Na Festo Sanga, Mahakama Kuu-Kigoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Kigoma, Mhe. Jaji Ilvin Mugeta amefungua rasmi awamu ya pili ya mafunzo ya Wasaidizi wa Kumbukumbu juu ya mifumo ya TEHAMA huku akiwasisitiza Watumishi hao kama watendaji muhimu wa masjala kuwa wana mchango mkubwa katika kuleta tija ya utendaji kazi kupitia mifumo mbalimbali ya Mahakama.
Akifungua mafunzo hayo mwishoni mwa wiki iliyopita, Mhe. Jaji Mugeta alisema kuwa upimaji wa utendaji kazi utazingatia eneo la matumizi ya TEHAMA na kusisitiza kila mmoja kutimiza wajibu wake.
“Matumizi ya TEHAMA yamelenga kurahisisha shughuli za utoaji haki, kuongeza uwazi, ubora wa taarifa na Takwimu na kuwapunguzia gharama wadaawa” alisema Jaji Mugeta.
Mhe. Jaji Mugeta aliongeza kuwa Mahakama imewekeza katika mifumo mbalimbali inayorahisisha upatikanaji wa haki na baadhi ya mifumo hiyo ni pamoja na wa Kusikiliza mashauri kwa njia ya Video (video conferencing), Mfumo wa kuwatambua mawakili (TAMS), Mfumo wa kusajili mashauri (JSDS II) na mfumo wa mawasiliano kwa barua pepe (Judicial mailing system).
Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Kigoma Mhe. Arnold Kirekiano alipongeza juhudi ambazo wasaidizi wa kumbukumbu wamefanya katika kuhuisha taarifa za mashauri na kusema mafunzo hayo yatawawezesha kufanya vizuri zaidi na kuhakikisha Kanda hiyo inakuwa ya mfano kwa usahihi wa taarifa na takwimu za mashauri.
Mafunzo hayo ya awamu ya pili katika utekelezaji wa Mpango wa ndani wa mafunzo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 yaliwezeshwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Kirekiano, Mtendaji wa Mahakama Kuu- Kigoma, Bw. Moses Mashaka na Afisa TEHAMA, Bw. Prosper Bonaventura Mahalala.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Kigoma, Mhe. Jaji Ilvin Mugeta akitoa neno alipokuwa akifungua rasmi mafunzo ya Wasaidizi wa Kumbukumbu juu ya matumizi ya mifumo ya TEHAMA kwa washiriki waliohudhuria mnamo Desemba 4, 2020. Kushoto ni Mhe. Arnold Kirekiano, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, na kulia ni Bw. Moses Mashaka, Mtendaji wa Mahakama Kuu- Kigoma.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Arnold Kirekiano akitoa mada juu miongozo kuhusu utoaji Huduma za Kimahakama kwa njia ya Mtandao.
Mhe. Jaji Ilvin Mugeta (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo. Kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kigoma Mhe. Arnold Kirekiano na Kulia kwake ni Mtendaji wa Mahakama Bw. Moses Mashaka.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni