Na Innocent Kansha – Mahakama.
Waziri
wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ameiomba Mahakama ya Tanzania
kuona uwezekano wa kubadilisha Sheria zile zinazotumika na kurejewa mahakamani
mara kwa mara zitafsiriwe kwa lugha ya Kiswahili ili kuwapa fursa wananchi
kupata uelewa mpana wa mambo ya kisheria pindi wanapoitafuta haki.
Akizungumza
na wajumbe wa kikao cha Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania wakati wa ziara
yake ya kikazi alipomtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania ofisini kwake Jijini Dar es
salaam jana Waziri Nchemba alisema hata maamuzi ya mashauri yanaweza
kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili kwa muhutasari tu ili kuwawezesha wadau
wengi zaidi kuelewa na kuondoa sintofahamu ya wananchi walio wengi.
“Hatumaanishi
kufuta lugha ya kiingereza lakini pia tusiwanyime wananchi walio wengi
kufurahia lugha yao wanayoitumia kama njia ya mawasiliano hasa kupitia Taasisi
muhimu na adhimu ya Mahakama ikiwa ndiyo chombo cha mwisho chenye kutoa maamuzi
kwa mujibu wa katiba yetu”, alisema Dkt. Nchemba.
Dkt.
Nchemba alishauri yatengenezwe mapendekezo na kuwasilishwa kwenye Mamlaka husika
kama Tume ya kurekebisha Sheria na kamati za kanuni na maboresho ya sheria za
Mahakama ili kuona uwezekano wa zile sheria zote zinazotumika kama rejea zitafsiriwa
kwa lugha ya Kiswahili.
Aidha,
Waziri Nchemba aliipongeza Mahakama kwa dira na dhima imara pia miongozo
thabiti iliyoleta mafanikio makubwa ya Taasisi, hasa Mpango Mkakati na
mafanikio yake makubwa yanayoonekana hivi sasa, “hatuna budi kuendelea kuunga
mkono juhudi hizi ili kutatua changamoto zinazoikabili Mahakama ifanye kazi kwa
ufanisi na kwa ukaribu mkubwa hasa kwa yale yote yaliyo ndani ya uwezo wetu
kama serikali”, alisisitiza.
Akizungumza
katika kikao hicho Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer
Mbuki Feleshi aliikumbusha Wizara kuendelea na ukamilishaji wa mchakato
ulioanza muda mrefu wa Sera ya Sheria “National Legal Policy” ili kuendana na
sera ya Mahakama ya mafunzo inayotumika kwa sasa.
“Mahakama
inaihitaji sana Wizara katika kutekeleza majukumu yake, ziara hii imetuachia
kitu cha kujivunia kama Mahakama na kuendelea kutekeleza majukumu yetu kwa
kujiamini kutokana na kujitoa kwako ulikoonesha kwetu”, aliongeza Jaji Kiongozi.
Aidha,
Jaji kiongozi ameithibitishia Wizara kwamba Mahakama haitarudi nyuma bali itaendelea
kushirikiana na wadau wake kwa ukaribu zaidi, huku akitolea mfano wa wa kipindi
cha ugonjwa wa COVID 19 ambapo Mahakama iliendelea kuchapa kazi kwa
kushirikiana na wadau wake kwa ufanisi mkubwa kwa kutumia mfumo wa Mahakama
mtandao “video Conference” na kwa kuzingatia kanuni za Wizara ya Afya.
Katika
hatua nyingine, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru
aliiomba Wizara kushirikiana kuhimiza Matumizi ya Kamati za Maadili ya Maofisa
wa Mahakama ambayo muongozo wake umeshatolewa kwa Wakuu wa Wilaya na Mikoa, kwa
kutafuta namna bora ya kuendesha Kamati hizo, badala ya kutumia majukwaa yao kuwafedhehesha
Maafisa hao kwa kuwa wao ni wenye viti wa kamati hizo.
“Tunapenda
watambue kuwa hilo ni jukumu lao kisheria na watoe ushirikiano ili kuondoa
sintofahamu inapotokea hali ya malalamiko”, alisema.
Bw.
Kabunduguru alitoa rai kwa Wizara kuona uwezekana wa kuongeza bajeti kwa Tume
ya Utumishi wa Mahakama kwani Tume hiyo ni kiungo muhimu katika masuala ya
kumshauri Rais namna bora ya kuendesha shughuli za Mahakama.
Naye,
Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama, Mhe. Zahra Maruma akitoa Taarifa ya
utekelezaji wa maboresho ya Mahakama alianisha mafanikio mbalimbali
yaliyotokana na Mpango Mkakati wa Mahakama wa mwaka 2015/16 hadi 2019/20,
ikiwemo kiwango cha wananchi kukubali huduma zitolewazo na Mahakama kupanda na
kufikia asilimia 78 kwa mwaka 2019, hii inatokana na huduma za Mahakama
kuboreka na ushirikishwaji wa wadau.
Maeneo
mengine ya mafanikio ni pamoja na miradi mikubwa ya ujenzi na ukarabati wa
miundombinu ya majengo ya Mahakama iliyokamilika na inayoendelea nchi nzima katika
ngazi zote kuanzia Mahakama Kuu, Hakimu Mkazi, Wilaya na za mwanzo.
Mhe.
Maruma alisema uanzishaji na uboreshaji wa mifumo ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) iliyorahisisha utoaji wa haki ilienda sambamba na uanzishwaji
wa matumizi ya Mahakama inayotembea kwa mikoa ya Dar es salaam na Mwanza.
Wakati
huo huo, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri, Mhe. Desdery Kamugisha akitoa
taarifa ya hali ya usikilizwaji wa mashauri, alisema Mahakama imefanya kazi
kubwa ya kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia Mpango Mkakati wake wa miaka
mitano na Dira ya maendeleo ya Taifa ya 2025.
Mahakama
imeendelea kupiga hatua katika kusikiliza na kumaliza mashauri kwa wakati, hii
inathibitishwa na taarifa kwamba kuanzia Januari 2020 hadi Novemba 2020,
Mahakama katika ngazi zote imefanikiwa kusikiliza mashauri 220,872 kati ya
mashauri 219, 527 yaliyofunguliwa na yale yaliyobaki mwezi Desemba 2019 ambayo
ni sawa na asilimia 101.
Mhe.
Kamugisha alisema jumla ya mashauri ya Jinai 2,499 yanaendelea kutajwa katika
Mahakama za Hakimu Mkazi. Kati ya mashauri hayo kuna mashauri 788 ya jinai
kawaida, mashauri 818 ya mauaji, mashauri 865 ya rushwa na uhujumu uchumi na
mashauri 28 ya makossa ya usalama barabarani.
Jumla
ya mashauri ya Jinai 4,469 yanaendelea kutajwa katika Mahakama za Wilaya
nchini. Kati ya mashauri hayo mashauri 1,232 ni ya jinai kawaida, mashauri
1,754 ya mauaji, mashauri 1,422 ya rushwa na uhujumu uchumi na mashauri 61 ya
makossa ya usalama barabarani, aliongeza Mhe. Kamugisha.
Waziri
wa Katiba na Sheria Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (katikati) akizungumza na
Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania (hawapo pichani) alipofanya ziara yake ya
kikazi kumtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania, Kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, Naibu Waziri
wa Katiba na Sheria Geofrey Mizengo Pinda (kushoto).
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa pili kushoto) akiwa kwenye
picha ya pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (wa
pili kulia) alipomtembelea ofisini, kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe.Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi na kushoto ni Naibu Waziri wa Katiba
na Sheria Geofrey Mizengo Pinda.
Waziri
wa Katiba na Sheria, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akisaini Kitabu cha wageni
mara baada ya kuwasili ofisini kwa Jaji Mkuu wa Tanzania Jijini Dar es salaam
kwa ziara ya kikazi, Desemba 23,2020 kulia ni Naibu Waziri wa Katibu na
Sheria Geofrey Mizengo Pinda.
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (kushoto)
akimkabidhi Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (kushoto) Miongozo
mbalimbali iliyoandaliwa na Mahakama kusaidia kurahisisha utoaji haki.
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akiwa
kwenye picha ya pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Mwigulu Lameck
Nchemba (wa pili kushoto), Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias
Kabunduguru (wa pili kulia), Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Geofrey Mizengo
Pinda (wa kwanza kushoto) na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert
Chuma (wa kwanza kulia) pamoja na Viongozi waandamizi wa Wizara naMahakama ya
Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni