Na Mary Gwera, Mahakama
Wadau
wa Kamati ya Kitaifa ya Kusukuma Mashauri
ya Jinai nchini kila mmoja kwa nafasi yake wametakiwa kusimamia sheria ambazo
hazitoi mwanya wa kuwa na mlundikano wa mashauri Mahakamani na msongamano wa
mahabusu gerezani.
Akizungumza na Wajumbe wa Kamati hiyo alipokuwa
akifungua rasmi kikao chao mapema Aprili 23, 2021, Msajili Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma alisema kuwa kumekuwa na ucheleweshaji wa
upepelezi hali inayosababisha mlundikano wa mashauri na mlundikano wa Mahabusu.
“Bado
hatusemwi vizuri kwenye suala la mlundikano wa mashauri unaosababisha
msongamano wa mahabusu gerezani kwa sababu mbalimbali kama vile kutokamilika
kwa upelelezi kwa wakati, Upatikanaji mashahidi, idadi ndogo ya rasilimali watu
kama vile Majaji na Mahakimu,waendesha mashtaka na kadhalika,” alisema Mhe. Chuma.
Alisema
kuwa changamoto zilizoainishwa zinaweza kuepukwa iwapo kila mdau atafuata
sheria, miongozo na taratibu zilizowekwa ili kuwezesha mchakato wa utoaji haki kufikika kwa wakati na ufanisi.
Msajili Mkuu aliongeza kuwa ili kudhibiti hayo Wadau wote wanatakiwa kuwa na utayari wa kutoa huduma na kuwajibika kila mmoja kwa nafasi yake na kutumia mamlaka tuliyonayo hata pale inabobainika kuwepo mashauri mahakamani yasiyo na tija.
“Kwa mfano kusimamia vifungu
vya 91,98,225 vya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai kwa upande wa
waendesha mashtaka na Mahakama. Mamlaka ya Mkuu wa Kituo kutoa adhabu ya faini;
kwa mujibu wa kifungu 170 (6) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (the
Criminal Procedure Act (Cap 20 RE 2019),” alibainisha.
Asisitiza
kuwa kwa mashauri yasiyokuwa na ushahidi wa kutosha, yanatakiwa kuwasilishwa maombi
maalumu mahakamani ya kuomba amri ya uangalizi kwa mujibu wa vifungu 70-73 vya Sheria
ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (the Criminal Procedure Act (Cap 20 RE 2019).
Kwa upande wa Magereza, Mhe. Chuma alishauri kuwa na Matumizi ya adhabu
mbadala ambapo Afisa Ustawi wa Jamii anawajibika kupendekeza adhabu mbadala kwa
watuhumiwa waliotiwa hatiani kwa makosa ambayo adhabu husika ni chini ya miaka
3, kama inavyobainishwa katika kifungu 3 (1) cha Sheria: The Community Services
Act (Cap. 291 R.E. 2019).
“Hivyo, kupitia kikao hiki ni matarajio yangu mtatoa mapendekezo zaidi yatakayowezesha kuendeleza maboresho
ya huduma ya utoaji haki nchini ili wananchi waweze kunufaika na huduma hiyo
iliyopo kikatiba,” alisisitiza.
Msajili
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (aliyesimama) akizungumza na
Wajumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Kusukuma Mashauri ya Jinai nchini (hawapo
pichani) alipokuwa akifungua rasmi kikao cha Kamati hiyo katika Ukumbi wa katika
ukumbi wa mafunzo wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto jijini Dar es Salaam,
Aprili 23, 2021. Kushoto ni Mhe. Sharmillah Sarwatt, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni