Na Lydia Churi- Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
ametoa wito kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo kuwaelimisha
wananchi sheria na taratibu za kimahakama ili
kuongeza uelewa wa masuala ya sheria kwa watanzania.
Akizungumza mara baada ya kuwaapisha Mahakimu wakazi 70
leo jijini Dar es salaam, Jaji Mkuu amewataka Mahakimu hao kuwasaidia wananchi kuelewa
taratibu zote zinazohusu mashauri
yaliyo mahakamani.
“Tusiwaachie wadaawa
waondoke mahakamani
bila kujua hatua mbalimbali ambazo shauri litapitia hadi kukamilika” alisema Jaji Mkuu.
Alisema katika
nchi yenye changamoto ya wananchi wengi kutofahamu sheria na taratibu za
kimahakama kama ilivyo kwa
Tanzania; Mahakimu na Majaji wanao wajibu mkubwa wa
kuelimisha Umma.
Kuhusu masuala ya maadili, Jaji Mkuu amewataka Mahakimu
hao kufanya kazi kwa uadilifu kwa kuwa wao ni nguzo muhimu ya utawala wa sheria
na wamepewa
mamlaka ya mwisho kwa mujibu wa Ibara ya 107A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika
utoaji haki.
Alisema kiapo walichoapa Mahakimu hao kinawakumbusha
Ibara ya 107B ya katiba ambayo imetambua
Uhuru wa Mahakimu katika kutoa
haki bila ya kuingiliwa na mamlaka nyingine.
Aidha amewashauri Mahakimu walioapishwa kuhakikisha
wanasoma na kuzielewa Sheria zote zinaosimamia
uendeshaji wa mashauri ya
Mahakama za Mwanzo ikiwa
ni pamoja na kujua pale Sheria inapofanyiwa
marekebisho.
Amesema ili wawe Mahakimu bora na wa kutegemewa wanapaswa
kufanya utafiti wa kutosha kabla ya kuandika hukumu au kutoa maamuzi ya mashauri watakayosikiliza. “Someni
pia maamuzi
ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani yaliyowekwa kwenye mfumo wa kuhifadhi mashauri (TANZLII).
Katika kuhakikisha mashauri hayakai kwa muda mrefu
mahakamani, Jaji Mkuu amewataka Mahakimu hao kutoa hukumu kwa wakati.
Alifafanua kuwa katika Mahakama
za Mwanzo
mashauri yanapaswa kumalizika ndani ya miezi sita na endapo litabaki mahakamani kwa zaidi ya muda huo, itakuwa ni mlundikano
wa mashauri.
Wakati huo huo, Prof. Juma amewataka Mahakimu kutoruhusu
Mawakili kuchelewesha mashauri kwani kwa kufanya hivyo husababisha kuwepo kwa mlundikano
wa mashauri katika Mahakama za Mwanzo. Aliwataka pia Mawakili wasitumike
kuzuia usuluhishi kwa kuwa usuluhishi
ni takwa
la katiba.
Kuhusu rushwa na maadili, Mahakimu hao wametakiwa kujiepusha na vitendo hivyo pamoja na mazingira
yeyote yanayoweza kupelekea wananchi kukosa imani na Muhimili wa Mahakama.
Jumla ya Mahakimu wakazi 70 waliapishwa leo na kufanya
idadi ya Mahakimu walioapishwa ndani ya wiki moja kufikia 140.
Baadhi ya Mahakimu Wakazi wakila kiapo mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo pichani) leo katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam. Jumla ya Mahakimu 70 waliapishwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni