Jumatatu, 21 Desemba 2020

WAWAKILISHENI VYEMA WANANCHI MAHAKAMANI: JAJI MKUU

 Na Mary Gwera, Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.  Ibrahim Hamis Juma amewaasa Mawakili wapya wa Kujitegemea kuwawakilisha vyema wananchi wanaosimamia kesi zao Mahakamani kwa kufuata sheria na kanuni stahiki za uwakili na kuziishi kanuni za kimaadili, nidhamu na tabia njema za Mawakili.

Akitoa hotuba yake mara baada ya kuwakubali na kuwapokea Mawakili hao mapema leo Desemba 21, 2020 katika Viwanja vya Karimjee-Dar es-Salaam, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa kuna baadhi ya Mawakili wamekuwa si waaminifu.

“Sote tunafahamu kuwa katika kazi zenu za uwakili mtawajibika kwa wateja wenu watakaowapa ajira. Lakini kumbukeni kuwa wajibu mnaotakiwa kuupa uzito wa juu zaidi ni wajibu wenu kwa Katiba, kwa Sheria za Nchi na kwa Mahakama mkiwa maafisa wa Mahakama,” alisema Mhe. Jaji Prof. Juma.

Aidha, Mhe. Jaji Mkuu aliongeza kwa kuwasisitiza Mawakili hao kuwa ni wajibu wao kuhakikisha kuwa hawawaingizi wateja wao/wananchi katika uvunjifu wa Sheria pamoja na kanuni za kimaadili, nidhamu na tabia njema za mawakili (the advocates (professional conduct and ettiquette) regulations, 2018 gn no. 118 of 2018) ambazo tayari zinatumika kuwaongoza katika kazi za uwakili.

“Bado ipo mifano inayoashiria kuwa wapo Mawakili wachache ambao bado hawaziishi kanuni tajwa za Mawakili, kila siku katika mitandao ya kijamii, hasa ya TWITTER, tumeona Mawakili wakitumia lugha zisizofaa (wengine wazi wazi, wengine kwa majina ya kubuni). Wapo Mawakili ambao wamejipambanua kwa kupotosha tafsiri ya maamuzi ya Mahakama na kuivuta Mahakama katika malumbano ya kisiasa,” alieleza Mhe. Jaji Mkuu.

Kwa upande wake, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa aliwataka Mawakili hao kuwa sehemu kubwa ya kuisaidia Mahakama kufikia maamuzi ya haki.

Niwakumbushe tu kwamba sasa mtakuwa maafisa wa Mahakama chini ya Sheria ya Mawakili, Sura ya 341. Hivyo mtakuwa na wajibu kwa Mahakama na kuhakikisha mnaisaidia Mahakama kufikia kwenye maamuzi ya haki na yanayotolewa kwa wakati,” alisema Dkt. Longopa.

Naye Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Dkt. Rugemeleza Nshala aliwataka Mawakili hapo kujiweka sawa katika matumizi ya lugha, Kiswahili na Kiingereza fasaha kwani lugha ni jambo muhimu katika kazi ya uwakili.

Aidha, katika sherehe hizo Mhe. Jaji Mkuu alimkaribisha Balozi Mstaafu Ami Mpungwe ambapo aliwakumbusha Mawakili hao kufanya kazi kuendana na kasi ya teknolojia iliyopo duniani.

“Dunia inakwenda kasi kulingana na mabadiliko ya teknolojia, Kampuni nyingi kwa sasa zinafanywa na mifumo, hivyo ni muhimu kuwa wabunifu katika suala hili kwa teknolojia inaweza kukuweka kanda,” alisema Balozi Mpungwe.

Katika sherehe hizo, Mhe. Jaji Mkuu amewakubali na kuwapokea jumla ya Mawakili wapya wa kujitegemea 166 na kufanya jumla ya idadi yao kuwa 10,128 kwa nchi nzima.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa hotuba wakati wa Mahafali ya 63 ya kuwapokea na kuwakubali Mawakili wapya (hawapo pichani), yaliyofanyika katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam, leo Desemba 21, 2020.

Baadhi ya Mawakili wapya wakitoa heshima kwa Mhe. Jaji Mkuu na meza kuu wakati wa tukio la kuwapokea na kuwakubali mawakili wapya.


 Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (anayesoma karatasi) akiwapokea na kuwakubali mawakili wapya. Waliosimama nae meza kuu ni baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Jaji Kiongozi na baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Baadhi ya Wananchi waliohudhuria katika Mahafali ya 63 ya kuwapokea na kuwakubali Mawakili wapya katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam.

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa akitoa nasaha zake katika hafla hiyo.  

Mhe. Jaji Mkuu na baadhi ya Majaji wakiwa katika picha ya pamoja na Mawakili wapya.


 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni