Na Mary Gwera, Mahakama
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw.
Mathias Kabunduguru amewataka Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama
kutunza afya zao, kuzingatia maadili ya kazi pamoja na kujiepusha na vitendo vya
rushwa kwa ustawi wa chombo hicho muhimu kwa Mahakama na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza
wakati akifungua rasmi Mafunzo ya Elimu ya kujikinga na Ugonjwa wa UKIMWI na Magonjwa
yasiyoambukizwa, Bw. Kabunduguru ambaye pia ni Katibu wa Tume hiyo alisema kuwa
Watumishi wa umma ni hazina muhimu kwa Serikali hivyo ni vyema kutunza afya ili
kuwa na nguvu kazi kwa maendeleo ya nchi.
“Mkiwa
na nguvu na afya bora mtazalisha, mapato yataongezeka na hatimaye mapato hayo
yatawezesha kupatikana kwa huduma za jamii,” alieleza Bw. Kabunduguru.
Aliwasisitiza
Washiriki wa mafunzo hayo kujiepusha na maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI kwa
kuwa ugonjwa huo bado upo hali kadhalika kujikinga na magonjwa yasiyoambukizwa
kama Shinikizo la damu (BP), Kisukari na mengineyo kwa kufuata kanuni stahiki za
afya.
“Tunapaswa
kuendelea kuchukua tahadhari, UKIMWI bado upo, UKIMWI unatisha na vilevile
magonjwa yasiyoambukizwa yasipotibiwa yanaathiri nguvu kazi,” alisisitiza.
Kwa
upande mwingine, Mtendaji huyo aliwaasa Watumishi hao kuzingatia maadili ya
kazi kwa kujiepusha na vitendo vya rushwa.
“Rushwa
ni hatari kwa familia na kwa nchi, rushwa ina tabia ya kumpumbaza mtu,
inamfanya mtu kuwa mtumwa, hakuna mla rushwa aliyebaki salama, hivyo ni muhimu
kufanya kazi na kujipatia kipato cha halali,” alisema Bw. Kabunduguru.
Aliongeza
kuwa Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo nyeti kinachotambulika kikatiba
hivyo ni muhimu kuunga mkono sera za Mkuu wa nchi ikiwemo mapambano dhidi ya
rushwa.
Mafunzo
hayo ya siku mbili (2) yameanza leo Novemba 20 na kuhitimishwa Novemba 21 yanafanyika
katika Ofisi za Tume hiyo zilizopo jijini Dar es Salaam. Mafunzo haya yamelenga
kuwawezesha watumishi hao kupata elimu ya afya, Ujasiriamali, Maadili na Rushwa
pamoja na elimu ya Maandalizi ya kustaafu.
Katika
siku ya kwanza ya Mafunzo hayo, Washiriki walipata fursa ya kufanyiwa vipimo vya UKIMWI, Kisukari, Shinikizo la Damu
pamoja na Chanjo ya homa ya ini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni