Na Lydia Churi-Mahakama, Arusha
Jaji Mkuu wa
Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewaomba wadau wa Mahakama
kushirikiakiana na Mhimili huo ili kusaidia kuufikisha kwenye azma yake ya
kutoa haki kwa wakati.
Akifungua Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na
wadau mkoani Arusha, Jaji Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume hiyo amesema
mchango wa wadau ni nguzo muhimu katika mafanikio ya Mahakama hivyo amewaomba kushirikiana
kwa dhati na Mahakama ili kuwezesha Mhimili huo kutekeleza jukumu lake la
msingi la kutoa haki kwa wakati.
“Ushirikishwaji wa wadau ni jambo muhimu na Mahakama
inalizingatia hilo ili kuweza kutekeleza majukumu yake ya upatikanaji wa haki
kwa urahisi”, alisema Jaji Mkuu.
Baadhi ya wadau wa Mahakama ni pamoja na Polisi,
Magereza, Uhamiaji, Takukuru, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya
Wakili Mkuu wa Serikali, Mkemia Mkuu, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Mawakili wa
Serikali na wa Kujitegemea.
Aidha, Jaji Mkuu alisema Mahakama imesimamia nguzo
tatu muhimu katika kutekeleza jukumu lake la msingi ambapo kupitia nguzo ya
kwanza imeweza kujibadilisha na kufuata utawala bora, uwajibikaji na usimamizi
wa rasilimali ili shughuli za utoaji ziwe endelevu.
Alisema kupitia nguzo ya pili ya Mpango Mkakati wake
wa miaka mitano, Mahakama imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa
wakati. Aliongeza kuwa nguzo ya tatu ya Mpango huo ni kuimarisha imani ya
wananchi kuhusu Mahakama yao na mifumo ya utoaji haki.
“Ili tuweze kutoa haki kwa wakati, imani ya wananchi
ni jambo la muhimu na tunalitathmini sana, wananchi ni chimbuko la mamlaka zote
yaani Serikali, Bunge na Mahakama”, alisisitiza.
Naye Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe.
Dkt. Eliezer Feleshi akielezea matarajio ya Mahakama kwa wadau alisema Mahakama
inapenda kuona wapelelezi wakitumia njia za kisayansi katika kufanya kazi yao na
kuondokana na upelelezi wa kimazoea. Alitoa mfano wa matumizi ya vipimo vya DNA
katika mashauri ya jinai na kuongeza kuwa Sheria inaruhusu matumizi hayo.
Jaji Kiongozi alisema wapelelezi hawana budi kushirikiana
na Mahakama ili kukamilisha upelelezi wa mashauri kwa haraka na inatarajia
kuona matumizi ya adhabu mbadala kwenye makosa ya jinai mepesi ili kupunguza msongamano
wa wafungwa na mahabusu magerezani.
Aidha, Jaji Kiongozi alisema suala la Maafisa Ustawi
wa Jamii kuwepo mahakamani hasa kwenye mashauri yanayohusu Watoto ni muhimu na
amesisitiza suala hili kwa kuwa hivi sasa halifanyiki kwa kiwango
kinachotakiwa.
Kuhusu uhusiano wa Mahakama na wadau wake, Dkt.
Feleshi amesema ni mzuri na hauna budi kuendelezwa. Aliongeza kuwa kwa wale
wadau wasiotimiza wajibu wao ipasavyo, Mahakama itaendelea kuwaweka hadharani
ili Umma na wale wanaotafuta haki waweze kuwabaini.
Tume ya Utumishi wa Mahakama inaendelea na ziara
katika Mikoa ya Arusha na Manyara kwa lengo la kuitangaza na kutoa elimu kwa
wadau wa Mahakama wakiwemo wajumbe wa kamati za Maadili za Mikoa na Wilaya
zinazowajumuisha wakuu wa Mikoa na wakuu wa Wilaya.
Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha wakiwa kwenye Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na Watumishi wa kanda hiyo jana mkoani Arusha. Kushoto ni Mhe. Mohamed Gwae na kulia ni Mhe. Robert Kassim.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi (kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru wakiwa kwenye Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na wadau mkoani Arusha,
Baadhi ya Watumishi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Arusha waliohudhuria Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na Watumishi hao uliofanyika kwenye ukumbi wa Hazina Ndogo mkoani Arusha jana.
Wadau wa Mahakama ya Tanzania wakiwa kwenye Mkutano kati yao na Tume ya Utumishi wa Mahakama uliofanyika jana katika ukumbi wa Hazina Ndogo mkoani Arusha jana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni