Na Innocent Kansha – Mahakama Njombe
Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi ametoa wito kwa Mahakimu na
Wasajili kote nchini kuacha kupokea ama kusajili Mahakamani mashauri yasiyo
kuwa na tija ili kupunguza kulundika kesi zisizo na msingi kwa lengo la
kuwapunguzia wananchi usumbufu.
Akizindua rasmi Jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya ya Njombe mnamo Aprili 27, 2021 Mhe. Dkt. Feleshi alisema kwa kufanya hivyo Mahakama itaendelea kuchochea uchumi na kuleta amani kwa wananchi.
"Hakimu au Msajili unapoletewa hati ya shauri jipya liwe la Madai au Jinai unatakiwa upokee shauri lenye sifa ya kusikilizwa na kama shauri halikidhi vigezo unatakiwa kutumia amri za awali “Initial Orders” kwa mujibu wa sheria kulimaliza shauri hilo lililopo mbele yako ama kwa kulirudisha likafanyiwe marekebisho au likafanyiwe upelelezi wa kina," alisema Mhe. Jaji Kiongozi.
Aliongeza kwa kusema kuwa kabla ya kutoa amri ya kuita watu Mahakamani, inabidi kujiuliza kama hati ya madai inaeleweka na kwa upande wa jinai Hakimu ni vyema kutumia sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai kuona kama shauri linakidhi vigezo vya kupokelewa na kusajiliwa Mahakamani, hii itasaidia kupunguza mashauri kukaa Mahakamani muda mrefu pasipo kuwa na ulazima bila kusikilizwa.
Jaji Kiongozi alisema ni
rai yake kwa Mahakimu kuwa yale mashauri ya jinai yasiyokuwa ya makosa makubwa
yanapopokelewa Mahakamani siku hiyo hiyo mshitakiwa asomewe mashitaka na hoja
za awali ili kesi ianze kusikilizwa wakati huo huo.
Aidha, Jaji Kiongozi
aliongeza kuwa Mahakama kwa sasa itaanza kushughulika na Mahakimu wanaopokea
kesi sizio na hadhi ya kupokelewa Mahakamani kwani eneo hili ni moja ya maeneo
ya kiukaguzi na kwa kutambua kuwa Mahakama inao wajibu wa kutoa elimu kwa watu
wanaoleta kesi za namna hii kwa kutoa ufafanuzi wa kwa nini mashuri ya namna
hiyo yasipokelewe Mahakamani kupitia Maafisa Masjala.
Jaji Kiongozi alitumia
wasaa huo kutoa ushauri kwa wadau wa Mahakama kuwa kila eneo lenye mamlaka ya
kiutawala na idadi kubwa ya watu kwa maana ya makazi mengi kuwe na gereza dogo
la Mahabusu ili kuisaidia Mahakama kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi
na wananchi kwani Mahakama kama taasisi tayari inayo miundombinu ya kutosha ya
kusaidia kutoa huduma.
"Ikumbukwe kwamba kabla ya
kuanzishwa kwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe mwaka 2012, kupitia Tangazo la Serikali Na. 9 la tarehe
01/03/2012 wananchi wa hapa Njombe na wilaya zake, ambazo ni Njombe,
Ludewa, Makete na Wanging’ombe, walilazimika kusafiri umbali wa kilomita 223
kufuata huduma za Mahakama ngazi ya Mkoa, mkoani Iringa," aliongeza Jaji
Kiongozi.
Mhe.Jaji Dkt. Feleshi, aliongeza kuwa umbali huo ulikua mrefu na wananchi waliathirika kwa kutumia muda wao mwingi kutafuta huduma za Mahakama, muda ambao wangeutumia katika shughuli zao za kiuchumi na kijamii. Lakini pia, umbali huo kwa namna moja au nyingine uliwakatisha tamaa baadhi ya wananchi kufuatilia haki zao Mkoani Iringa na wengine hawakuweza kumudu gharama za kujikimu, hivyo kukosa haki zao.
Wananchi walio wengi katika Mkoa huu ni Wakulima, wafanyabiashara na Wafugaji, jamii ambayo kwa hakika inahitaji muda mwingi ili waweze kujikita katika shughuli zao za kiuchumi. Uwepo wa jengo hili jipya ni nafuu na ukombozi kwa wananchi wote wa Njombe kwani litaokoa muda na fedha ambazo wanachi walikuwa wakipoteza hapo awali, aliongeza Dkt. Feleshi.
Akiendelea kufafanua Jaji Kiongozi alisema moja ya mikakati iliyowekwa na Mahakama ya Tanzania ni kuhakikisha kuwa kila eneo jipya la kiutawala linaloanzishwa, kunajengwa Mahakama, kwa kuwa huduma za Mahakama ni muhimu kama ilivyo huduma nyingine za umma. Serikali inapoanzisha Mkoa, Wilaya, Tarafa na hata Kata mpya ni kwa sababu kwamba wananchi wa maeneo hayo wanahitaji huduma za Serikali kwa ukaribu na wepesi zaidi. Vigezo hivyo vinaonesha pia umuhimu wa kusogezewa kwa huduma za Mahakama karibu na wanachi.
Kwa sasa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe wanasajili wastani wa mashauri 524 kwa mwaka, pia Mkoa huo una mashauri mengi ya mauaji ambayo husikilizwa na Mahakama Kuu. Jengo hili linayo nafasi ya kutosha kuwezesha Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu kuendesha vikao vya Mahakama Kuu bila tatizo lolote.
“Natoa rai kwa watumishi wa Mahakama kwamba, majengo haya ya kisasa na miundombinu bora, iambatane na upatikanaji wa huduma bora kwa mwananchi. Niwasihi watumishi wenzangu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe na Mahakama nyingine hapa nchini kubadili mienendo na tabia ambazo zinakiuka miiko na maadili ya kazi kwa watumishi wa umma”, alisisitiza Dkt. Feleshi.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Njombe Eng. Lubilya Marwa akitoa salamu za mkoa aliushukuru Uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kukamilisha ujenzi wa miradi mitatu (3) ya majengo ya kisasa ya Mahakama katika Wilaya tatu kati ya nne za Mkoa wa Njombe.
“Uzinduzi wa Mahakama hizi tatu za Njombe, Makete na Wanging’ombe kwetu sisi ni tukio la kihistoria kwa kipindi kirefu Mkoa umekuwa ukifanya kazi zake kwenye mazingira magumu si kwa Mahakama tu hata Taasisi zingine na sasa Muhimili wa Mahakama utafanya kazi katika mazingira bora na rafiki”, alisema Mkuu wa Mkoa Eng. Marwa.
Eng. Marwa aliongeza kuwa ni imani ya Uongozi wa Mkoa kuwa hata Wilaya ya Ludewa iliyosalia na yenye changamoto kubwa itafikiliwa na kutengewa bajeti ili nayo iweze kupata Jengo lake la Mahakama hali itakayo imarisha utendaji wa shughuliza zake za kimahakama.
Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa Mhe. Pentelni Mlisa Kente alisema Mahakama ya Tanzania imepitia nyakati ngumu na historia ndefu kuhusu suala la majengo nyakati fulani Mahakama ilikuwa ikitoa huduma zake kwa kutumia majengo ya Chama Cha Mapindunzi hadi ilipofika mwaka wa 1992 kulipoanzishwa Vyama Vingi vya Siasa, Mahakama ikanza kusaka hifadhi huku na huku.
“Sisi kama Mahakama leo tunayo furaha sana kupokea jengo hili la kisasa nadhani hata wewe Mkuu wa Mkoa furaha uliyonayo haiwezi kulinganishwa na sisi wanamahakama kwa sababu kuna msemo unasema ‘Huwezi kulia msibani ukamzidi mama wa marehemu”, alisisitiza kwa bashasha Jaji Mfawidhi.
Naye Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Martin Chuma aliwaomba watumishi wa Mahakama na wadau wote watakao tumia jengo hilo la kisasa kufanya kazi kwa bidii na huduma wakazotoa zisawiri muonekeno wa jengo husika, ikiwa ni pamoja na kutenda kazi kwa kuzingatia viapo vyao.
Muonekano wa jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Njombe lililozinduliwa rasmi na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi Aprili 27, 2021.
Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akifunua kitambaa kuashiria uzinduzi rasmi wa Jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe na
Mahakama ya Wilaya Njombe, Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mwandisi Lubilya
Marwa (wa katikati aliyeshika kitambaa) na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya
Iringa Mhe. Panterine Kente akishuhudia (wa kwanza kushoto).
Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akiteta jambo na
mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mwandisi. Lubilya Marwa (wa pili kulia) wakati wa hafla ya uzinduzi, wengine ni
Baadhi ya Wananchi waliohudhuriauzinduzi
rasmi wa Jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe na Mahakama ya Wilaya Njombe wakisikiliza hotuba ya Mgeni Rasmi (hayupo pichani)
Picha na Innocent Kansha - Mahakama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni