Jumanne, 13 Aprili 2021

JAJI MKUU ATOA RAI KWA WAKUU WA MIKOA NA WILAYA KUTENDA HAKI

 Na Lydia Churi-Mahakama, Kilimanjaro

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ametoa rai kwa wakuu wa Mikoa na Wilaya kusimamia suala la upatikanaji wa haki kwenye maeneo yao ya kazi ili kupunguza idadi ya mashauri yanayofunguliwa mahakamani.

Akifungua mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na wajumbe wa kamati za Maadili za Mkoa na wilaya katika Mkoa wa Kilimanjaro, Jaji Mkuu alisema mfumo wa utoaji haki huishia mahakamani lakini haki inaanzia hata kwenye taasisi za Serikali.

Akitolea mfano wa ukusanyaji wa kodi mbalimbali za Serikali ambao ni moja ya kazi zinazofanywa na Serikali, Jaji Mkuu alisema mfano huo unagusa moja kwa moja suala la upatikanaji wa haki kwa wananchi.  

Aidha, Jaji Mkuu amewataka viongozi hao wa mikoa na wilaya nchini kuwabana wapelelezi na waendesha mashtaka wafanye kazi zao kwa haraka na weledi ili mashauri yamalizike kwa wakati na haki kutendeka.

Alisema msingi wa kesi unajengwa na wapelelezi na kushinda au kushindwa katika kesi hutokana na waendesha mashitaka na mawakili wa serikali.

“Sheria zimefanyiwa marekebisho makubwa ili kurahisisha ukusanyaji wa ushahidi hivyo hakikisheni inawahimiza wapelelezi kutumia sheria hizo ili kurahisisha suala la upatikanaji” alisisitiza Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu alisema, Sheria ya DNA ipo tangu mwaka 2009 lakini haitumiki katika kesi za ubakaji na kuongeza kuwa kosa linapotokea sampuli hazichukuliwi mapema na wakati huo huo mwathirika anapimwa lakini mtuhumiwa hapimwi mapema wakati tayari sheria imerahisisha ukusanyaji wa ushahidi kwenye kesi za aina hiyo.

Alisema kutotumika kwa sheria hiyo pamoja na ile ya matumizi ya video katika ukusanyaji wa ushahidi wakati mtuhumiwa akihojiwa katika kituo cha polisi na sheria ya kulinda mashahidi kunasababisha Mahakama kutupiwa lawama isizostahili.  

Jaji Mkuu pia amewaomba wakuu wa mikoa na wilaya ambao ni wenyeviti wa kamati za maadili ya maafisa wa Mahakama wa mikoa na wilaya kufuatilia shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mahakama ili waweze kuwaelimisha wananchi masuala yanayohusu mhimili huo.

“Changamoto za Mahakama zinaweza kutafsiriwa na wananchi kuwa ni masuala ya kinidhamu, endapo wajumbe wa hizi kamati watazifahamu watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuwaelezea wanannchi”, alisema.

Alisema kamati za maadili za mikoa na wilaya zinaisaidia Mahakama kuwa huru na kufanya kazi zake kwa haki bila rushwa wala upendeleo. “Jukumu la kamati hizi ni kutunza nidhamu kwa Majaji na Mahakimu huku mkikumbuka kuwa watumishi hawa wana haki zao za msingi za kutosingiziwa wala kulaumiwa bila sababu, alisema.   

Prof. Juma alisema madhumuni ya Tume ya Utumishi wa Mahakama kufanya ziara mkoani humo ni kuona hali halisi ya utekelezaji wa majukumu ya Mahakama, kukutana na wajumbe na kubadilishana uzoefu, kupokea maoni mbalimbali na kusikiliza changamoto zilizopo.

Jaji Mkuu alisema Tume hiyo ni ya kikatiba inayoisaidia nchi katika safari ya kuwa Jamhuri iliyo bora na hivyo mihimili yote ya dola haina budi kuifikisha nchi  kwenye uhuru, haki, udugu na amani.

Tume ya Utumishi ya Mahakama imeundwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 112 kwa lengo la kusimamia mambo muhimu yanayohusu Mhimili wa Mahakama. Wajumbe wa Tume hiyo ni pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania (Mwenyekiti), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji moja wa Mahakma ya Rufani anayeteuliwa na Rais, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, na wajumbe wengine wawili wanaoteuliwa na Rais.

 Baadhi ya kazi za Tume hiyo ni pamoja na kumshauri Mhe. Rais katika uteuzi wa Majaji wa Mahakama Kuu, kumshauri Rais kuhusu masuala ya nidhamu, mishahara na maslahi ya Majaji, na kushauri kuhusu ajira za Mahakimu na kusimamia nidhamu yao.

Tume ya Utumishi wa Mahakama inafanya ziara katika Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara kwa lengo la kuitangaza na kutoa elimu kwa wajumbe wa kamati za Maadili za Mika na Wilaya ambao ni wakuu wa Mikoa na wakuu wa Wilaya.

Wajumbe wa kamati za Maadili za Mkoa na wilaya katika Mkoa wa Kilimanjaro wakiwa kwenye Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama unaofanyika kwa lengo la kuitangaza Tume hiyo, kuwakutanisha wajumbe na kubadilishana uzoefu, kupokea maoni mbalimbali na kusikiliza changamoto zilizopo. Mkutano huo unafanyika katika Chuo cha Uhamiaji mjini Moshi. 
Baadhi ya wajumbe wakiwa kwenye Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama unaofanyika kwa lengo la kuitangaza Tume hiyo, kuwakutanisha wajumbe na kubadilishana uzoefu, kupokea maoni mbalimbali na kusikiliza changamoto zilizopo. Mkutano huo unafanyika katika Chuo cha Uhamiaji mjini Moshi. 
Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya (wa kwanza kulia), mmoja wa wajumbe wa kamati za Maadili za wilaya akiwa pamoja na wajumbe wengine kwenye Mkutano huo. 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni