· Viongozi wa Serikali wakumbushwa kutekeleza agizo la Rais la kutokalia taarifa
Na Lydia
Churi- Mahakama, Morogoro
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.
Innocent Bashungwa ameipongeza Mahakama ya Tanzania kutokana na maboresho
mbalimbali iliyofanya na inayoendelea kufanya katika huduma zake.
Waziri Bashungwa ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza
na Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Taasisi mbalimbali za Serikali alipokuwa
akifungua Mkutano wa mwaka wa waandaaji wa vipindi vya Redio na Televisheni ulioandaliwa
na Shirika la Utangazaji Tanzania TBC mjini Morogoro.
“Mahakama ya Tanzania inafanya kazi nzuri sana ya
kuboresha huduma zake na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora”, alisema
Waziri Bashungwa.
Alisema hivi sasa wananchi wanashuhudia huduma
zikisogezwa karibu zaidi ambapo majengo ya Mahakama yamekuwa yakiendelea
kujengwa katika maeneo mblimbli nchini hatua inayomfanya kuupongeza Mhimili huo
kwa maboresho hayo.
Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo pia amelipongeza
shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa kuwakutanisha Maafisa Habari, Mawasiliano
na Uhusiano wa Taasisi za Serikali ikiwemo Mahakama ya Tanzania ili kupata
mafunzo yatakayosaidia kuboresha namna ya utangazaji wa shughuli za serikali.
“Serikali inawathamini Maafisa Mawasiliano kwa kuwa ni
daraja muhimu sana kati yake na wananchi, hivyo tumieni elimu na weledi wenu kufikisha
ajenda muhimu za serikali kwa wananchi ukiwemo Mpango wa Taifa wa maendeleo wa
miaka mitano ili wananchi waufahamu vizuri”, alisema.
Naye Katibu Mkuu wa wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbas amewakumbusha
viongozi wa Serikali kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliyoyatoa Juni 4 mwaka jana ambapo aliwataka viongozi
hao kuhakikisha shughuli za Serikali zinatangazwa.
Akitoa mada kwenye Mkutano wa waandaaji wa vipindi vya
Redio na Televisheni, Dkt. Abbas Serikali katika kipindi cha pili cha serikali
ya awamu ya tano, itafanya tathmini ya utoaji wa taarifa za serikali kwa
Viongozi wa Taasisi pamoja na Maafisa Mawasiliano kwani wako watendaji wakuu wa
Taasisis ambao ni kikwazo katika utoaji wa taarifa zinazohusu utekelezaji wa
shughuli za serikali.
Aidha, Katibu Mkuu huyo na Msemaji wa Serikali amezitaka
Taasisi za Serikali kutoa taarifa sahihi na kwa wakati ili wananchi wafahamu
shughuli mbalimbali pamoja na mafanikio ya Serikali yao.
Alisema hivi sasa hali ya utoaji wa taarifa za
serikali ni nzuri hivyo amewataka Maafisa Mawasiliano wa Serikali kuongeza
juhudi, vifaa na kuwa wabunifu ili waweze
kuandaa na kutoa habari zilizofanyiwa utafiti wa kutosha, zenye takwimu na zinazoonesha Ushahidi wa maendeleo
yaliyofikiwa.
Mkutano wa 104 wa waandaaji wa vipindi vya Redio na
Televisheni ulioandaliwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) unahudhuriwa na
Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Zaidi ya 80 kutoka Taasisi mbalimbali
za Serikali mjini Morogoro. TBC ilianza
kuandaa mikutano ya aina hii tangu miaka ya 1980’s.
Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano kutoka Taasisi za Serikali wakiwa kwenye Mkutano wa Mwaka wa waandaji wa vipindi vya Redio na Televisheni ulioandaliwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) mjini Morogoro. Mkutano huo ulifunguliwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa leo.
Katibu Mkuu wa wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbas
akitoa mada kwenye Mkutano huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni