Na Mary Gwera, Mahakama
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru ametoa rai kwa Naibu Wasajili
na Watendaji wa Mahakama nchini kuendelea kuwajibika ipasavyo katika maeneo yao
ya kazi ikiwa ni pamoja na kuwa na usimamizi thabiti wa bajeti ili kufanikisha
mipango mbalimbali ya Mahakama inayolenga kuboresha huduma ya utoaji haki
nchini.
Akifunga
rasmi Mafunzo Elekezi ya Utunzaji Kumbukumbu kwa Watendaji hao leo Aprili 17,
2021 katika Chuo cha Mipango jijini Dodoma, Mtendaji Mkuu aliwahakikishia
washiriki hao kuwa katika kutekeleza shughuli mbalimbali bajeti ya Mahakama ya
mwaka wa fedha wa 2021/2022 imezingatia mahitaji muhimu ili kuwawezesha
kutekeleza majukumu yao ya utoaji haki kwa wananchi.
“Ni
matumaini yangu mtaongeza bidii na kujitoa zaidi na zaidi ili kufanikisha
majukumu ya kuhakikisha kuwa huduma za Mahakama zinapatikana kwa wakati
unaostahili kwa mujibu wa taratibu na viwango vinavyokubalika,” alisema Bw.
Kabunduguru.
Aidha, Mtendaji
Mkuu aliongeza kuwa pamoja na utekelezaji wa majukumu ya kimkakati aliwataka
Maafisa hao wa Mahakama kuendelea kusimamia na kuhamasisha matumizi bora ya
TEHAMA kila mmoja kwa eneo lake.
“Mahakama
inatarajia kuanza utekelezaji wa mpango mkakati mpya ambapo katika mkakati huo imepanga
kuongeza matumizi ya huduma za ki-elektroniki kwenye shughuli za Mahakama,”
alisisitiza.
Hali
kadhalika, aliwakumbusha Washiriki wa Mafunzo hayo kuendelea kusimamia miongozo
inayotolewa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) ili kuwa na udhibiti bora wa
mifumo mbalimbali ya TEHAMA iliyopo Mahakamani.
Kwa
upande wake, Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma aliwakumbusha
washiriki wa Mafunzo hayo kushirikiana katika kazi kwa kuwa wote wanajenga
nyumba moja.
“Shirikianeni
kutekeleza azma ya utoaji haki kwa wakati, bila kusahau kutekeleza kwa wakati
maagizo yanayotolewa na Viongozi ili kusonga mbele,” alisema Mhe. Chuma.
Msajili Mkuu aliongeza kwa kuwataka Wasajili na Watendaji hao kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi walio chini yao ili kuwapa motisha ya kufanya kazi zaidi.
Katika
mafunzo hayo Washiriki walipitishwa katika mada mbalimbali ikiwemo uhusiano na
umuhimu uliopo baina ya utunzaji kumbukumbu, matumizi ya majalada na uandishi
wa nyaraka mbalimbali, usajili wa mashauri kwa mfumo wa kielektroniki.
Nyingine
ni usimamizi na ukaguzi wa Mahakama, usimamizi wa masuala ya fedha na
kumbukumbu zake kupitia mfumo mpya wa ‘MUSE’ na mifumo ya ndani na usimamizi wa
bajeti.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni