Na Lydia Churi-Mahakama- Kilimanjaro
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
amewaomba wadau wa Mahakama kuungana na Mhimili huo katika matumizi ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kusogeza haki karibu zaidi na
wananchi.
Akizungumza katika mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama
na wadau wa Mahakama mkoani Kilimanjaro, Jaji Mkuu wa Tanzania ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Tume hiyo aliwaambia wadau hao kuwa Mahakama tayari imeshaingia
kwenye matumizi ya Tehama na mfumo hauwezi kukamilika endapo wadau wake
watakuwa nje ya mfumo huo.
“Mahakama na wadau, wote wanao wajibu wa kutoa haki
kwa wakati, wadau ni sehemu ya mnyororo wa utoaji haki hivyo kukiwa na dosari
yoyote katika mnyororo huo, haki haiwezi kupatikana kwa wakati”, alisema Jaji
Mkuu.
Alisema endapo wadau wa Mahakama watawekeza kwenye
matumizi ya Tehama, wajibu wa utoaji haki utakuwa bora Zaidi. Akitolea mfano wa
janga la ugonjwa wa COVID 19, Jaji Mkuu alisema Mahakama ilifunga vifaa vya
Tehama kwenye Magereza mbalimbali nchini hatua iliyowezesha mashauri mengi Zaidi
kusikilizwa.
Alisema uzoefu uliotokana na janga la COVID unaonesha
ni kwa kiasi gani Teknolojia inaweza kusaidia kurahisisha shughuli za utoaji
haki. Aliongeza kuwa kwa mujibu wa wataalam, dunia inaweza kukumbwa na majanga
mengine, ugonjwa wa COVID si janga la mwisho kuikumba dunia na changamoto ni kwa
namna gani Mahakama na wadau wanaweza kutumia Tehama kuwavusha katika majanga
mbalimbali yanayoweza kutokea.
“Teknolojia inasogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi
na wananchi bila ya kutegemea majengo peke yake, katika karne hii ya 21 haki
haitegemei majengo, mwananchi anaweza kupata taarifa kupitia simu yake ya
mkononi, hana ulazima wa kufika mahakamani”, Jaji Mkuu alisisitiza matumizi ya
Tehama.
Aidha, Jaji Mkuu pia ametoa rai kwa wadau hao kuwa
mstari wa mbele katika kuzibadilisha sheria zilizopitwa na wakati ili ziendane
na hali ya sasa kwani kwa kufanya hivyo wataisaidia jamii kuifikia haki kwa wakati.
“Sheria zetu zilitungwa katika maudhui ya karne ya 20,
dunia ya wakati huo ilikuwa ni dunia ya karne ya 20 hivyo wadau tujisomee,
tubadilike na tuangalie sheria zetu zinazohitaji kufanyiwa marekebisho”,
alisema.
Wakati huo huo, Jaji Mkuu amewataka wadau wa Mahakama
kuongeza matumizi ya vipimo vya vinasaba (DNA) ili kupunguza malalamiko
yanayotokana na mashauri ya ubakaji. Amewataka wapelelezi kutokutumia nguvu
katika kukusanya Ushahidi badala yake watumie sayansi na teknolojia.
Jaji Mkuu alisema Sheria imeruhusu matumizi ya kipmo hicho
muda mrefu sasa lakini hakifanyiki. “Ni nadra sana DNA kuchukuliwa wakati wa
tukio”, alisema.
Kuhusu matumizi ya Video katika kukusanya Ushahidi,
Prof. Juma alisema sheria ilishabadilishwa kuruhusu mahojiano ya mtuhumiwa na
polisi kwa njia ya video ili kuondokana na malalamiko ya kubambikiziwa kesi. Alisema
sheria iko mbele lakini taratibu bado ni zile zile za zamani hivyo amewataka
wadau kuliangalia suala hilo kwa mapana yake.
Tume ya Utumishi wa Mahakama inafanya ziara katika
Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara kwa lengo la kuitangaza na kutoa elimu
kwa wadau wa Mahakama wakiwemo wajumbe wa kamati za Maadili za Mikoa na Wilaya ambao
ni wakuu wa Mikoa na wakuu wa Wilaya.
Tume ya Utumishi ya Mahakama imeundwa kwa mujibu wa
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 113 kwa lengo la kusimamia
mambo muhimu yanayohusu Mhimili wa Mahakama. Wajumbe wa Tume hiyo ni pamoja na
Jaji Mkuu wa Tanzania (Mwenyekiti), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji moja wa
Mahakama ya Rufani anayeteuliwa na Rais, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, na wajumbe wengine wawili wanaoteuliwa na Rais.
Baadhi ya kazi
za Tume hiyo ni pamoja na kumshauri Mhe. Rais katika uteuzi wa Majaji wa
Mahakama Kuu, kumshauri Rais kuhusu masuala ya nidhamu, mishahara na maslahi ya
Majaji, na kushauri kuhusu ajira za Mahakimu na kusimamia nidhamu yao.
Baadhi ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania wakiwa kwenye mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na wadau wa Mahakama mkoani Kilimanjaro. Mkutano huo unalenga kuwakutanisha wadau na Mahakama ili kubadilishana uzoefu, kuitangaza Tume hiyo na kujadili changamoto mbalimbali za utoaji Haki nchini.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo jana mjini Moshi.
Wadau wa Mahakama ya Tanzania wakiwa kwenye mkutano kati yao na Tume ya Utumishi wa Mahakama mkoani Kilimanjaro.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Anna Mughwira akiwa kwenye Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na Wadau wa Mahakama mkoani Kilimanjaro. Mkutano huo unalenga kuwakutanisha wadau na Mahakama ili kubadilishana uzoefu, kuitangaza Tume hiyo na kujadili changamoto mbalimbali za utoaji Haki nchini. Kulia ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni