Na Innocent Kansha – Mahakama Kigoma
Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi ameupongeza Uongozi wa Mkoa
wa Kigoma kwa jitihada zake za kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na
Mahakama ya Tanzania za kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi
wa Mkoa huo.
Akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Bw. Thobias Andengenye alipomtembelea Ofisini kwake mapema
Aprili 21, 2021 Mjini Kigoma, Jaji Kiongozi Dkt. Feleshi alieleza kuridhishwa kwa jinsi Mahakama inavyopewa ushirikiano na Uongozi wa
Mkoa katika masuala ya kiutendaji hasa ya kuanzishwa kwa maeneo mapya ya kiutendaji
wa Mahakama.
“Natambua kuanzishwa kwa
huduma ya Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu katika Mkoa huu, Uongozi wa Mkoa
umeshirikiana nasi kwa kiwango cha hali ya juu na hata wakati tunazindua jengo
la Mahakama Kuu mwaka jana uongozi ulitoa msaada mkubwa katika kuandaa shughuli
ile iliyoongozwa na Hayati Rais Magufuli hatuna budi kutoa pongezi zetu kwa
Uongozi”, alieleza Jaji Kiongozi.
Aidha, Jaji Kiongozi
aliongeza kuwa jukumu moja wapo la Viongozi ni kupima matokeo mathalani kwa
kuanzishwa huduma ya Mahakama Kuu kwa maana ya kusimamia kwa ukaribu Mahakama
za chini kama Mahakama ya Mkoa, za Wilaya na Mwanzo kumeongeza ufanisi na tija
katika huduma ya utoaji wa haki.
"Kwa viwango na vigezo Mahakama ilivyojiwekea
viashiria vinaonyesha matokeo ya kuanzishwa kwa huduma ya Mahakama Kuu Mkoa wa
Kigoma matokeo yake yanalidhisha kwani Viongozi wa Kanda hii wamekuwa mstari wa
mbele wakizunguka maeneo yote kuwajengea uwezo Maafisa wa Mahakama ili kuwaweza
kuendesha na kumudu majukumu yao ya utoaji haki kwa wananchi kwa wakati na kwa
viwango vya kuridhisha wadau wetu," aliongeza Jaji Kiongozi.
Dkt. Feleshi alimweleza
Mkuu wa Mkoa huyo kuwa utendaji wa Masjala Kuu ukitoa masjala 4 maalumu za Ardhi, Kazi, Biashara
na Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi utaona hakuna Masjala yenye mlundikano wa
kesi ukilinganisha na vigezo ambavyo Mahakama ilivyojiwekea vya umri wa
mashauri kukaa Mahakamani ndani ya miezi 24.
Jaji kiongozi pia alitoa
rai kwa Uongozi wa Mkoa na kamati nzima ya usalama inapotimiza majukumu yake itambue
kuwa Mahakama inatoa huduma ya haki kwa wananchi na suala la haki ni jambo la
kiusalama na linahusisha wadau wote muhimu, hivyo akaiomba ofisi ya Mkuu wa
Mkoa kuendelea kusaidia kadri inavyowezekana ili kuleta utengamano katika
shughuli za kiutendaji.
Kwa upande wake Mkuu wa
Mkoa wa Kigoma Bw. Thobias Andengenye ameishukuru Mahakama ya Tanzania kwa
jitihada zake za makusudi kuanzisha huduma ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani
Mkoani Kigoma kwani imetatua changamoto ya muda mrefu ya wananchi wa Mkoa huo
kufuata huduma kwa umbali mrefu mkoani Tabora.
“Huduma hii sasa
inamwezesha mwananchi kutafuta haki karibu kabisa hata kwa ngazi ya juu na ya mwisho
ya kimahakama, imepunguza manung’uniko ya je? nitapata wapi nauli ya kusafiri
kufuata huduma hii huko mkoani Tabora, maswali yote ya wananchi na wadau wa
Mahakama yamepatiwa ufumbuzi”, aliongeza Mkuu huyo wa Mkoa.
Akielezea hali ya
uendeshaji wa Vikao vya Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama Bw. Andengenye
alisema kikao cha hivi karibuni cha kamati hiyo kilichokaa hakikuibua
changamoto yoyote ya kiutendaji wa shughuli za Mahakama kwa kiasi kikubwa hali
ni shwari na hakukubainika changamoto ya maadili na ya kiutendaji kwa
Maafisa hao.
Mkuu wa Mkoa alisema
changamoto iliyopo ni ukosefu wa elimu na uelewa mdogo wa taratibu za
kimahakama kwa baadhi ya wadau, hivyo wanashirikiana na Mahakama kutoa elimu kwenye
maeneo hayo ili wananchi wapate uelewa katika kutafuta haki zao.
Wakati huo huo Jaji Kiongozi alipata wasaa wa kukutana na Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma na kupokea taarifa ya kiutendaji na kutoa salamu za Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni