Na Lydia Churi-Mahakama, Manyara
Jaji Mkuu wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume
ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Mahakimu wote nchini
kuwa na nidhamu na kutekeleza majukumu yao ya utoaji haki kwa kuzingatia
Maadili.
Akizungumza na Watumishi wa Mahakama wakiwemo Mahakimu
katika ziara ya ya Tume hiyo mkoani Manyara, Jaji Mkuu amesema majukumu ya
Hakimu ni makubwa kwa jamii na kutokana na majukumu hayo jamii hufuatilia
mwenendo wao hivyo amewaasa kuwa na nidhamu ya hali ya juu ili kujenga imani ya
wananchi kwa Mhimili huo.
“Ukiwa na changamoto ya kutokuwa na nidhamu utatembea
na rekodi yenye dosari wakati wote hivyo zingatieni suala la kuwa na nidhamu ya
hali ya juu”, alisema Jaji Mkuu.
Alisema suala la Maadili ni muhimu kwa Maafisa wa
Mahakama pamoja na watumishi wote wengine wa Mhakama hivyo aliwataka watumishi
hao kuzisoma na kuziishi kanuni za Maadili ili kujenga taswira chanya ya
Mhimili wa Mahakama. Aliongeza kuwa Tume hiyo iliandaa Kanuni za Maadili kwa
Maafisa wa Mahakama zilizoanza kutumika Novemba 20, mwaka jana.
Kuhusu suala la utendaji kazi, Jaji Mkuu alisema
Mahakama ya Tanzania imepewa pongezi na wadau wake kwa kutokana na kuweka
vigezo vya kupima utendaji kazi na kujitathmini kwa watumishi wake hasa Majaji
na Mahakimu.
“Majaji na Mahakimu wamewekewa vigezo vya kupima utendaji
kazi wao ambapo kila Jaji hutakiwa kusikiliza na kumaliza mashauri 220 kwa
mwaka, Hakimu wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya mashauri 250
kwa mwaka na Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo mashauri 260 katika kipindi cha
mwaka mwaka mmoja”, alifafanua Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu pia aliwapongeza watumishi wa Mahakama ya
Tanzania kwa kutekeleza vema maboresho ya huduma za Mahakama kupitia Mpango
Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama (2015/16-2019/21). Alisema maboresho
yaliyofanyika yameleta mabadiliko ya kimtazamo katika utoaji wa huduma na
mabadiliko ya huduma zinazotolewa na Mahakama.
Alisema Mahakama imefanikiwa kutekeleza dhana ya
utoaji haki unaomsikiliza na kumjali Mteja, utafiti uliofanywa na Taasisi ya
Repoa, kuhusu kuridhika kwa mteja kutokana na namna Mahakama inavyotoa
haki ulionesha kuwa asilimia 57 ya
wananchi walirishwa na huduma hizo mwaka 2015 na asilimia 70 waliridhishwa na
huduma za Mahakama mwaka 2019”, alisema.
Tume ya Utumishi wa Mahakama imemaliza ziara katika
Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara iliyokuwa na lengo la kuitangaza na
kutoa elimu kwa wadau wa Mahakama wakiwemo wajumbe wa kamati za Maadili za
Mikoa na Wilaya zinazowajumuisha wakuu wa Mikoa na wakuu wa Wilaya.
Tume ya Utumishi ya Mahakama imeundwa kwa mujibu wa
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 112 kwa lengo la kusimamia
mambo muhimu yanayohusu Mhimili wa Mahakama. Wajumbe wa Tume hiyo ni pamoja na
Jaji Mkuu wa Tanzania (Mwenyekiti), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji moja wa
Mahakama ya Rufani anayeteuliwa na Rais, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, na wajumbe wengine wawili wanaoteuliwa na Rais.
Baadhi ya kazi
za Tume hiyo ni pamoja na kumshauri Mhe. Rais katika uteuzi wa Majaji wa
Mahakama Kuu, kumshauri Rais kuhusu masuala ya nidhamu, mishahara na maslahi ya
Majaji, na kushauri kuhusu ajira za Mahakimu na kusimamia nidhamu yao.
Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Gerald Ndika (katikati) na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (kulia) wakiwa ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara Bw. Joseph Mkirikiti (kushoto) wakati Jaji Mkuu alipomtembea akiwa katika ziara ya Tume ya Utumishi wa Mahakama mkoni humo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni