Ijumaa, 23 Aprili 2021

JAJI KIONGOZI AZINDUA JENGO LA MAHAKAMA YA WILAYA KASULU; ASISITIZA USHIRIKIANO

 Na Innocent Kansha, Mahakama Kigoma

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi ametoa rai kwa wadau wote wa haki Jinai na Madai kuunga mkono jitihada za Mahakama ya Tanzania za kuboresha Miundombinu kwa kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi ili kuondoa mlundikano wa mashauri na kupunguza malalamiko yasiyo na tija kwa ustawi wa jamii.

Akizindua rasmi Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Aprili 22, 2021, Jaji Kiongozi Dkt. Feleshi aliwakumbusha wadau na wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwani Mahakama ni sehemu ya kichocheo cha maendeleo na ustawi wa jamii.

“Mnapoiangalia Mahakama sio ya Jaji Mkuu wala ya Jaji Kiongozi ni yetu sote wananchi, sio ya mtu, kwa uzuri wake isitumike na wadau wachache kama kichaka cha kupaki kesi na kuchelewesha haki za watu, lengo letu ni kuhakikisha tunashirikiana na wadau wote kumaliza mashauri kwa wakati na kuondoa malalamiko yasio na tija kwa wananchi”, alisistiza Jaji Kiongozi.

Aidha, Jaji Kiongozi aliwataka watumishi wa Mahakama kufanya kazi kwa bidii kwa kutoa huduma nzuri kwa wateja kama ambavyo wakifanya siku zote.

Dkt. Feleshi aliwakumbusha wadau kwamba ujenzi wa jengo hilo zuri na la kisasa ulitokana na sababu kadhaa zikiwemo Mahakama ya Wilaya kutokuwa na jengo lake tangu mwaka 1961 ilipoanza kufanya kazi. Hata jengo lililokuwa likitumika halikukidhi mahitaji ya watumiaji.

Akifafanua zaidi, Jaji Kiongozi alieleza kuwa, Mahakama ya   Wilaya ya Kasulu inahudumia pia Wilaya ya Buhigwe iliyoanzishwa mwaka 2012. Hivyo basi, Mahakama ya wilaya Kasulu inahudumia wananchi wapatao laki 888,380, Wilaya ya Kasulu ikiwa na wananchi 634,038 na Buhigwe wananchi 254,342, kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012.

"Kuogezeka kwa idadi ya mashauri katika ngazi ya wilaya, kwa wastani wa usajili wa mashauri 700 kwa mwaka, umuhimu wa kuwa na jengo linalozingatia ushiriki wa wadau wengine wa utoaji haki, kama vile Mawakili, Waendesha Mashtaka na Maafisa huduma kwa jamii na uhitaji wa Jengo linaloweza kuwa na mifumo ya TEHAMA na pia kumbi za Mahakama ni muhimu ili kuongeza ufanisi na uwazi katika usikilizaji mashauri, alieleza Jaji kiongozi.

Jaji Feleshi alieleza kuwa, moja ya mikakati iliyowekwa na Mahakama ya Tanzania ni kuhakikisha kuwa kila eneo jipya la kiutawala linaloanzishwa kunajengwa Mahakama, kwa kuwa huduma za Mahakama ni muhimu kama ilivyo huduma nyingine za umma. Serikali inaporidhika na vigezo vya kuanzishwa kwa Mkoa, Wilaya, Tarafa na Kata, vigezo hivyo huleta umuhimu wa kusogezwa kwa huduma za Mahakama karibu na wananchi.

Hivyo basi, kwa kutambua umuhimu huo, na kwa kutambua kwamba Mkoa wa Kigoma unazo Wilaya tatu mpya za Uvinza, Buhigwe na Kakonko ambazo kimahakama bado zinahudumiwa na Mahakama za Wilaya ya Kigoma, Kasulu na Kibondo; Mahakama ya Tanzania tayari imetangaza zabuni ya ujenzi wa Mahakama za Wilaya, Uvinza, Buhigwe na Kakonko, ambapo ujenzi wake utaanza muda wowote mara baada ya taratibu za manunuzi kukamilika, alisema Jaji Kiongozi.

Aidha, nafahamu kuwa katika Mpango wa miaka mitano ya Maendeleo ya Miundombinu ya Mahakama, Mkoa wa Kigoma pia utanufaika na ujenzi wa Mahakama nne (4) za Mwanzo, ikiwemo Mahakama ya Mwanzo Heru Juu iliyopo umbali wa Kilometa tisa (9) kutoka hapa tulipo ambayo itasaidia kupunguza mlundikano wa mashauri katika Mahakama ya Mwanzo Kasulu Mjini. Mahakama nyingine za Mwanzo zitajengwa Manyovu katika Wilaya ya Buhigwe, Nguruka katika Wilaya ya Uvinza na Kigoma katika Wilaya ya Kigoma.

Jaji Kiongozi alimuomba Mhe. Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya kupitia Kamati za Mikoa na Wilaya za Maadili ya Mahakimu kuhakikisha kamati hizo zinatimiza wajibu wake katika kulea, kuonya na kuchukua hatua.  Aidha muendelee kuwaelimisha wananchi   wajibu wa kamati hizi na utaratibu wa kuwasilisha malalamiko pale yanapotokea matukio au mienendo isiyofaa kwa Mahakimu katika utekelezaji wa majukumu yao ya msingi ya utoaji haki.

Kwa upande mwingine, Jaji Kiongozi aliziagiza Kamati za Nidhamu kwa Watumishi wasio Maafisa wa Mahakama zilizokasimiwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama (Kifungu Na.33 (1) cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama ya mwaka 2011 na Kanuni ya 19 ya Kanuni za Uendeshaji wa Mahakama za mwaka 2021) jukumu la usimamizi wa nidhamu katika Kanda, kuhakikisha zinafanya kazi iliyokusudiwa kwa weledi na ufanisi.

Kwa upande wake, Mkoa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Thobias Andengenye aliushukuru Uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kurasimisha rasmi uzinduzi wa Jengo hilo la kimkakati la Mahakama la kutoa haki kwani ilikuwa ni kiu ya muda mrefu ya wanakasulu na Kigoma kwa ujumla.

“Nimatarajio yetu na hamu kubwa kuona kuwa Uongozi wa Mahakama unaendelea kusogeza huduma hizi za utoaji haki karibu na wananchi hasa kwa Wilaya zilizobakia zisizo na huduma hii kama vile Uvinza, Buhigwe na Kakonko pia upatikanaji wa Mahakama hizi utasaidia kupunguza umbali wa kusafiri kwa wananchi kwenda kutafuta haki na kupunguza wingi wa mashauri ya Wilaya moja inayolazimika kubeba mashauri ya Wilaya mbili na hatimaye kupunguza muda wa mashauri kukaa Mahakamani vyote hivi kwa pamoja vitasaidia kuinua uchumi wa wananchi kwani watatumia muda mwingi kufanya kazi za uzalishaji mali”, alieleza Mkuu wa Mkoa

Kamishna Andengenye aliongeza kuwa ujenzi wa Mahakama hizi utakuza hali ya usalama wa wananchi na itawezesha Jamii kutafuta haki kwa njia stahiki bila kutumia njia za mkato kwakuwa Mahakama ipo karibu hali ambayo itasaidia kupunguza vipigo, Imani za kishirikina, kujeruhiana kwani sasa mtu atafahamu pa kukimbilia endapo hajaridhika na jambo fulani.

“Uwepo wa Mahakama hii utaongeza ustaarabu, tunategemea nchi ya uchumi wa kati iwe ni nchi ambayo pia ustaarabu wake umekuwa na uwepo wa vyombo vya kutoa haki. Ninawaomba wanakasulu na Kigoma kwa ujumla wake kuendelea kuzitumia Mahakama kutatua migogoro miongoni mwenu badala ya kujichukulia sheria mikononi,alisisitiza Kamishna Andengenye.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma Mhe. Ilvin Mugeta alisema watumishi wa Mahakama Kanda ya kigoma ni waadilifu, wachapa kazi, nadhifu na wanatekeleza majukumu yao kabla ya kudai haki zao na ushahidi katika hilo ni takwimu za mashauri zinazoonyesha kuwa mashauri katika Mahakama za Mwanzo hayadumu zaidi ya miezi mitatu (3) na ifikapo Desemba 31 Mahakama za Mwanzo kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo takwimu zake husomeka mashauri sifuri.

Aliongeza kuwa wastani wa umri wa mashauri kukaa Mahakamani kwa ngazi ya Mahakama za Wilaya na Mkoani ni miezi mine (4) isipokuwa kwa mashauri yale wasiokuwa na mamlaka nayo, kwa upande wa Mahakama Kuu wastani ni miezi sita (6) hii ni rekodi ya kipekee ambayo tutaendelea kutamba nayo na hatutegemei kuvunjwa na mtu yeyote, aliongeza Jaji Mugeta.

Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Moses Mashaka alisema  mradi huo umetekelezwa na Mkandarasi Moladi Tanzania Ltd chini ya mshauri elekezi(Consultant) Aru Built Environment Consulting Company LTD (ABECC) ambayo ni kampuni ya Chuo Kikuu Ardhi kwa kushirikiana na Norplan Tanzania Limited. Kampuni ya Chuo Kikuu Ardhi katika mradi huu wanatoa ushauri kwenye maeneo ya usanifu majengo na ukadiriaji majenzi na kwa upande mwingine,Kampuni ya Norplan wao wanahusika zaidi katika ushauri wa mambo ya uhandisi.Gharama za mradi ni Tsh 658,243,593.00. Kuongezeka.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (wa kwanza kushoto) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Jengo la Mahakama ya Wilaya Kasulu mkoani Kigoma. Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Thobias Andengenye (wa pili kulia), wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Ilvin Mugeta, na kwanza kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Athuman Matuma. Uzinduzi wa jengo hilo umefanyika Aprili 22, 2021.

 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akizungumza na wananchi (hawapo pichani) walioshiriki hafla ya uzinduzi rasmi wa Jengo la Mahakama ya Wilaya Kasulu mkoani Kigoma. Kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Kigoma Mhe. Ilvin Mugeta, katikati ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma Mhe. Athuman Matuma.

Muonekano wa jengo la Mahakama ya Wilaya Kasulu lililozinduliwa rasmi na Jaji Kiongozi.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (wa kwanza kulia) akifunua kibao kuashiria uzinduzi rasmi wa jengo la Mahakama ya Wilaya Kasulu. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kamishna Thobias Andengenye.

   Baadhi ya wananchi waliohudhuria hafla ya uzinduzi rasmi wa Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wakifuatilia shughuli hiyo.

       Meza Kuu katika picha ya Pamoja na Watumishi wa Mahakama Kasulu.     

 (Picha na Innocent Kansha,  Festo Sanga - Mahakama.)







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni