Jumanne, 9 Februari 2021

JAJI IMANI ABOUD ASHINDA KWA KISHINDO UCHAGUZI WA MAJAJI WA MAHAKAMA YA AFRIKA

·       Ashinda kwa kura 51 kati ya 52 zilizopigwa
Mhe. Jaji Imani Aboud.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Divisheni ya Kazi, Mhe. Jaji Imani Aboud (pichani) ameshinda kwa kishindo katika uchaguzi wa Majaji wanne (4) wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na kumuwezesha kupata nafasi nyingine ya kuwa miongoni mwa Majaji wa Mahakama hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Februari 07, 2021 na Mkurugenzi wa Mawasiliano, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Emmanuel Buhohela anasema kuwa Jaji Aboud alichaguliwa kwa kura 51 kati ya 52.

“Mgombea wa Tanzania, Mhe. Jaji Imani D. Aboud alichaguliwa kwa muhula wa pili kwa kura 51 kati ya 52 zilizopigwa,” alieleza Bw. Buhohela kupitia taarifa hiyo.

Kwa ushindi huo, Mhe. Jaji Aboud atakuwa Jaji wa Mahakama hiyo akiiwakilisha Kanda ya Afrika Mashariki kwa muhula wa miaka sita (6).

Uchaguzi huo umefanyika katika Mkutano wa 38 wa Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika kwa njia ya mtandao Februari 04 mwaka huu.

Aidha, taarifa hiyo inaweka bayana kuwa ushindi wa Mhe. Jaji Aboud unadhihirisha uwezo mkubwa walio nao Watanzania pamoja na Mhe. Jaji Aboud na heshima kubwa iliyonayo Tanzania katika Bara la Afrika.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni