Na Innocent Kansha – Mahakama.
Mahakama
ya Tanzania imetafsiri Kanuni za
utaratibu wa kuendesha mashauri ya uchaguzi katika lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha
wadaawa wa mashauri hayo kuwa na uelewa wa kanuni hizo katika lugha rahisi pale
watakapotaka kuzitumia katika kutafuta haki zao.
Aidha, kanuni hizo zimetafsiriwa kupitia Tangazo la Serikali
No. 934 na 935 la tarehe 23 Oktoba mwaka 2020 kwa lengo la kuhakikisha haki
inawafikia watu wote na kuondoa vikwazo vya ucheleweshwaji wa
upatikanaji wa haki.
Akifungua Kikao cha Kamati ya Kitaifa cha kusukuma
mashauri ya jinai kilichofanyika jana Jijini Dar es salaam, Msajili Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma alisema, Kanuni hizo ni zile za mashauri ya Uchaguzi
Mkuu na za uchaguzi wa Serikali za Mitaa zote za Mwaka 2020.
Kwa
mujibu wa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhimili huo umefanya marekebisho na kuandaa kanuni, miongozo ya taratibu
mbalimbali kwa lengo la kuharakisha usikilizwaji wa Mashauri yanayohusu
uchaguzi.
Alisema
Mahakama ina mpango wa kuendelea
kutafsiri kanuni nyingine katika lugha ya Kiswahili kadri itavyowezekana. Baadhi
ya kanuni hizo ni zile za Mahakama ya Rufani kwa lengo la kurahisisha
taratibu katika Mahakama ya Rufani na Kanuni za makosa ya Rushwa na uhujumu
Uchumi (The Economic and Organized Crime Control (The Corruption and Economic
Crimes Division) (Procedure Rules, 2016.GN No. 267/2016), ili kuweka utaratibu mzuri wa kushughulikia watuhumiwa
wa makosa aina hiyo.
Mhe.
Chuma alizitaja kanuni nyingine zitakazotafsiriwa kuwa ni pamoja na Kanuni za Madalali
wa Mahakama na Wasambazaji Nyaraka na Kanuni za kuwasilisha nyaraka za Mahakama
kupitia mfumo wa kielectroniki.
“Pamoja
na mafanikio hayo nitumie hadhira hii kuwaomba wadau wa haki jinai kuunga mkono
juhudi hizi kwa kila mmoja kutekeleza wajibu wake ili kupunguza, kuziba na
kutokomeza kabisa mianya ya rushwa kwa kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano “TEHAMA” inayoonyesha ufanisi mkubwa,” alisisitiza Msajili Mkuu.
Mhe.Chuma
alisema Mahakama ya Tanzania inakusudia kuondokana na matumizi ya karatasi na
kuimarisha matumizi ya mifumo ya kielekitroniki maarufu kama “E. Filing Digitized and Access to Justice
Information Centre”, na kwamba imekiteua kituo cha Mahakama ya Wilaya Kigamboni kuanzisha usajili wa shauri,
usikilizwaji wake mpaka shauri linapomalizika kwa kutumia mfumo wa TEHAMA.
Huduma
hii ilizinduliwa tangu Novemba Mosi, 2020 na kuanza kutolewa katika Mahakama ya
Wilaya Kigamboni na itapelekwa kwenye Mahakama nyingine kwa kuwa dhamira ya
Mahakama ni kuondokana na mfumo wa kutumia karatasi na kuingia kwenye mfumo wa
kutumia mifumo ya TEHAMA katika shughuli zote za uendeshaji wa mashauri na
shuguli nyingine za Mahakama, aliongeza Msajili Mkuu.
Kwa
upande wa mashauri ya mlundikano Mhe. Chuma alieleza kuwa, takwimu
zinathibitisha kuwa pamoja na mashauri mengine, yapo Mashauri 39 ya dawa za
kulevya katika Mahakama Kuu ambayo ni ya mlundikano.
Alisema
taarifa ya mashauri ya kuanzia mwezi Januari hadi mwezi wa Oktoba, 2020 kwa
upande wa Mahakama za mikoa kuna jumla ya mashauri mlundikano 3,015 kati ya
hayo mashauri 1178 ni ya uhujumu uchumi na Mauaji ambayo Mahakama hizi hazina
mamlaka ya kuyasikiliza, aliongeza Mhe Chuma.
Msajili
Mkuu alieleza kuwa katika Mahakama za Wilaya kuna mashauri ya mlundikano 3,632 na
kati ya mashauri hayo, 1751 ni ya uhujumu uchumi na Mauaji ambayo pia Mahakama
hizi hazina mamlaka ya kuyasikiliza.
“Mashauri
hayo yapo katika hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutokamilika kwa
upelelezi, hivyo hatuna budi kushirikiana ili kuweka mikakati ya kuyaondosha”,
alisisitiza Msajili Mkuu.
Alitoa wito kwa wadau wa Mahakama kila moja kuwajibika ili kuepuka lawama ambazo mara nyingi huelekezwa mahakamani. Aliongeza kuwa wadau wana wajibu wa kuimarisha mfumo wa utoaji haki na kutatua changamoto zilizopo ili kuongeza Imani kwa wananchi.
Naye Naibu Kamishna wa jeshi la Polisi Bw. Salehe
Ambika akizungumza kwa niaba ya Mkurungenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai alisema
Polisi Kitengo cha Usalama barabarani kinakwenda kwa kasi katika kuratibu
shughuli zake kwa njia ya TEHAMA, kwani hivi sasa watuhumiwa wote wa makosa ya
usalama barabarani wanashunghulikiwa kesi zao kwa njia hiyo kabla hata ya
kufikishwa mahakamani.
Kwa upande wa makosa ya jinai yanayopokelewa vituoni,
Kamishna huyo alisema kwa sasa
yanashughulikiwa kwa njia ya mfumo wa TEHAMA unaofahamika kama “Case Management
System” maana yake ni kusaidia kufuatilia taarifa za jalada husika na kujua
hatua zilizochukuliwa ili kutoa taarifa sahihi za kiutendaji na kiukaguzi,
aliongeza Bw. Ambike.
Bw. Ambike ametoa rai kwa Taasisi zote
zinazojishughulisha na maswala ya mnyororo wa haki jinai kuwa mstari wa mbele
kutoa elimu kwa Umma juu ya masuala mbalimbali ya haki zao ili kuondoa taharuki
ili wadau wasibaki kutoa lawama kwa kutojua vizuri utendaji wa Taasisi husika,
hilo litasaidia kupunguza malalamiko ya kuonewa au kutotendewa haki hasa pale
wanapokinzana na sheria za nchi.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania
Mhe. Wilbert Chuma akizungumza wakati wa
uzinduzi mbele ya Wajumbe wa Kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Kusukuma Mashauri
ya Jinai (hawapo pichani) kilichofanyika katika ukumbi wa Kituo cha Mafunzo na
Habari cha Mahakama kilichopo Kisutu Jijini Dar es salaam, kushoto ni Msajili
wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Sharmillah Sarwatt ambaye ni Mwenyekiti wa
Kamati hiyo.
Baadhi ya Wajumbe wa Kikao cha Kamati
ya Kitaifa ya Kusukuma Mashauri ya Jinai wakifuatilia kwa makini wakati
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Usimamizi wa Mahauri Mhe. Desdery Kamugisha
alipokuwa akiwasilisha mada ya hali ya usikilzwaji wa mashauri mahakamani.
Baadhi Baadhi ya Wajumbe wa Kikao cha
Kamati ya Kitaifa ya Kusukuma Mashauri ya Jinai wakiwa kwenye kikao hicho
wakipiga makofi kuonesha kufurahishwa na hotuba ya ufunguzi iliyotolewa na Mgeni Rasmi
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma (aliyesimama
mbele).
Baadhi Baadhi ya Wajumbe wa Kikao cha
Kamati ya Kitaifa ya Kusukuma Mashauri ya Jinai wakiwa kwenye kikao hicho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni