Jumanne, 16 Februari 2021

KASI YA UJENZI WA VITUO JUMUISHI YAMKOSHA WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA

Na Innocent Kansha, Mahakama.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ameupongeza Uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa ubunifu mkubwa na matumizi mazuri ya rasilimali fedha katika ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Mahakama vya utoaji haki.

Akizungumza mapema Februari 15, 2021 katika ziara yake ya ukaguzi wa miradi hiyo inayotekelezwa na Mahakama ya Tanzania katika Vituo vya Temeke na Kinondoni Jijini Dar es Salaam, Waziri Nchemba alisema vituo hivi vinavyojengwa katika maeneo  sita nchini vitakuwa vya manufaa makubwa sana kwa wananchi katika kusogeza huduma karibu za utoaji haki.

“Utakubaliana nami kwamba wananchi, taasisi za umma, makampuni binafsi, hata makundi mbalimbali wana imani kubwa sana na Mahakama kwani ni kiungo muhimu sana cha kulinda amani, usalama, utulivu na kukuza uchumi wa Taifa kwa ujumla”, alisema Dkt. Nchemba.

Dkt. Mwigulu aliongeza kuwa Mahakama imeonyesha ubunifu mkubwa sana, huku akisema kuwa ingeweza kuwa na rasilimali fedha lakini ikafanya kitu ambacho kisingekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi lakini imefanya upembuzi makini na imeweza kujenga miradi hiyo ambayo itaisaidia jamii yetu, kwa kuweka huduma za utoaji haki za ngazi mbalimbali katika jengo moja ni msaada mkubwa kwa mwananchi wa kawaida utakaomuwezesha kutumia muda mchache na kupunguza gharama aliongeza katika kutafuta huduma ya haki.

Aidha, Dkt. Mwigulu aliongeza kuwa ameona na kuridhishwa na jinsi ambavyo majengo hayo yanavyojengwa kwa ustadi kuanzia usalama wa jengo, wa watoa huduma ya haki ikiwa ni pamoja na kuzingtia usalama wa wadau wote muhimu.

“Kama nchi ni lazima tutambue kwamba akitoka Mungu kwenye masuala ya utoaji haki, kingine ni chombo hiki cha Mahakama pekee chenye dhamana hiyo, kama serikali ni lazima kukipa ushirikiano wa karibu katika kutimiza majukumu yake,” alieleza.

Kwa upande mwingine, Waziri Nchemba alitumia ziara hiyo kuwaasa wananchi wasiinyooshee kidole Mahakama, bali kama jamii ni lazima itambue ina wajibu wa kulinda maadili, utu, udugu, usawa na kutojielekeza kwenye uhalifu kwakuwa si jambo jema kwa jamii ya wastarabu, ni matamanio ya wote kuwa na jamii inayotenda haki na kutii sheria ili kuwapunguzia mzigo mzito watoa haki.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru alisema dhana  ya Mahakama jumuishi kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, Tanzania ni nchi ya kwanza kutekeleza mradi wa aina hii wa ujenzi wa vituo vinavyounganisha Mahakama ya Mwanzo, Wilaya, Hakimu Mkazi na Mahakama Kuu kwenye jengo moja pamoja na wadau wote muhimu wanaoshirikiana na Mahakama.

“Lengo la mradi huu wa kisasa utakaotumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika usikilizaji wa mashauri na migogoro ya wananchi ni kutafuta namna bora ya kumpunguzia mwananchi gharama za upatikanaji wa haki kwa wakati,” alisema Mtendaji Mkuu.

Akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa miradi hiyo, Mwandisi-Ujenzi, Mahakama ya Tanzania, Mwandisi. Khamadu Kitunzi alisema miradi yote sita hadi kukamilika kwake itagharimu jumla ya Tshs. 42,420,601,790 ikihusisha majengo ya Mahakama, mifumo ya umeme na viyoyozi, mifumo ya Tehama, genereta, Transfoma na kazi za kuboresha mazingira pamoja na maegesho ya magari.

Mradi wa ujenzi wa vituo jumuishi sita vya utoaji haki unatarajia kukamilika ifikapo mwezi mei, 2021.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (kushoto) akifafanua jambo wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa vituo jumuishi vya utoaji haki vilivyopo Temeke na Kinondoni Jijini Dar es salaam, (wa pili kulia) ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru na katikati ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru (wa pili kushoto) akifafanua jambo mbele ya Waziri Mwigulu Lameck Nchemba (mwenye alipokuwa kwenye ziara ya ukaguzi wa Vituo Jumuishi vya Kinondoni na Temeke. Kushoto ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,Mhe. Wilbert Chuma (aliyenyoosha mkiono) akitoa maelezo mbele ya Waziri na Mtendaji Mkuu wa Mahakama wakati wa ukaguzi huo, wengine ni viongozi waandamizi wa Mahakama na wakandarasi wa mradi.

Mkuu wa kitengo cha usimamizi wa majengo Mwandisi Khamadu Kitunzi (katikati) akitoa maelezo ya jinsi miradi inavyojengwa kwa Waziri wa Katiba na sheria Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba na Mtendaji Mkuu wa Mahakama Bw. Mathias Kabunduguru akiwepo na viongozi wandamizi wa Mahakama.


Mkuu wa kitengo cha usimamizi wa majengo Mwandisi Khamadu Kitunzi (katikati) akitoa maelezo ya jinsi miradi inavyojengwa kwa Waziri wa Katiba na sheria Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba na Mtendaji Mkuu wa Mahakama Bw. Mathias Kabunduguru akiwepo na viongozi wandamizi wa Mahakama.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (katikati ) akijadiliana jambo na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma (kushoto) pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru (kulia) mara baada ya zoezi la ukaguzi wa miradi hiyo.

Picha na Innocent kansha, Mahakama.

 

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni