Na Mwandishi wetu, Mahakama-Singida
Mahakimu Wakazi
wa Mahakama ya Mkoa wa Singida wametakiwa kutumia muda mwingi kujifunza vitu
vipya ili kuongeza ujuzi katika kazi yao ya utoaji haki kwa wananchi.
Akizungumza
wakati akifungua rasmi kikao kazi kilichojumuisha Mahakimu wapatao 40 wa Mkoa
huo, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Jaji George Masaju alisema kuwa
mafunzo na uzingatiaji wa weledi katika kufanya kazi ni vitu muhimu katika
kuboresha huduma ya utoaji haki.
Mhe. Jaji
Masaju ambaye alifungua Mafunzo hayo kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu, Kanda ya Dodoma aliwaambia Mahakimu hao kuwa mada za kikao kazi hicho
zitumike kuboresha huduma kwa wananchi.
Katika kikao
hicho Mahakimu hao walipatiwa mada mbalimbali ikiwa ni Pamoja na uendeshaji wa
mashauri ya uhujumu uchumi, upokeaji, utunzaji na uondoshaji wa vielelezo,
uendeshaji na usimamiaji wa mashauri ya mirathi kwa Mahakama za Mwanzo na
Wilaya, Makosa yanayojirudia katika uendeshaji wa mashauri ya unyanyasaji wa
kijinsia.
Mada nyingine
ni uendeshaji wa mashauri ya ndoa na talaka, uendeshaji wa mashauri ya madai
kwa Mahakama za Mwanzo, maadili ya Mahakimu na utekelezaji wa hukumu kwa
Mahakama za Mwanzo na Wilaya.
Aidha, katika
kipindi cha kikao hicho cha siku tatu kilichofanyika kuanzia Aprili 22 hadi
Aprili 24, 2021, ilifanyika pia semina ya Mahakimu Wafawidhi wa Wilaya za mkoa
wa Singida juu ya uongozi, ukaguzi, usimamizi na mahusiano.
Kikao kazi hiki kiliandaliwa na Ofisi ya Hakimu
Mkazi Mfawidhi Mkowa Singida kwa kushirikiana na Chama cha Majaji na Mahakimu
Tanzania (JMAT) tawi la Singida, ambapo pia tawi hilo lilifanya kikao chao cha
robo mwaka.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni