Na Lydia
Churi-Mahakama
Mahakama ya Tanzania inatarajia kuanzisha kituo Maalum
kitakachoshughulikia mashauri yanayohusu mirathi na masuala ya kifamilia (ndoa
na talaka) kwa lengo la kusogeza na
kurahisisha utoaji wa huduma za kimahakama kwa wananchi.
Akiwasilisha mada mbele ya wajumbe wa Kamati ya kudumu
ya bunge ya katiba na Sheria, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe.
Messeka Chaba aliwaambia wajumbe hao kuwa kituo hicho kinajengwa wilayani
Temeke jijini Dar es salaam na ujenzi wa jengo hilo uko katika hatua za
ukamilishwaji.
Kwa mujibu wa Mhe. Chaba, Mahakama imeamua kuanzisha
kituo hicho maalum (One Stop Centre) kufuatia kuwepo kwa idadi kubwa ya
mashauri yanayohusiana na masuala ya Mirathi, Ndoa na Talaka. Utafiti
uliofanywa na Mahakama katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 ulionesha kuwa kulikuwa
na jumla ya mashauri 5072 yanayohusu
masuala hayo ambapo mashauri ya mirathi pekee yalikuwa ni 3474 na familia 1598 katika
Mkoa wa Da es Salaam.
Alisema
huduma hiyo itaanza mara baada ya taratibu za kisheria kukamilika na kutangazwa
rasmi na mamlaka husika. Aidha, mchakato wa kuandaa kanuni (Rules) ikiwa ni
pamoja na kanuni za uendeshaji wa kituo hicho (The One Stop Centre
Operationalization Rules, 2021) sambamba na Mwongozo wa utendaji kazi
(Operational Manual for One Stop Centre) tayari zimeandaliwa na zinafanyiwa
kazi.
Mhe. Chaba alizitaja faida za kuanzishwa kwa kituo hicho kuwa ni kupatikana kwa huduma ya kusikiliza na kutoa uamuzi katika mashauri ya mirathi, ndoa na talaka na usimamizi wa mali za marehemu ndani ya siku saba (7) na kusaidia kuwaleta pamoja wadau wa haki ndani ya jengo moja wakiwemo ofisi ya Mwanansheria mKuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Mawakili wa kujitegemea, watoa msaada wa kisheria, watendaji wa madhehebu ya dini na ustawi wa jamii.
Alisema Mahakama za Mwanzo na Wilaya zitakuwa na mamlaka ya kusikiliza mashauri ya mirathi, ndoa na talaka katika kituo hiki katika mkoa mzima wa Dar es salaam. Aliongeza kuwa hatua hii itachochea kuifikia haki kwa haraka na wakati.
Faida nyingine zitakazotokana na kuanzishwa kwa kituo hiki ni kuokoa muda
na kupunguza gharama za uendeshaji wa
mashauri kwa wadaawa, pamoja gharama za kutafuta Mawakili na watoa msaada wa kisheria.
Kuanzishwa kwa kituo hicho pia kutapunguza ucheleweshaji wa kumalizika kwa
mashauri ya ndoa, talaka, mirathi na usimamizi wa mali za marehemu na kutoa
hamasa na kupanua wigo wa matumizi ya rasilimali katika uendeshaji wa mashauri
ya aina hii.
Mahakama ya Tanzania kupitia Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (2015/16 - 2019/20) unaokwenda sambamba na Dira ya Taifa
ya Maendeleo (2025) iliweka malengo ya kujenga majengo ya Mahakama ambayo
yatatumika kama Vituo Jumuishi vya Utoaji haki (Intergrated Justice Centre) kwa
lengo la kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi na kurahisisha utoaji haki. Katika
kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati,
Mahakama iliona umuhimu wa kuanzisha kituo kimoja Jumuishi cha Utoaji Haki (One
Stop Centre) kitakachoshughulikia mashauri ya mirathi na familia.
Kituo
kimoja Jumuishi cha Utoaji Haki ni jengo maalum lililobuniwa na kujengwa kwa
ajili ya kutoa huduma zote za usikilizwaji wa mashauri ya familia, mirathi, ndoa
na usimamizi wa mali za marehemu. Kituo hiki kitajumuisha ngazi za Mahakama ya
Mwanzo, Wilaya, Hakimu Mkazi na Mahakama Kuu pamoja na ofisi za wadau wote
muhimu wanaoshughulika na mashauri ya aina hii kukaa ndani ya jengo moja ili
kutekeleza majukumu yao ya utoaji haki.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akisikiliza hoja za wajumbe wa Kamati ya kudumu ya bunge ya katiba na Sheria walipokutana na ujumbe wa Mahakama ya Tanzania. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru na kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Najma Murtaza Giga.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni