaji haki nchini hasa uanzishwaji wa Vioski ya kusajili mashauri
kwa njia ya mtandao, na Mahakama inayotembea. “kwa hili niupongeze Uongozi wa
Mahakama”, aliongeza Mkuu wa Wilaya.
Msajili
Mkuu yupo kwenye ziara ya kikazi katika Kanda ya Bukoba kukagua shughuli
mbalimbali za kimahakama ili kujionea utendaji kazi wa watumishi katika
Mahakama za kanda hiyo.
Msajili
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akizungumza na watumishi
wa Mahakama ya Wilaya ya Biharamulo (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya
kikazi kukagua shughuli za Mahakama Kanda ya Bukoba, kulia ni Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba Mhe. Janeth Masesa na kushoto ni
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Biharamulo Mhe. Flora Ndale.
Msajili
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akiwa kwenye picha ya
pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Muleba, kulia ni Hakimu Mkazi
Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba Mhe. Janeth Masesa na kushoto ni
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Biharamulo Mhe. Asha Mwidudira.
Msajili
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akiwa kwenye picha ya pamoja
na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Biharamulo, kulia ni Hakimu Mkazi
Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba Mhe. Janeth Masesa na kushoto ni
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Biharamulo Mhe. Flora Ndale.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (kulia) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhandisi Richard Henry Ruyango machapisho ya Mahakama wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni