- Atoa rai kwa Waandishi wa habari kutoa habari sahihi za Mahakama kwa umma
Na Mary Gwera, Mahakama
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma ametoa rai kwa waandishi wa habari nchini kutekeleza majukumu yao kwa kufuata misingi na taratibu za kazi hiyo ili kutopotosha umma katika taarifa mbalimbali zinazohusu Mhimili wa Mahakama kwa kupata taarifa sahihi kutoka vyanzo vya Mahakama.
Machi 9-15, 2021, moja ya Magazeti ya wiki lilitoa habari yenye kichwa cha habari ‘Mahabusu waozea ndani’ likielekeza tuhuma kwa Mahakama juu ya ucheleweshaji wa kesi mbalimbali na masuala mengineyo ya kisheria.
“Niwashukuru wanahabari kwa kazi nzuri mnayofanya ya kuuhabarisha umma kuhusu taarifa mbalimbali zinazohusu Mahakama. Hata hivyo ni rai yangu kuwa ni vyema kabla ya kutoa habari kwa umma mnatakiwa kufuata taratibu na kanuni za taaluma ya uandishi wa habari ili kujiridhisha taarifa zinazotolewa ni sahihi na hivyo kuwa na manufaa kwa umma,” alisema Mhe. Chuma.
Katika Mkutano wake na Waandishi wa Habari mapema Machi 17, 2021 katika ukumbi wa Mikutano Mahakama Kuu-Dar es Salaam, Mhe. Chuma alisema kuwa Mahakama inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia elekezo la kikatiba linaloilazimu Mahakama kuzingatia takwa la kutochelewesha haki bila sababu za msingi.
Msajili Mkuu alieleza kuwa Mahakama imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa mashauri yanasikilizwa kwa wakati huku akitoa takwimu kwa mujibu wa ripoti ya utendaji kazi wa Mahakama kwa mwaka 2020 kuwa kati ya Januari hadi Desemba, ya mwaka huo jumla ya mashauri 238,786 yalisajiliwa na kusikilizwa mashauri 243,464 sawa na asilimia 102 ya mashauri yaliyofunguliwa.
Aidha, kwa upande wa mashauri ya madai, Mhe. Chuma alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano (5) iliyopita Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara ilisikiliza mashauri yenye thamani ya Trilioni 4 na bilioni 1 sawa na asilimia 3 ya pato la taifa kwa mwaka.
“Kwa muktadha huo, ni dhahiri ya kuwa ndani ya Mahakama hakuna Sera ya kuchelewesha kesi bila sababu, vilevile hakuna Jaji au Hakimu anayependa kuchelewesha shauri ama kumuweka mtuhumiwa/mshitakiwa mahabusu muda mrefu bila sababu za msingi,” alisisitiza Mhe. Chuma.
Katika kuhakikisha kuwa Mahakama inatekeleza ipasavyo takwa la kikatiba, imejiwekea mikakati mbalimbali yenye lengo la kuhakikisha kuwa mashauri yanasikilizwa na kumalizwa kwa wakati ikiwa ni pamoja na kupanga muda maalum na idadi ya kesi kwa kila ngazi ya Mahakama na kwa kila Jaji au Hakimu.
“Mahakama imejiwekea sera ya kuhakikisha kuwa mashauri yanamalizwa kwa wakati, kwa mfano Mahakama za Mwanzo ziliwekewa malengo ya kumaliza mashauri ndani ya miezi sita (6) tangu kufunguliwa kwake, Mahakama za Wilaya na za Hakimu Mkazi mashauri yanatakiwa kusikilizwa na kumalizika ndani ya mwaka mmoja (1) huku Mahakama Kuu ikiwekewa muda wa miaka miwili (2) kesi kukamilika,” alieleza.
Jitihada nyinginezo za kuhakikisha kuwa mashauri yanamalizwa kwa wakati ni kuweka kipaumbele katika matumizi ya TEHAMA ikiwemo kuendesha kesi kwa njia ya mtandao ‘video conference’.
“Mtakubaliana nami kwamba hata wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya corona, pamoja na changamoto hiyo Mahakama iliendelea kutoa huduma,” alisema.
Kwa upande mwingine, Msajili huyo aliongeza kuwa katika kutoa huduma ya haki jinai Mahakama hushirikiana na wadau wengine wa mfumo wa haki tangu kusajiliwa kwa shauri hadi kufikia mwisho, hivyo ushirikiano zaidi ni muhimu ili kuhakikisha kila mmoja anatekeleza jukumu lake ili kutokuwa na ucheleweshaji wa kesi.
Miongoni mwa sababu mbalimbali zinazosababisha baadhi ya mashauri kutomalizika kwa wakati ni pamoja na upelelezi kutokamilika kwa wakati, kutopatikana kwa mashahidi kwa wakati na taratibu mbalimbali za kisheria.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akizungumza na Waandishi wa habari (hawapo pichani) katika mkutano na Waandishi wa habari uliofanyika leo Machi 17, 2021.
Pichani ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (katikati), kushoto ni Msajili wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Kevin Mhina na kulia ni Msajili-Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt.Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari (hawapo pichani).(Picha na Innocent Kansha, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni